Mbunge luhaga mpina afichua siri nzito bungeni inayoua viwanda vya mazao ya kilimo nchini, aishauri serikali kuchukua hatua

 


Mbunge wa Jimbo la Kisesa, Mhe. Luhaga Mpina akichangia hotuba ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2021/2022 bungeni Dodoma ambapo ameshauri Serikali kuchukua hatua kusaidia wakulima.

MBUNGE wa Kisesa, Mhe.  Luhaga Mpina ameibua bungeni tatizo kubwa  linalochangia kuua viwanda na ajira za vijana
wa kitanzania kupitia Kilimo kutokana na mfumo wa kikodi kuwapendelea waagizaji
bidhaa kutoka nje ya nchi na kuwakandamiza wazalishaji wa ndani wanaotegemewa
kutoa ajira na kukuza uchumi wa nchi.

Hivyo
ameshauri Serikali kuchukua hatua ili kumaliza mkwamo huo uliodumu kwa zaidi ya
miaka sasa na kuwezesha sekta ya kilimo kukua zaidi kwa kuwezesha wakulima
kupata bei nzuri ya mazao yao pamoja na soko la uhakika.

Tunakubaliana
kwamba sekta za kilimo, mifugo na uvuvi 
ni muhimu sana kwa maendeleo ya taifa letu kwani zinatoa asilimia 25 ya
fedha za kigeni,   asilimia 30 ya pato la
taifa, asilimia 65 ya malighafi, asilimia 70 ya ajira zote na asilimia 100 ya
mahitaji ya chakula ni sekta muhimu na ndio maana tunasema ni uti wa mgongo.

Tanzania
inazalisha mazao mbalimbali ambayo mengi yanatumika nchini na mengine yanauzwa
nje ya nchi kama tumbaku, korosho, mkonge, michikichi, kokoa, pamba, kahawa,
chai, maharage, maharage ya soya, alizeti, maua, matunda, mbogamboga, choroko,
mbaazi, ufuta, dengu, viungo, miwa, viazi, mihogo, mahindi, mtama, karanga.

Pamoja
na uzalisha huo mpaka sasa kwa takwimu zilizopo tunaagiza chakula kutoka nje ya
nchi chenye thamani ya wastani wa sh. Trilioni 1.3 kwa mwaka jambo ambalo ni
aibu kwa nchi yetu yenye ardhi nzuri yenye rutuba na fursa lukuki za kilimo. 

Aidha ifahamike pia kuwa zaidi ya asilimia 40 ya watanzania kipato chao
kinatokana na kilimo cha zao la Pamba.

Zaidi
ya asilimia 40 ya watanzania wote wanategemea kipato chao kupitia zao la pamba.

Takwimu
zinaonesha kuwa uzalishaji wetu wa mazao unashuka na mauzo yetu nje ya nchi
yanashuka mfano kupitia hotuba ya Waziri uzalishaji wa pamba umeshuka kutoka
tani 348,958 mwaka 2019/2020 hadi tani 122,833 mwaka 2020/2021, uzalishaji wa
korosho ulishuka kutoka tani 232,631 mwaka 2019/2020 hadi kufikia tani
206,718.88 mwaka 2020/2021.

Waziri
anakiri kwamba moja ya sababu za kushuka uzalishaji wa mazao ni kushuka kwa bei
na baadhi ya wakulima kuamua kuachana na kilimo. Kama Bunge ni lazima tutafute suluhisho la suala hili.

Hata
hivyo kabla sijaendelea na mchango wangu niwapongeza TAHA chini ya C.E.O wao
Dk. Jacqueline Mkindi kwa kufanya vizuri sana katika kilimo na biashara ya
mazao ya  mbogamboga, matunda, maua na
viungo ambapo mauzo yake nje ya nchi yamekuwa yakiongezeka kwa kasi kubwa
kutoka Dola za Marekani milioni 412 mwaka 2015 hadi kufikia Dola za Marekeni
milioni 779 mwaka 2019.

Tunapozungumzia
uzalishaji lazima tujiulize maswali mengi, mwenendo wa uzalishaji wetu wa mazao
mbalimbali ukoje, hali ya wakulima wetu ikoje?, hali ya bei na masoko ndani na
nje ya nchi ya mazao yao ikoje? 

Serikali inasaidiaje kuongeza uzalishaji wa
mazao nchini? changamoto zilizopo za wakulima na wadau wa kilimo zinatatuliwaje,
mipango na bajeti tunazoidhinisha zinawagusa vipi wadau wa sekta?

Kwa
kifupi sekta ya kilimo inakabiliwa na mizigo mizito ya changamoto kama
ifuatavyo 

(i)
Upungufu mkubwa wa wataalamu wa ugani, katika maeneo ya kilimo hakuna wataalamu
wa kilimo na hivyo wakulima walio wengi hawana wa kuwaelekeza mbinu bora za
kilimo, magonjwa ya mimea na matumizi sahihi ya viuatilifu wanalima wenyewe
hawana wa kumsaidia.

Mfano katika Jimbo la Kisesa kuna maafisa ugani 15 tu kati
ya vijiji 50 na Wilaya ya Meatu kwa ujumla ina maafisa ugani vijijini 33 tu
kati ya vijiji 109 tu na kwa hotuba ya Mhe. Waziri anakiri kuwa maafisa ugani
waliopo ni 6, 704 wakati mahitaji ni 20,528 kwa takwimu hizi ni wazi kuwa zaidi
ya vijiji 7,000 havina afisa ugani hapa nchini.

