MBOWE NA WENZAKE 8 WASHINDWA KUJITETEA MAHAKAMANI…..KESI YAPIGWA KALENDA







Viongozi
9 wa CHADEMA, akiwemo Mwenyekiti  wake Freeman Mbowe wameshindwa kuanza
kujitetea katika kesi ya uchochezi inayowakabili Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu kwa sababu mawakili wanaowatetea wanasimamia kesi Mahakama
Kuu ya Tanzania.




Leo
viongozi hao 9 walitarajia kuanza kujitetea baada ya Mahakama hiyo
kuwakuta na kesi ya kujibu kutokana na ushahidi wa mashahidi 8
uliofungwa na Upande wa Mashitaka.

Wakili
Gaston Garubindi amedai hayo leo Jumanne Septemba 17, 2019  akieleza
kuwa maelekezo aliyopewa na wakili Peter Kibatala anaomba shauri hilo
liahirishwe.

“Wakili
Profesa Safari (Abdallah) yuko Mahakama Kuu Shinyanga mbele ya Jaji
Mkeha na Kibatala yuko Mahakama Kuu mbele ya Jaji Tiganga baada  ya
kupata wito wa dharura jana kutakiwa afike mahakamani hapo leo,” amedai
wakili Garubindi.

Wakili
Garubindi amedai wakili mwingine katika kesi hiyo, Hekima Mwasipu yuko
Mahakama Kuu Tanga kwenye kesi ya madai namba 7/2019 mbele ya Jaji
Mruma.

Sababu
nyingine iliyoelezwa na wakili Garubindi ni mshtakiwa wa pili, mbunge
wa Iringa Mjini, Mchungaji  Peter Msigwa na mshtakiwa wa nane, mbunge wa
Tarime Vijijini, John Heche wamefiwa na ndugu zao hivyo wanafanya
taratibu za kwenda kwenye mazishi.

Wakili
mkuu wa Serikali, Faraji Nchimbi alipinga sababu hizo kutokana na
kutoelezwa Profesa Safari yupo katika kesi gani, sambamba na barua ya
wito.

Kuhusu
Mchungaji Msigwa na Heche kusafiri, amesema kuna haja ya kusikia kutoka
kwa washtakiwa wenyewe pamoja na kupata uthibitisho ikiwemo cheti kwa
ajili ya kumbukumbu ya mahakama.

Hakimu
Simba baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili alieleza
kutoridhishwa kuahirisha kesi hiyo kwa siku 20 na kuipanga kuendelea
Septemba 24 hadi 27 na Oktoba 1 hadi 3, 2019.