Na Abubakari W Kafumba, UAE
Katibu Mkuu wa Wizara Maliasili na Utalii Dkt. Allan Kijazi ametembelea banda la Tanzania kwenye maonesho ya Expo 2020 Dubai ambapo amepolekewa na Mkurugenzi wa Banda la Tanzania Bi. Getrude Ng’weshemi kutoka TanTrade na watumishi wengine kutoka Taasisi zinazoshiriki.
Dkt. Kijazi ambaye alifanya ziara hizo juzi alipata fursa ya kufanya kikao kifupi na watumishi hao kutoka Taasisi zinazoshirki katika maonesho haya zikiwemo Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Eneo la Hifadhi la Ngorongoro (NCAA), Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ambapo alipokea taarifa ya maandalizi ya ushiriki wa Tanzania kwenye maonesho ya Expo 2020 Dubai, mafanikio yaliyopatikana na hatua zinazochukuliwa katika kuimarisha ushiriki wa uhakika wa Tanzania kwenye maonesho haya.
Aidha, Dkt Kijazi amesistiza maandalizi ya uhakika ya wiki ya Utalii yanayotarajiwa kufanyika tarehe 12 hadi 18 Desemba, 2021 pamoja na siku ya kitaifa ‘National Day’ itakayofanyika tarehe 26 Februari 2022. Maandalizi ya ushiriki katika programu ambazo zimeandaliwa yafanywe mapema kama ilivyopangwa na waratibu wa maonesho haya.
Amesema kuwa,” Fursa hii ya kushiriki kwenye maonesho haya ni ya kipekee na sisi kama Taifa tuna jukumu la kuitumia nafasi hii kuhakikisha Tanzania ina ushiriki wenye tija. Ninasisitiza Sekta zote zilizopata fursa ya kuwa sehemu ya maonesho haya ziendelee kuhamasisha ushiriki wa Tanzania hapa Expo 2020 Dubai hasa kwa Watanzania walio nyumbani ambao bado ushiriki wao ni mdogo. Naziasa Wizara, Taasisi na Sekta Binafsi kuwa kitu kimoja katika kuiwakilisha nchi na kuhamasisha ushiriki wa wadau mbalimbali wenye ushawisi katika jamii ili tulibebe jambo hili kwa pamoja kama taifa.
Vilevile, alitembelea banda la Tanzania ili kujionea jinsi nchi inavyotumia fursa hii kujitangaza kupitia sekta mbalimbali na inavyowavutia wawekezaji kupitia miradi mikubwa iliyopewa kipaumbele. Banda lingine alilotembelea ni la Saudi Arabia ambapo lengo lilikua ni kuangalia, kujifunza na kuandaa vema ushiriki wa Sekta ya Utalii kama ilivyopangwa kwenye programu kuu ya ushiriki ya Taifa.