Wakazi kutoka mikoa ya kanda ya Kaskazini wakitembelea mabanda katika viwanja vya nane nane, Themi Jijini Arusha |
Na Mahmud Ahmed, APC BLOG, ARUSHA
SERIKALI imewataka watanzania kuanza uzalishaji wa mazao ya asili ikiwemo uvuvi kutokana na uhitaji mkubwa wa mazao hayo kidunia na kuwepo kwa soko la uhakika.
Mtaalam kutoka Wizara ya mifugo na Uvuvi Fredrick Francis akitoa maelezo katika banda la wizara hiyo katika viwanja vya Nanenane Themi jijini Arusha |
Hayo yamelezwa na Mtaalamu wa Mifugo na Uvuvi kutoka wizara wa mifugo na uvuvi Fredrick Frances alipokuwa akizungumza na wananchi waliotembelea banda la wizara ya mifugo na uvuvi katika viwanja vya Nane nane Themi, jijini Arusha.
Anasema Serikali imekuwa ikipokea maombi mengi kutoka nchi mbalimbali duniani kuhusu kuhitaji mazao ya uvuvi, hususani vyakula vinavyotokana na mazao ya bahari lakini wamekuwa wakikosa majibu kutokana na upungufu wa mazao hayo.
Frances anasema mazao ya uvuvi yamekuwa na soko kubwa duniani kuliko biashara nyingine ambazo baadhi ya watu wamekuwa wakilazimisha kuzifanya wakiamini kuwa watapata faida kubwa na mapema.
Anasema kwa kuzingatia ukweli huo, wananchi wanatakiwa kupata elimu ili wajikite katika ufugaji ili waweze kujikwamua kiuchumi na wachangie pato la taifa kupitia sekta ya uvuvi.
”Watu wanalalamika umaskini lakini kuna fursa nyingi sana katiak ujasiriamali hasa katika sekta ya uvuvi na mifugo, Sisi tunaomsaidia mheshimiwa Rais tunawajibu wakuwaonesha wananchi fursa hizo,” anasema.
Anasema baada ya hivi sasa Serikali kufanikiwa kutokomeza tatizo la uvuvi haramu kwa asilimia 90, ni muda pekee kwa viongozi kusimamia utoaji elimu kwa wananchi kuhusu ufugaji na uvuvi ili waweze kuingia katika biashara hiyo.
“ Nikiwa kama mtaalam wa Wizara hii, ningependa kuwaomba wataalam wa na maofisa wa idara ya uvuvi waandae miradi ya kuwasaidia wananchi kujua namna ya kufuga samaki bora wa asili kwaajili ya soko la kimataifa,”anasema.
Pia amewataka viongozi na watendaji ambao maeneo yao yanajishughulisha na uvuvi, hasa maeneo ya Pwani ya Bahari ya Hindi wahakikishe wanatumia maeneo hayo kwa faida.