Dkt pima atangaza dau kwa watendaji, ni watano wa kwanza kumaliza zoezi la anwani za makazi

 Na Seif Mangwangi, Arusha

Mkurugenzi wa Jiji la Arusha amesema Jiji hilo limeandaa zawadi maalum ya fedha na cheti kwa watendaji wa kata tano za mwanzo watakaokamilisha zoezi la kuweka anwani za makazi kwa wakati katika kata zao bila ya kikwazo chochote.

Akifunga mafunzo ya siku moja leo jumapili, Februari 13, 2022 Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dkt John Pima amesema anajua watendaji wa Halmashauri ya Jiji la Arusha ni wachapakazi wazuri lakini ili kuwapa motisha zaidi, menejimenti yake itawapatia zawadi ya fedha pamoja na cheti kama ambayo imekuwa ikifanya kwa walimu ambao wanafunzi wao wamepata alama A katika masomo yao ya kidato cha nne.

“Maafisa watakaokamilisha zoezi hili tutawapatia zawadi, naamini menejimenti yangu haitaniangusha katika hili, kama ambavyo tumekuwa tukifanya kwa walimu ambao wanafunzi wao wanapata alama A katika mitihani ya mwisho basi na huku tutawapatia, mtu akiwa nyumbani kwake anatundika cheti chake anaona jinsi alivyothaminiwa kutokana na uchapakazi wake,”Amesema.

Watendaji wa kata, tarafa na baadhi ya maafisa wa jiji wakisikiliza hotuba ya Mkurugenzi wa Jiji Dkt John Pima 
watendaji wa kata za Halmashauri ya Jiji la Arusha wakisikiliza hotuba ya Mkurugenzi wa Jiji Dkt John Pima (hayupo pichani)

Amewataka maafisa watendaji wa kata zote za Jiji la Arusha kufanyakazi hiyo kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu na kuimaliza kwa wakati kwa kuwa Jiji hilo lilishaanza kazi hiyo hata kabla ya zoezi hilo na kwamba endapo kuna changamoto yoyote itakayojitokeza yeye yupo lakini pia kila kata ina maafisa kutoka ndani ya ofisi yake.

“Nyie watendaji wa kata ndio wakurugenzi ndani ya kata zenu, naomba kama kuna changamoto yoyote wasilianeni na mimi lakini pia kila kata ina mlezi ambae ni Mkuu wa idara katika Jiji  hivyo naamini zoezi hili litaendeshwa kwa kasi sana na kumalizika kwa wakati,”amesema.

Na kuongeza,”kama unafikiri kuna kitu unahitaji zaidi tuandikie, kama ni matangazo ya kuhamasisha ofisi zetu zote zipo na bajeti yake pia itakuwepo, naombeni sana tufanye liwezekanalo kazi hii iishe kwa wakati, ukiniangusha mimi mmemuangusha Rais wa Nchi Mheshimiwa Samia Suluhu ambaye ameliita zoezi hili ni operesheni maalum, na sisi tulifanye kwa umaalum wake,”amesema.

Dkt Pima pia amewataka watendaji kuajiri vijana watakaoshiriki kwenye zoezi hilo kutoka ndani ya mitaa husika ili kuepusha usumbufu wa kufanya utambuzi wamiliki wa maeneo na nyumba katika maeneo hayo wakati wa kuanza kubandika anwani za makazi katika maeneo hayo.

Amezitaja kata ambazo zoezi lake litachukua muda mfupi sana kuliko maeneo mengine kutokana na kata hizo kuwa na anwani tangu awali kuwa ni pamoja na kata ya Kaloleni, Themi, Levolosi, Mjini kati na Sekei.