Wizara ya maliasili na utalii yaendelea kutoa elimu ya kukabiliana na wanyamapori wakali kwa wananchi.

 

 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Same, Anastazia Tutuba
akifungua rasmi mafunzo shirikishi ya mbinu za kudhibiti migongano baina
ya binadamu na wanyamapori wakali na waharibifu Wilayani same ambapo
amewataka wananchi kuwa wakweli katika kutoa taarifa ya matukio ya
uvamizi wa wanyamapori katika maeneo yao.

Afisa Wanyamapori Mkuu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii,akizungumza
wakati wa ufunguzi wa Mafunzo ambapo amewataka wananchi kutoa
ushirikiano kwa askari wanyamapori katika kukabiliana na wanyama wakali
na waharibifu.

Mtafiti kutoka Taasisi ya utafiti wa wanyamapori Nchini (TAWIRI), Dkt.
Janemary Ntalwila akitoa maelezo ya awali wakati wa ufunguzi rasmi wa
mafunzo shirikishi mbinu za kudhibiti migongano baina ya wanadamu na
wanyamapori waharibifu na wakali,wilayani same mkoani Kilimanjaro.

 Serikali
kupitia Wizara ya maliasili na utalii imeendelea kutoka mafunzo
shirikishi ya mbinu za kudhibiti migongano kati ya wanyamapori Wakali na
waharibifu kwa lengo la kuwalinda wananchi na mali zao. 

Akizungumza
Wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa askari wa wanyamapori wa vijiji vya
wilaya za Same na Mwanga, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya
ya Same, Anastazia Tutuba amesema pamoja na Serikali kuweka nguvu ya
katika kupambana na changamoto ya wanyamapori katika maeneo ya makazi ya
binadamu, wananchi nao wanapaswa kuwa wakweli katika utoaji wa taarifa
za matukio ya uvamizi wa wanyamapori katika maeneo yao na kuwa wakweli
katika kutoa taarifa za kiwango cha uharibifu.

 ‘ Jana kuna
mwananchi ametupigia simu kuwa tembo wamevamia shamba lake na kuharibu
hekari nane,tumeenda pale tumekuta kiwango cha uharibifu alicho sema
mtoa taarifa ni tofauti na hali halisi lakini pia alifyeka sehemu ya
shamba lake yeye mwenyewe ili apate fidia’ amebainisha Tutuba. 

Kwa
Upande wake Afisa Wanyamapori Mkuu wa wa Wizara ya Maliasili na Utalii,
Antonia Raphael amewataka askari wanao patiwa mafunzo kufuatilia vyema
mbinu na mafunzo wanayopewa huku akibainisha kuwa ushiriki wa wananchi
katika kutoa taarifa utaifanya kazi hiyo iwe rahisi.

‘Ninyi wananchi ni kiungo muhimu sana katika mapambano haya ,mtoe
ushirikiano kwa wakufunzi. 

Amesisitiza Antonia.

Katika hatua nyingine, Mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori
Tanzania (TAWIRI) Dkt. Janemary Ntalwila amesema mkakati huo wa mafunzo
shirikishi ni endelevu kwa maeneo yote yenye changamoto ya wanyamapori.