Veta ishirikishwe katika sekta ya madini ili kuongeza wataalamu.

Mwenyekiti wa Wachimbaji Madini Mikoa ya Dar es salaam na Pwani Josephat Mkombachepa

Egidia Vedasto 

Arusha

Wadau wa sekta ya Madini Nchini wametambua umuhimu wa kuvishirikisha vyuo vya ufundi stadi kwa maana ya kuwapa nafasi katika makampuni ili waongeze ujuzi na ubobezi katika fani zao.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Jukwaa la Tatu la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini Mwenyekiti wa Wachimba Madini Mikoa ya Dar es salaam na Pwani Josephat Mkombachepa, amesema ni dhahiri mapinduzi makubwa yataenda kuonekana katika sekta ya madini kutokana na upeo walioupata katika jukwaa hilo.

Aidha ameeleza umhimu wa kushirikiana kati ya makampuni ya uchimbaji, viwanda vya uzalishaji bidhaa za migodini na vyuo vya ufundi stadi nchini ili kuongeza wataalam watakaosaidia kuleta ushindani wa kitaalam katika soko la sekta madini.

” Kuna umuhimu mkubwa wa kuangalia viwanda vinavyozalisha bidhaa za migodini ziwe na kiwango cha kukubalika, kuwepo na mawasiliano kati ya makampuni ya uchimbaji na viwanda pia wataalam  wabobezi katika masuala ya uzalishaji viwandani ili kuepuka uzalishaji wa bidhaa zisizo na kiwango na kusababisha hasara kwa makampuni” amesema Mkombachepa.

Naibu Waziri wa Madini Dkt Steven Kiruswa akifunga jukwaa hilo, amesema serikali imepokea maazimio yote na itaendelea kuyafanyia kazi kwa mustakabali wa kukuza uchumi wa Wananchi na Taifa kwa ujumla.

“Tunatambua umuhimu wa sekta ya madini, imechangia pakubwa kuongeza pato la taifa, kuongeza ajira na kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja, niahidi sisi kama wizara tutazingatia maazimio yote, na hilo la kuzalisha wataalam watakaofanya kazi katika viwanda vya kuzalisha bidhaa za madini tutashughulika nalo” amesema.

Dkt.Kiruswa amesema katika jukwaa lijalo wataalika nchi jirani hasa zile zinazofanya vizuri katika sekta ya madini kama Kongo na Zambia ili kubadilishana uzoefu na kushauriana katika masuala ya uwekezaji.

Hata hivyo Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Magharibi inayoundwa kwa ya Tabora, Simiyu Shinyanga na Kigoma Asanterabi Kanza, ameeleza kwamba umefika wakati wa kuboresha mitaala ya kozi zinazotolewa ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia lakini pia kuongeza ushindani kati ya wazawa na wageni.

” Ni wakati wa kuimarika kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Madini, Wizara ya Viwanda na Biashara na Wizara ya Elimu ili kwa pamoja kuwa na maazimio yatakayofanya mageuzi makubwa katika sekta ya madini”amesema Kanzi

Sambamba na hayo Mkuu wa chuo cha Veta mkoa wa Shinyanga Magu Mabelele amesema chuo hicho ni cha pekee nchini kwa uzalishaji wa Wataalam wa uchimbaji madini na uongezaji thamani madini ambao huendesha mitambo inayotembea.

“Wataalamu hao hufanya kazi katika viwanda vya mbolea, viwanda vya sukari na migodini kwa maana ya kuchimba na kutengeneza mitambo ya uchimbaji” amesema.

Chuo chetu ni cha pekee nchini kinachotoa mafunzo ya ukataji na ung’arishaji wa madini ya vito kama Tanzanite na Rubi na wadau wa sekta ya Madini wameshuhudia namna tunavyofanya kazi” amesema Mabelele.

Wadau wa VETA walioshiriki katika Jukwaa la Tatu la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini Jijini Arusha_
Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kaskazini Monica Mbelle (kushoto)

Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kaskazini, Monica Mbelle ameiomba Wizara ya Madini na wadau wengine kutoa nafasi kwa wanafunzi kujifunza katika makampuni yao na kuwawezesha kwenda kuongeza ujuzi katika vyuo vya nje ili kuwaongezea ujuzi, ubunifu na weledi katika utendaji kazi.

“Nawaomba ikiwezekana, kila kampuni litoe ufadhili kwa baadhi ya wanafunzi   wakaongeze elimu katika vyuo vya nje au kuleta wataalam hapa nchini kwa lengo la kubadilishana uzoefu” amesema Mbelle.

Naibu Waziri wa Wizara ya Madini, Dkt . Steven Kiruswa akiwa katika picha ya pamoja na watendaji mbalimbali walioshiriki Jukwaa la tatu la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini nchini.