Egidia Vedasto
Arusha
Wazazi na walezi wamekumbushwa utaratibu wa kukaa pamoja kuzungumza na kusikilizana ili waweze kubaini kama kuna changamoto hasa kwa upande wa watoto, maana familia ni chanzo cha jamii na iwapo watoto watalelewa katika misingi mizuri Taifa la kesho litakuwa na watu makini.
Akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Familia, katika Ofisi za Shirika la Amani Centre lisilokuwa la kiserikali Jijini Arusha, Afisa Maendeleo ya Jamii wilaya ya Arusha Martha George, kwa niaba ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi ya Watoto Dkt. Dorothy Gwajima, amesema ni muhimu wazazi kuwa makini kukabiliana na changamoto za malezi zitokanazo na matokeo hasi ya maendeleo ya teknolojia ya habari, mawasiliano na mwingiliano wa mila na desturi zisizofaa za mataifa mengine.
Aidha ameongeza kuwa licha ya majukumu makubwa waliyonayo wazazi ya kutafuta mahitaji ya familia pia ni mhimu kukaa na watoto hasa muda wa usiku ambapo wazazi na watoto kwa muda huo wanakuwa pamoja, kuwasikiliza watoto wao kama wanakutana na changamoto zozote, hatua itakayowasaidia namna bora ya kuwashauri watoto wao.
“Wizara na Wadau wake kupitia Mwongozo wa Taifa wa Wajibu wa Wazazi na Walezi Katika Malezi ya Watoto na Familia imeendelea kutoa elimu ya Malezi chanya kwa jamii kupitia redio na runinga mikutano ya wazi na makongamano yanayohusisha wananchi na mitandao ya kijamii” amesema George.
_Mratibu wa Shirika la Amani Centre mkoa wa Arusha Naomi Kimaro_ |
Kwa upande wake Mratibu wa Shirika la Amani Centre lililopo Jijini Arusha, Naomi Kimaro, amesema shirika hilo linafanya kazi na jamii kwa kushirikiana na serikali na limekuwa likihudumia watoto wanaoishi katika mazingira magumu, wanaofanyiwa vitendo vya ukatili na waliotelekezwa.
Sambamba na hayo amesema maadhimisho ya siku ya familia hufanyika kila mwaka tarehe 15 mei, ambapo mwaka huu wameamua kuwakutanisha wazazi wa watoto wanaowalea katika kituo chao ili kuwakumbusha wajibu wao katika malezi ya watoto.
“Niwakumbushe wazazi mlioko hapa, suala la malezi halitaki tofauti, bali wazazi mnatakiwa kushirikiana ili kuibua na kubaini changamoto katika malezi ili watoto wenu wawe na maadili mema na watumishi wema wa taifa la kesho” amefafanua Kimaro
Pia Afisa Ustawi wa Jamii katika Shirika la Amani Centre Hassan Aufi anayefanya kazi na na Jamii ameongeza kwamba, katika maadhimisho ya mwaka huu shirika limewakumbusha wazazi kuwa makini na mitandao ya kijamii kwa maana ya kuwaachia watoto simu, suala ambalo huwafanya watoto kuperuzi vitu visivyowahusu (vya kikubwa) kuwaathiri kisaikolojia na wengine kutaka kujaribu walichokiona kwenye simu hizo.
“Wazazi mlioko hapa mkawe mfano kwa wazazi wengine huko mitaani kwenu, mkawape elimu mliyoipata hapa kuhusu namna bora ya kulea watoto na kuwa makini na matumizi ya teknolojia ambayo kwa kiasi kikubwa inachangia mmonyoko wa maadili” amesema Aufi.
Hatahivyo Grace Mboya ambaye pia ni Afisa Ustawi wa Jamii katika Kituo cha Amani Centre amewataka wazazi kuwa na utamaduni wa kusikiliza na kukagua watoto wao ili kubaini changamoto kwani watoto wengi wamekuwa wakiripoti kwa walimu ukatili wanaokutana nao badala ya kuwaambia wazazi wao.
“Nafahamu wazazi mna kazi kubwa lakini ukirudi nyumbani jitahidi kuongea na mwanao, muulize anakutana na changamoto gani kutwa nzima na uweze kumsaidia, jitahidi mzazi kuwa rafiki wa mwanao na sio adui” Mboya amewakumbusha wazazi hao.
Mmoja wa Wazazi walioshiriki katika Maadhimisho hayo Katika kituo cha Amani Centre Josephat Masatu mkazi wa mtaa Sanawari amewaasa wanaume wenzake kuwa makini kushirikiana na wenza wao katika malezi ili kuepuka majuto ya baadae.
“Mimi ni mmoja wa wanaume waliotelekeza watoto wakalelewa na mama yao, lakini baada ya miaka mingi nilikutana nao wakiwa wamemaliza vyuo, na ukweli ni kwamba hawana mapenzi kabisa na mimi, suala hilo linaniumiza sana na ninajuta mno kwa kitendo hicho” amesema Masatu.
Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Familia mwaka huu yamebeba kaulimbiu “Tukubali Tofauti Zetu Kwenye Familia Kuimarisha Malezi ya Watoto”