Hifadhi ya Munywana ya Afrika Kusini yakabidhi Faru weupe 18 kwa Hifadhi ya Ngorongoro.

Na, Egidia Vedasto

APC Media, Arusha.

Faru moja ya wanyama wakubwa nchini waliokuwa hatarini kupotea, tumaini limerejea upya baada ya hifadhi ya Munywana ya Afrika Kusini kukabidhi Faru weupe 18 kati ya 36 wanaotarajiwa.

Akizungumza katika hafla ya kupokea Faru Weupe waliopandikizwa katika eneo la Ngorongoro Crater Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt.Pindi Chana amesema mategemeo ni kuona faru wanaongezeka maana uwezo na uzoefu uliopo katika sekta ya uhifadhi ni mkubwa.

“Ushirikiano wetu ulianzishwa na Waasisi wetu Mwalimu Julius Nyerere na Mzee Nelson Mandela na sasa hatua hii ya kutukabidhi Faru hawa, inadhihirisha muendelezo wa uhusiano wetu mzuri katika pande zote mbili, ombi langu ni kwamba tuendeleze mashirikiano haya kwa lengo la kusukuma maendeleo yetu mbele” amesema Dkt. Pindi Chana.

Aidha amepongeza jitihada kubwa zinazoendelea kufanywa na serikali ya awamu ya sita ya Dkt. Samia za kuhakikisha hifadhi zinatunzwa, hatua ambayo imechochea ongezeko la Watalii Nchini kutoka milioni 5 kufikia Milioni 5.3.

Kiongozi wa mila wa jamii ya Makhasa iliyopo Afrika Kusini iNkasi Zwelinzima Gumede amesema wataendelea kutoa ushirikiano kwa Tanzania kuhakikisha wanalinda wanyama hao na wanaendelea kuongezeka.

Hatahivyo amefafanua jinsi nchi ya Afrika Kusini ilipitia wakati mgumu wa majangiri kuanzia mwaka 2008 ambapo kufikia 2023 waliuliwa Faru takriban 10000, na kufafanua kuwa hifadhi ya Munywana imekuwa ikisambaza faru wake katika nchi za Botswana, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na leo Tanzania lengo ni kuhakikisha Faru weupe wanaongezeka ukanda wa Afrika.

“Sisi Hifadhi ya Munywana tunaahidi ushiriikiano wakati wowote mtakapotuhitaji ili kuendeleza mapambano dhidi ya ujangiri wa Faru weupe” amesema Gumede.

Upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Mkuu wa Majeshi Mstaafu Generali Venance Mabeyo amesema ushirikiano na kutokata tamaa vimechangia sehemu kubwa ya mafanikio ya kupatikana tena Faru Weupe Nchini.

“Licha ya kwamba ilionekana kuwa ngumu kufanikisja hili, lakini leo imekuwa furaha kubwa na historia imeandikwa Duniani kuwa Tanzania inakuwa na Faru Weupe, shukrani za dhati ziwaendee Wizara ya Fedha kupitia Mamlaka ya Mapato (TRA) waliohakikisha vibali vyote vinapatikana”,

” Kwa dhati tunaahidi kuwamamia vyema Watumishi wa Hifadhi ya Ngorongoro ili kuhakikisha Faru hao wanaongezeka na kuhakikisha hakuna vitendo vya ujangiri” amefafanua Mabeyo.

Katika namna hiyo hiyo Kalishna wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Dkt. Elirehema Doriye amesema upandikizwaji wa Faru weupe umezingatia usalama na uhakika wa malisho ya majani mafupi.

“Kuna tofauti kidogo kati ya Faru weupe na weusi, hawa weupe wanakula nyasi na wale weusi na wanapendelea kukaa maeneo tambalale ndio maana tumeona hapa panafaa zaidi kwa ustawi wao tofauti na wale weusi wanapenda kukaa maeneo yenye vichaka na kula majani ya juu juu, hivyo ulinzi wa hawa viumbe unamtegemea kila mtanzania” amesema Dkt. Doriye.

Vilevile Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utali CPA Benedict Wakulyamba amesisitiza ushirikiano na umoja katika kulinda hifadhi zote ili kutopoteza Wanyama adimu duniani.

“Hifadhi ya Munywana wamefanya kazi yao nzuri na sasa ni zamu yetu, tuhakikishe usiku na mchana tunalinda hifadhi zetu” amesema CPA Wakulyamba.