Naibu waziri kasekenya awasisitiza wakandarasi nchini kumaliza miradi kwa wakati

 

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi
Mhandisi Godfrey Kasekenya (wa kwanza), akikagua ujenzi wa daraja dogo
la Mvugwe, katika barabara ya Kabingo, Kasulu hadi Manyovu (KM 260)
mkoani Kigoma, kipande cha Mvugwe hadi Nduta (KM 59.35), kinachojengwa
na Kampuni ya STECOL Corporation kwa kiwango cha lami.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi,
Mhandisi Godfrey Kasekenya, akimuelekeza jambo Mhandisi Mkazi Tadesse
Dirba (Wakwanza kulia), wakati akikagua mradi wa ujenzi wa barabara ya
Kabingo- Kasulu hadi Manyovu, kipande cha Kanyani hadi Mvugwe (KM 70.5),
kinachojengwa na Kampuni ya Sinohydro Corporation Limited kwa kiwango
cha lami .

Mhandisi Mkazi Khatibu Khamis,
akimuelezea jambo Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey
Kasekenya (wa tatu kushoto), wakati akikagua ujenzi wa barabara ya
Kabingo, Kasulu hadi Manyovu (KM 260) mkoani Kigoma, kipande cha Mvugwe
hadi Nduta (KM 59.35), kinachojengwa na Kampuni ya STECOL Corporation
kwa kiwango cha lami.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi
Mhandisi Godfrey Kasekenya, akimuelekeza jambo Mhandisi Mkazi Khatibu
Khamis (wa pili kushoto), wakati akikagua ujenzi wa barabara ya Kabingo,
Kasulu hadi Manyovu (KM 260) mkoani Kigoma, kipande cha Mvugwe hadi
Nduta (KM 59.35), kinachojengwa na Kampuni ya STECOL Corporation kwa
kiwango cha lami.

Mtaalamu wa kupima udongo katika
maabara ya kampuni ya Zhejiang Communications Construction Group Co. Ltd
(ZCCC), inayojenga kipande cha barabara ya Manyovu hadi Kasulu
(KM68.25) mkoani Kigoma, akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na
Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya (katikati), wakati akikagua
utendaji kazi wa maabara hiyo. Kushoto ni Meneja wa Wakala wa Barabara
(TANROADS) mkoa wa Kigoma, Mhandisi Narcis Choma.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi
Mhandisi Godfrey Kasekenya, akizungumza na wananchi wa eneo la Mvugwe
mkoani Kigoma, baada ya kumaliza ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa barabara
ya Kabingo- Kasulu hadi Manyovu, kipande cha Kanyani hadi Mvugwe (KM
70.5), kinachojengwa na Kampuni ya Sinohydro Corporation Limited kwa
kiwango cha lami.

Ujenzi wa daraja dogo la Mvugwe
ukiendelea katika barabara ya Kabingo, Kasulu hadi Manyovu (KM 260)
mkoani Kigoma, kipande cha Mvugwe hadi Nduta (KM 59.35), kinachojengwa
na Kampuni ya STECOL Corporation kwa kiwango cha lami.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi
Mhandisi Godfrey Kasekenya, akimuelekeza jambo Meneja wa Wakala wa
Barabara (TANROADS) mkoa wa Kigoma, Mhandisi Narcis Choma, wakati
akikagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Kabingo, Kasulu hadi Manyovu,
kipande cha Kanyani hadi Mvugwe (KM 70.5), kinachojengwa na Kampuni ya
Sinohydro Corporation Limited kwa kiwango cha lami.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi
Mhandisi Godfrey Kasekenya, akizungumza na Mhandisi Mkazi Gelawdiwos.
kwenye mradi wa ujenzi wa barabara ya Kabingo, Kasulu hadi Manyovu
mkoani Kigoma, kipande cha Manyovu hadi Kasulu (KM68.25), kinachojengwa
na Mkandarasi Zhejiang Communications Construction Group Co. Ltd (ZCCC),
kulia kwa Naibu Waziri ni Meneja wa Wakala wa barabara (TANROADS) mkoa
wa Kigoma, Mhandisi Narcis Choma.

