Sekta ya uvuvi kufanya mapitio ya baadhi ya sheria na kanuni-waziri ndaki

 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.
Mashimba Ndaki (Mb) akizungumza na wadau wa sekta ya uvuvi wa mkoa wa
Kagera (hawapo pichani) ambapo amewaeleza kuwa wizara itafanya mapitio
ya sheria na kanuni za uvuvi ili ziweze kuendana na mazingira ya sasa.
Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa
Kagera.

Mmoja ya wadau wa sekta ya uvuvi
mkoani Kagera, Bw. Pancras Mtungireli akitoa maoni yao kuhusu maendeleo
ya sekta ya uvuvi kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi (hayupo pichani) kwenye
kikao cha wadau hao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa
Mkoa wa Kagera.

…………………………………………………………………….

Sekta ya Uvuvi imepanga kufanya mapitio ya baadhi ya sheria na kanuni za uvuvi ili ziweze kuendana na mazingira ya sasa.

Haya yamesemwa na Waziri wa Mifugo na
Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki wakati alipozungumza na wadau wa sekta ya
uvuvi wa mkoa wa Kagera kwenye kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Waziri Ndaki alisema kuwa kumekuwepo
na malalamiko kutoka kwa wadau kuwa baadhi ya sheria na kanuni za uvuvi
zimekuwa kikwazo katika utekelezaji wa shughuli zao. Hivyo wizara imeona
ni muda muafaka kufanya mapitio ya baadhi ya sheria na kanuni hizo ili
ziendane na mazingira ya sasa na kutokuwa kikwazo katika ufanyaji wa
shughuli za uvuvi.

Lakini pamoja na mapitio hayo ya
sheria na kanuni, wadau wa sekta ya uvuvi wametakiwa kuhakikisha
wanafuata taratibu zote zilizopo katika utekelezaji wa shughuli zao za
uvuvi na sio kusubiri mpaka wafuatiliwe. Aidha Waziri Ndaki aliwasihi
wadau hao kuhakikisha wanashiriki kikamilifu kwenye udhibiti wa uvuvi
haramu kwani bila kufanya hivyo samaki wataisha majini na wao
itawalazimu kutafuta shughuli nyingine za kufanya.

Vilevile kwa upande wa wataalam
wametakiwa kuendelea kuwaelimisha wavuvi kutumia mbinu bora za uvuvi ili
waondokane na uvuvi haramu. Aidha, amewaonya wataalam kutojihusisha na
vitendo vya uvuvi haramu kwani endapo watabainika watachukuliwa hatua.
Pia amewataka wataalam kuendelea kuwaelimisha wavuvi kuhusu suala la
ufugaji wa samaki kwenye vizimba.

Waziri Ndaki aliwaeleza wadau hao kuwa
kazi wanayoifanya ya uvuvi ni halali na inatambulika kiserikali na
serikali inategemea kupata mapato kutokana na shughuli za uvuvi hivyo
wanatakiwa kuwa huru wakati wanapofanya shughuli zao na endapo
wanakutana na changamoto ni vema wawe wanazifikisha kwenye mamlaka
husika.

Pia amezishauri mamlaka za serikali za
mitaa kutathmini upya tozo walizoziweka kwenye mazao ya uvuvi, biashara
ya uvuvi au kwenye shughuli ya uvuvi kwani ni nyingi.

Wadau hao wa sekta ya uvuvi wa mkoa wa
Kagera wamemshukuru waziri kwa kuitisha kikao hicho ambacho wameweza
kutoa changamoto na maoni yao juu ya maendeleo ya sekta ya uvuvi kwani
ni kitu ambacho hawajawai kutegemea kuja kukaa na waziri na
kuwasikiliza.