Karibu Tawala Mkoa wa Arusha Dkt Athumani Kihamia |
Na Mwandishi Wetu,Arusha.
Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Dkt Athumani Kihamia amewataka watumishi wa halmashauri ya Jiji hilo kutumia busara katika kushughulikia malalamiko ya wananchi ikiwa ni pamoja na kufuata taratibu na sheria zinazoongoza ushughulikiaji wa malalamiko yao.
Akizungumza katika kikao cha utambulisho wa Mkuu wa Wilaya ya Arusha kwa watumishi wa jiji hilo, Dkt Kihamia amesema Ilani ya Chama cha Mapinduzi inatilia mkazo suala la kuwahudumia wananchi kwa busara ili kuhakikisha haki inapatikana.
“Kwanza katika kughulikia malalamiko ya wananchi ni wajibu apokelewe vizuri, asikilizwe vizuri na aelekezwe vizuri, na ndiyo maana tunaambiwa katika kuwahudumia wananchi inapaswa busara itumike kwa asilimia 30, taratibu na sheria inachukua asilimia 70” Alisema Dkt Kihamia.
Kwa upande mwingine Katibu Tawala huyo ameipongeza idara ya ardhi kuendelea kushughulikia vyema migogoro ya ardhi hali iliyopelekea migogoro hiyo kupungua kwa kiasi kikubwa na kusema hatua hiyo inaonyesha idara imejipanga na inafanya kazi kwa kushirikiana.
Ameongeza kusema kuwa ili watumishi waweze kutimiza malengo ya serikali ambayo ni kutoa huduma bora kwa wananchi ni lazima kuwepo kwa motisha kutoka kwa wakubwa wao wa kazi, hivyo suala la motisha kwa watumishi ni la muhimu.
Akizungumza na watumishi hao, Mkuu wa wilaya ya Arusha Said Mtanda ameipongoza halmashauri hiyo kwa ukusanyaji wa mapato hali iliyopelekea jiji hilo kuwa miongoni mwa majiji yanayofanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato nchini.
“Siyo kwa upande wa mapato pekee, hata katika idara nyingine kama vile afya, elimu na mazingira, mmefanya vizuri sana, hivyo ni jambo la kujivunia licha ya kuwa ni lazima tuweke mikakati ya kuboresha zaidi” Alisema Mkuu wa wilaya.
Mkuu wa Wilaya ya Arusha Said Mtanda |
Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dkt John Pima |
Watumishi wa Jiji la Arusha |
Na katika kufanikisha mkakati huo ameiagiza idara ya Uchumi na fedha kufanya zoezi la sensa kwa muda wa mwezi mmoja kwa wafanyabiashara ili kubaini ni nani anastahili kupata mapato ya halmashauri na ni nani halipi na majibu ya sensa hiyo aipate baada ya kukamilika kwa zoezi hilo.
Mkuu wa wilaya pia amewataka watumishi hao kushirikina na Chama cha Mapinduzi katika kuwahudumia wananchi pamoja na kuzingatia suala la nidhamu na kuheshimiana miongoni mwa mwao bila kujali vyeo na madaraja waliyonayo ili kuleta nguvu katika kuisaidia serikali kuwahudumia wananchi wake.
Awali akimkaribisha mkuu huyo wa wilaya, Mkurugenzi Mtendaji wa jiji la Arusha Dkt John Pima amemuhakikishia mkuu huyo wa wilaya kuwa ofisi yake itampa ushirikiano wa kutosha kwa kuwa wanafanya kazi kama timu moja.
Dkt Pima amesema wao katika kutimiza majukumu yao wanazingatia kauli mbiu inayowaongoza ya “kutoa huduma bora kwa wananchi ili kutimiza malengo ya serikali” na ndiyo sababu wameweza kukusanya mapato kwa kiwango kikubwa.
“Sisi jiji tutakupa ushirikiano wa kutosha, na kwa kuwa tunafanya Kazi kwa timu, hili litawezekana kwani hata haya mapato kupanda ni kutokana na kufanya Kazi kwa ushirikiano kama timu moja” alisema Dkt Pima.