PICHA NA WUU

………………………………………………………………………….

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi,
Mhandisi Godfrey Kasekenya, amewataka Wakandarasi wanaojenga miradi ya
barabara nchini kuhakikisha wanafanya kazi usiku na mchana hususan
katika kipindi cha kiangazi ili kukamilisha miradi kwa wakati.

Kasekenya ameyasema hayo wilani
Kasulu, mkoani Kigoma, wakati alipokuwa akikagua maendeleo ya mradi wa
barabara ya Kabingo- Kasulu- Manyovu yenye urefu wa kilometa 260.

Amefafanua kuwa kitendo cha kuongeza
muda wa kufanya kazi kwa Makandarasi hao kutafidia muda watakaoupoteza
wakati wa kipindi cha masika ambapo miradi ya barabara husimama kutokana
na mvua.

“Nimepita kuangalia maendeleo ya mradi
huu wa barabara yenye urefu wa kilometa 260 ambao unatekelezwa na
makandarasi mbalimbali katika vipande vinne tofauti, nimefurahishwa na
baadhi ya makandarasi hawa kujiongeza kwa kuamua kuongeza muda wa
ufanyaji kazi, hii itasaidia hata miradi kukamilika kwa wakati, hivyo
nawaagiza makandarasi wengine nao kuiga mfano huu”, amesema Kasekenya.

Aidha, amewataka Makandarasi na
wasimamizi wa miradi hiyo kuzingatia viwango vya ubora wakati wa ujenzi
wa miradi hiyo na kuhakikisha kuwa kila kilichoandikwa kwenye mchoro
ndicho kinachofuatwa.

Amewasisitiza Makandarasi na
wasimamizi wa miradi hiyo kubainisha changamoto zozote zinazowakabili
ili zitatuliwe mapema wakati mradi ukiwa kwenye hatua za awali.

Amewahakikishia Makandarasi hao na
wasimamizi wake kuwa Serikali itaendelea kutoa fedha kwa wakati ili
kuhakikisha miradi haikwami kutokana na ucheleweshaji wa malipo.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri
Kasekenya wakati akimalizia ziara yake wilayani Kibondo mkoani humo,
akiwa anakagua kipande cha Tatu cha barabara cha Mvugwe – Nduta Junction
(Km 59.35) amesema kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutapunguza muda
wa safari kutoka wilayani hapo kuelekea mikoa mingine kama vile Mwanza,
Kagera na nchi jirani ya Burundi.

Kwa upande wake, Mhandisi Mshauri
kutoka kampuni ya Afrisa, ambao ni wasimamizi wa kipande cha barabara
kutoka Kanyani – Mvugwe (Km 70.5) Reginald Kaganga, amesema kuwa
kipande hicho kinatekelezwa na Mkandarasi Sinohydro ambapo kazi
zinazoendelea kwa sasa ni kusafisha, kujenga tuta na kuweka tabaka la
mwanzo la barabara pamoja na ujenzi wa makalvati.

Nao wananchi wa Kasulu wamesema kuwa
kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo kutarahisisha huduma za usafiri
na usafirishaji wa mazao na hivyo kuweza kuyafikia kwa urahisi masoko
ya ndani na nje ya nchi.

Barabara hii ya Kabingo- Kasulu-
Manyovu yenye urefu wa kilometa 260 inajengwa kwa vipande vinne tofauti
ambavyo ni Kasulu – Manyovu (Km 68.25), Kanyani – Mvugwe (Km 70.5),
Mvugwe – Nduta Junction (Km 59.35) na Nduta Junction – Kabingo (Km 62.5)
ambapo ujenzi wa vipande hivi vyote unafadhiliwa na Benki ya maendeleo
ya Afrika ( AfDB).

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi