Sido arusha yawafunda wamiliki viwanda vidogo

 Na Magesa Magesa,Arusha

SHIRIKA la kuhudumia
viwanda vidogo nchini (SIDO)Mkoani hapa, limewataka wamiliki wa viwanda vidogo
mkoani hapa kuhakikisha kuwa wanakuwa wabunifu na kuzalisha bidhaa bora ili
kukabiliana na ushindani wa kibiashara uliopo sasa.

Meneja wa SIDO Mkoani hapa Jalphary Donge aliyasema hayo jana Jijini
hapa, alipokuwa akifunga mafunzo ya siku mbili kwa wamiliki na wakurugenzi wa
viwanda vidogo yaliyofanyika katika ofisi za shirika hilo.

“Msifanye biashara kwa uzoefu hakikisheni mnakuwa wabunifu, zalisheni
bidhaa bora zenye viwango vya hali ya juu kwani kwa sasa kumekuwa na ushindani
mkubwa sana pindi bidhaa zifikapo sokoni”alisisitiza Donge

Mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uwezo wamiliki na wakurugenzi
hao juu utoaji wa huduma za maendeleo ya biashara(BDS)ambayo yalifadhiliwa na
UNICO-JICA kwa kushirikiana na SIDO Mkoani hapa.

Kwa upande wake mkufunzi wa mafunzo hayo,Edward Rwegoshora kutoka Shirika
la kubadilisha na kuboresha maisha ya watanzania(STAWI)aliwataka washiriki wa
mafunzo hayo kuhakikisha kuwa wanazingatia yale yote waliyofundishwa na waende
wakayafanyie kazi kwa vitendo.

 Aliwataka kuhakikisha kuwa wanafanya utafiti ili kupata
uzoefu na kupima utayari wa upokeaji wa huduma za maendeleo ya biashara lengo likiwa
ni kuendeleza biashara zao na kuvutia wateja wengi zaidi.

Kwa upande wake mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Diana Mamuya
kutoka

kiwanda cha kutengeneza mvinyo cha Anna aliwapongeza SIDO kwa
kuandaa mafunzo hayo  na kusema kuwa yamekuja kwa wakati muafaka na
kushauri muda uongezwe katika kupatiwa mafunzo hayo