Waziri wa nishati akutana na wadau mradi wa lng

 

20, Juni 2021-Lindi

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard
Kalemani (MB) amekutana na wadau wa mradi wa kusindika gesi asilia kuwa
kimiminika (Liquefied Natural Gas-LNG) katika mkutano uliofanyika Mkoani
Lindi kwa lengo la kutoa taarifa ya maendeleo ya mradi huo.

Akizungumza na wadau, Waziri Kalemani
alieleza kuwa Serikali imedhamiria kwa dhati kuteleleza mradi wa LNG na
tayari kazi mbalimbali zimekwishafanyika ikiwemo utwaaji wa ardhi ya
mradi yenye ukubwa wa hekta 2,071, ulipaji wa Bilioni 5.7 kama fidia kwa
wananchi watakaopisha mradi, upembuzi wa awali wa kihandisi (Pre FEED)
pamoja na kuundwa kwa Timu ya Serikaki ya Majadiliano (Government
Negotiation Team-GNT) na Timu ya Wataalam (Technical Team) itakayofanya
kazi na GNT.

Waziri Kalemani alieleza kuwa Serikali
imejipanga kukamilisha majadiliano ya Mkataba wa Nchi Hodhi (Host
Governmemt Agreement-HGA) ndani ya miezi 6 ili kuwezesha utekelezaji wa
mradi kuanza mapema, “kufikia mwezi wa kumi majadiliano ya HGA yatakuwa
yamekamilika” alieleza Waziri Kalemani. Waziri Kalemani pia aliilekeza
TPDC kukamilisha ndani ya mwezi mmoja zoezi la uwekaji wa mipaka katika
eneo la mradi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa
TPDC, Dkt. James Mataragio alieleza sababu zilizopelekea mradi kuchukua
muda mrefu ambazo ni pamoja na zoezi la upitiaji wa mikataba ambapo
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania liliiagiza Serikali kufanya
mapitio ya Mikataba ya Ugawanaji Mapato (Production Sharing Agreement-
PSA). Zoezi la kupitia Mikataba ya PSA lilitekelezwa na ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali na lilipelekea majadiliano yaliyokuwa
yameanza mwaka 2016 kusimama kupisha zoezi hilo muhimu kukamilika,
alieleza zaidi Dkt. Mataragio.

Nae Mkuu wa Wilaya Mteule wa Lindi,
Ndg. Shaibu Ndemanga aliemuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Lindi katika kikao
hicho alieleza kufurahishwa kwake kwa namna ambayo TPDC imekuwa
ikiwashirikisha wadau wa LNG Lindi kwa kuwapa taarifa za mara kwa mara
jambo ambalo liliondoa sintofahamu juu ya mradi huu. Ndg. Ndemanga pia
alisema “kipekee niwashukuru Wizara ya Nishati na TPDC kwa namna ambayo
walishughulikia zoezi la fidia kwa waathirika wa mradi wa LNG ambapo
wananchi walifuatwa katika maeneo yao na hivyo kuwaondolea usumbufu wa
kusafiri umbali mrefu kufuata haki yao”

Mkutano wa Wadau wa mradi wa LNG
ulihudhuriwa na Wabunge wa Lindi na Mtwara, Wafanyabishara wa Lindi,
Wawakilishi wa wawekezaji kutoka kampuni za Shell na Equinor,
Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa wa Lindi na watumishi wa Wizara ya
Nishati na wale wa TPDC

Mradi wa LNG unatarajiwa kutekelezwa
katika Mkoa wa Lindi, Manispaa ya Lindi, Kata ya Mbanja katika mitaa ya
Likong’o, Mto Mkavu na Masasi ya Leo. Uwekezaji katika mradi huu
unaelezwa kufikia hadi Dola za Marekani Bilioni 30 na utatekelezwa na
Serikali kupitia TPDC kwa upande mmoja na wawekezaji ambao ni Kampuni za
Shell na Equinor pamoja na washirika wao kwa upande mwingine. Mradi huu
utawezesha gesi asilia iliyogundulika katika kina kirefu cha maji
baharini (futi za ujazo trilioni 47.08) kuweza kuvunwa kibiashara ambapo
sehemu ya gesi hiyo itauzwa soko la kimataifa katika nchi za Asia na
nyinginezo na kiasi kingine kitatumika kwa matumizi ya ndani ya nchi
pamoja kanda.