Na Mwandishi Wetu- Dodoma
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Bw. Kaspar Mmuya amesema serikali itaendelea kusimamia uandaaji wa bajeti unaozingatia masuala ya kijinsia kama sehemu ya mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia kuhakikisha vitendo hivyo vinakomeshwa.
Naibu Katibu Mkuu huyo ametoa kauli hiyo Aprili 20, 2022 wakati akifungua mafunzo ya Uandaaji wa Bajeti zinazozingatia Usawa wa Kijinsia ili kuwajengea uwezo Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo kutoka ofisi hiyo yaliyofanyika Dodoma ambapo alisema elimu hiyo itasaidia watendaji kuzingatia utengwaji wa bajeti zenye mrengo wa kijinsia kama hatua ya mapambano ya ukatili nchini.
Alifafanua kwamba uzingatiaji wa bajeti zinazozogusa jinsia ni muhimu hasa wakati huu ambapo Wizara mbalimbali zinawasilisha bajeti zao katika vikao vya Bunge linaloendelea upo umuhimu wa kuhusisha masuala ya jinsia hatua itakayosaidia kutatua changamoto zinazojitokeza.
“Tupo kwenye hatua ya kupeleka bajeti zetu bungeni na baadaye kuridhiwa na Bunge lakini kwenye bajeti hizi yawezekana kuna eneo muhimu sana ambalo limeguswa au limeguswa kwa kiasi kidogo jicho la kuangalia bajeti zetu Je,zinagusa mtazamo wa jinsia? unavyopanga bajeti unaangalia utekelezaji wake utagusa wanawake? utagusa jinsia nidcho kitu cha msingi hivyo tunaamini mafunzo haya yatatujenga vizuri,”Alisema Bwa. Mmuya.
Vile vile albainisha kwamba mafunzo hayo ni muhimu na yamefanyika wakati muafaka kwa watumishi wa ofisi hiyo huku akizipongeza taasisi na mashirika yanayoiunga mkono serikali kusimamia usalama wananchi na kulinda haki za binadamu utakaochochea ustawi wa raia na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Mwezeshaji kutoka Sekretarieti ya Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) Bwa. Joel Mangi ambaye pia ni Mchumi Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum alitaja baadhi ya sababu ambazo zinasababisha kuendelea kwa matukio ya kikatili ndani ya jamii.
“Utafiti unaonyesha chanzo kimojawapo cha ukatili ni umasikini hususani wanawake,ukosefu wa elimu ,mila na desturi kandamizi wanapokuwa hawajitegemei kiuchuni inachochea ukatili ndani ya familia kwahiyo tukaona tuelimishe jamii kuhusu namna ya kujijenge kiuchuni na katika mila na desturi pia tuliwekeza katika elimu kupinga mila kandamizi kwa wanawake na watoto,”alieleza Mwezeshaji huyo.
Aidha Afisa Mradi Mwandamizi kutoka Shirika lisilo la Kiserikali la Women Fund Tanzania-Trust (WFT-T) Bi. Neema Msangi alisema utengwa kwa bajeti inayozingatia jinsia itasaidia fursa ya kutatua changamoto mbalimbali ambazo huwakabili wananwake na watoto ndani ya jamii.
“Tunapozungumzia bajeti yenye mrengo wa jinsia tutaweza kuona picha halisi ya namna gani tusipotazama bajeti zetu kwa kuzingatia jinsia ziatenda kuwapa shida na watoto ndiyo maana sisi kama WFT-T kwetu tuliona ni nafasi kubwa na tuliona tuna sababu kabisa ya kuungana na nyie,”alifafanua Afisa huyo.