* Ni katika Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa vyombo vya habari Mkoa wa Arusha
Na Seif Mangwangi
Arusha
Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Habari Maelezo, Mobhare Matinyi ni miongoni wa wageni watakaohudhuria kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa vyombo vya habari Duniani ambayo Mkoa wa Arusha wataadhimisha kesho.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Chama Cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha, Matinyi atapata fursa ya kuzungumza na waandishi wa habari wa Mkoa wa Arusha ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo.
Mgeni mwingine atakayehudhuria maadhimisho hayo ni Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari nchini ( UTPC), Kenneth Simbaya ambaye kwa upande wake atapata fursa ya kutoa mada kuhusiana na kauli mbiu ya maadhimisho ya Mwaka huu inayosema ” Waandishi wa Habari na changamoto za mabadiliko ya Tabia nchi”.
Aidha Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA), itawasilisha mada kuhusiana na matumizi sahihi ya Mtandao pamoja na Sheria ya Mawasiliano nchini ambapo pia itazungumzia majukumu na mipaka ya Mamlaka hiyo kisheria.
Mwenyekiti Claud Gwandu amesema pia ofisi yake imewaalika wadau mbalimbali wa habari Mkoa wa Arusha, ikiwemo Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, taasisi za Serikali na binafsi, wahadhiri na wanachuo wanaosomea masuala ya habari.
” Kongamano letu litajikita zaidi kujadili masuala ya kitaaluma, kutafakari utendaji wetu wa kazi kwa msimu ulioisha na kupanga matokeo ya baadae,ili Mwakani tukija tena tujipongeze pale tulipofanikiwa na tulipokosea tuboreshe zaidi, utaona tumealika pia wadau wa habari, lengo ni kutafakari kwa pamoja na kupokea mawazo yao ili kuboresha kazi zetu,” anasema.