Na Mwandishi Wetu, DODOMA
WAZIRI wa habari, mawasiliano na teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ameipongeza klabu ya Waandishi wa Habari Arusha (APC), kwa hatua yake ya kuanzisha Taasisi ya Waandishi wa Habari Mtandaoni, Tanzania Online Media Alliance (TOMA) yenye lengo la kusimamia maslahi ya waandishi wa habari pamoja na kusaidia Asasi za Kiraia kufanya kazi na serikali kwa Karibu.
Waziri Nape ameyasema hayo Februari 10, 2023 Jijini Dodoma katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Habari Maelezo Gerson Msigwa wakati wa uzinduzi wa taasisi hiyo Jijini humo.
Aidha Waziri Nape ameutaka uongozi wa klabu ya waandishi wa Habari Arusha kutumia taasisi hiyo kuendesha mafunzo ya weledi kwa waandishi wa habari mtandaoni kwa kile alichosema wengi wao hawafuati misingi ya uandishi wa habari.
Amesema kwasasa vyombo vya habari mtandaoni vingi vinasumbuliwa ni weledi kwa baadhi kuzusha habari zisizokuwepo jambo ambalo ni hatari kwa jamii na Usalama wa nchi.
“Napenda kuwaomba wadau wa masuala ya habari na wamiliki wa vyombo vya habari kuzingatia weledi katika utendaji kazi wao hasa katika kipindi hiki cha Mapinduzi ya teknolojia kwa kuhakikisha wanazingatia maudhui yanayoendana na taaluma hii,”amesema na kuongeza:
“Sisi tunapaswa tujitahidi kujitofautisha na hao ili tulinde taaluma yetu na Serikali sio kwamba haioni juhudi za vyombo vya habari inaona na ndio maana imetoa uhuru wa kutosha kila mmoja kuanzisha na kumiliki chombo cha habari ila changamoto inatokea namna gani ya kuchuja kipi kiende hewani na kipi kisiende kulingana na maudhui yake,”amesema Msigwa
Msigwa amesema kuwa kutokana na kukuwa kwa matumizi ya TEHAMA imerahisisha habari kufika kwa jamii kwa haraka sana hivyo vyombo vya mitandaoni imekuwa tegemeo kama chanzo kikuu cha habari kwa haraka.
“Tasnia ya Habari ipo mikononi mwa vyombo vya habari Mtandaoni, kwa sasa vyombo vya habari Mtandaoni imekuwa nguzo kubwa kwa sekta ya habari nchini ila nitoe angalizo kwa sababu kadiri zinavyoongezeka inaonekana kama weledi wake unapungua hivyo niwatale TOMA kuhakikisha waandishi wa habari mtandaoni wanakuwa na uelewa mkubwa juu ya machapisho wanaotuma mtandaoni,
“Hicho ndicho kitakachotufanya tuaminike na jamii ni lazima tuangalie maadili ya uandishi wa habari yanasema nini, ni lazima tuangalie sheria za nchi yetu zinasema nini, hatuwezi kuwa waandishi wa habari za mtandaoni kwa kujikita tu kwenye kuzua taharuki, kuvunja sheria au kuchonganisha jamii na jamii au jamii na serikali,
“Tumetoka tulipotoka vyombo vya habari vikimilikiwa na wanasiasa na wafanyabiashara, akija mmiliki anasema weka hiki usiweke hiki,tuacheni kutumika, hapo ndipo heshima yetu itakuwepo, fanya kazi yako kwa weledi”.
Akitoa salamu za Ubalozi wa Marekani, Afisa ubalozi Japheth Sanga amesema kwa miaka mingi Nchi ya Marekani kupitia taasisi yake ya Maendeleo USAID imekuwa mshirika mkubwa na tasnia ya habari nchini.
Mtendaji wa Taasisi ya TOMA Seif Mangwangi akitoa maelezo kuhusu mtandao wa TOMA, mtandao huo ulizinduliwa rasmi na Msemaji wa Serikali Gerson Msigwa (wa nne kutoka kushoto waliosimama mbele) |
Amesema kuanzishwa kwa taasisi ya wanahabari Mtandaoni ni njia mojawapo ya kuimarisha Demokrasia lakini pia waandishi wa habari watapata mafunzo mbalimbali ya kuwajenga kitaaluma na kiuchumi na kuifanya sekta hiyo kuwa Bora zaidi.
Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Freedom House Tanzania, Wakili Daniel Lema |
Amesema mradi huo ambao umekuwa ukifanywa na Chama Cha Waandishi wa Habari Arusha ( APC), umeleta mafanikio makubwa kwa tasnia ya habari nchini ambapo baadhi yao wamepatiwa mafunzo mbalimbali.
Mwenyekiti wa bodi ya TOMA Claud Gwandu |
Mwenyekiti wa bodi ya Arusha Press Club ambaye pia ni Mwenyekiti wa bodi ya taasisi ya TOMA, Claud Gwandu amesema taasisi hiyo imeanzishwa baada ya kuonekana tasnia ya habari mtandaoni imekuwa ikikua kwa kasi lakini taarifa ambazo zimekuwa zikiripotiwa zimekuwa zikikosa weledi na kusababisha taharuki kubwa kwa jamii.
” Tutahakikisha TOMA inakuwa na wanachama wengi nchini na watakaokuwa na weledi kwenye uandishi wao, tutawapatia mafunzo ya kila aina ili kuwajenga na kuwa mfano, basi niwaombe waandishi mjiunge kwa wingi sana,”Amesema Gwandu.
Wageni mbalimbali wakishuhudia tukio la uzinduzi wa taasisi ya TOMA Jijini Dodoma |