Kwa
nini Serikali imeruhusu upungufu huu uwepo?, huku tunasema kilimo ni uti wa
mgongo wa taifa letu lakini hatuwekezi vya kutosha, ni nani anayesaidia
wakulima wetu kupambana na magonjwa ya mazao yao?

Ni nani anayesaidia kuongeza
uzalishaji mashambani?, nauliza maswali haya muhimu kwa kuwa hata maafisa ugani
waliopo hivi sasa wako kama picha tu kwa kuwa hawana usafiri wala posho ya
kuwawezesha kuyafikia mashamba ya wakulima.

Kwanini
Serikali isiamue leo hii kuajiri maafisa ugani kila kijiji ili kuongeza tija
katika kilimo?. Kwa nini Serikali isigawe pikipiki  na posho ya kila mwezi kwa maafisa ugani ili
kuwawezesha kuwafikia wakulima? 

Nimpongeze sana Mhe. Waziri kwa kuamua kupeleka
pikipiki 1,500 kwa Mikoa ya Dodoma, Singida na 
Simiyu na bila kusahau maafisa ugani wa Jimbo langu la Kisesa ambao
wanafanya kazi kubwa ya kujituma na wamejitolea kwa muda mrefu hivyo kwa mgao
huu ni haki yao kupata pikipiki wote.

(ii)
Upatikanaji wa mbegu bora, Waziri ameeleza uzalishaji wa mbegu nchini ambapo
amekiri kuwa uzalishaji ni mdogo na sehemu kubwa tunategemea mbegu kutoka nje
ya nchi. Kwanini taifa letu hadi leo liendelee kutegemea mbegu za kutoka nje?. 

Inawezekanaje  Taifa ambalo zaidi ya
asilimia 75 ya wananchi wake wanategemea kilimo alafu litegemee mbegu za
kuagiza kutoka nje ya nchi?.

Ni
kwanini hata mbegu zinazozalishwa hapa nchini zinauzwa kwa gharama kubwa kiasi
cha wakulima kushindwa kumudu gharama hizo na kuamua kutumia mbegu za asili
ambazo hazina tija, Mbaya zaidi hata taasisi zetu za Serikali zinazozalisha
mbegu nazo zinauza mbegu kwa gharama kubwa sana.

Mfano kilo moja ya mbegu ya
mahindi na mtama inauzwa kati ya sh. 6,500 mpaka 7,000 wakati kilo ya mahindi
inauzwa kwa sh 300 mpaka 500, ni nini kinachosabisha mbegu hizi kuuzwa kwa
gharama kubwa kiasi hicho?.

(iii)
Mazao mengi ya wakulima yanakabiliwa na magonjwa mfano zao la pamba na mahindi,
kumekuwepo wadudu sugu ambao hawafi hata baada ya kupuliziwa viuatilifu/dawa
hali inayopelekea hasara kubwa kwa wakulima wetu. Baadhi ya viuatilifu
vinavyoingizwa nchini kutoka nje havina uwezo wa kuua wadudu hali inayopelekea
hasara kubwa kwa wakulima wetu na taifa kwa ujumla.

Taasisi
zetu za utafiti zinafanya nini hadi tuwe na wadudu wasioweza kudhibitiwa? Nani
anawafidia wakulima hawa ambao kuingia gharama kubwa ya kununua viuatilifu na
baadae mazao yao kushambuliwa na kukosa mavuno?.

Waziri anakiri kuwa TPRI
ilipofanya ukaguzi wa kimaabara ukanda wa kusini peke yake yalipatikana maduka
15 yanayouza viuatilifu ambavyo havijasajiliwa, Inawezekanaje hali hii kutokea
usimamizi wa TPRI ukoje? Wizara ya Kilimo na Wizara ya Viwanda na Biashara mko
wapi hadi haya yatokee?

(iv)
Uanzishwaji wa vyama vya ushirika na kuua soko huria, inawezekana kuna baadhi
ya mazao ushirika wa aina hiyo ukahitajika lakini kwa wakulima wa pamba,
choroko, ufuta, dengu na alizeti utaratibu huu haufai ni kwanini uanzishe
ushirika wa kuwaondoa wanunuzi wengine wote na kubaki wao pekee? Tuelezwe tangu
ushirika uanzishwe nchini umesaidiaje upatikanaji wa soko na bei kwa wakulima
wa mazao haya?.

Mfumo
huu wa manunuzi umeleta changamoto kubwa sana kwa wakulima kwa kushindwa kupata
fedha zao kwa wakati kutokana na kukopwa kwa kuwa vyama vya ushirika havina
pesa na badala yake wanategemea mpaka wanunuzi binafsi waje kununua katika
ushirika wao, wamekuwa wakikusanya pamba au choroko bila kulipia.

Mwananchi
mwenye mahitaji ya fedha kwa ajili ya matibabu na ada za wanafunzi atafanyaje?
Baadhi ya vyama vya ushirika vimepata hasara na kushindwa kulipa madeni ya
wakulima nani anawafidia wakulima hao?

Katika
Jimbo langu kuna baadhi ya wakulima wanadai madeni kwa zaidi ya miaka mitatu
sasa bila msaada wowote kutokana na pamba kuungua na hasara za vyama vya
ushirika, ajira zimekufa mfano katika kijiji kimoja kulikuwa na wanunuzi zaidi
ya 10 leo amebaki mmoja hali ambayo imeleta usumbufu mkubwa kwa wananchi kukaa
kwenye foleni kusubiri kuuza mazao yao lakini pia ajira za vijana zimekufa.

Waziri
anaeleza ushiriki wa vijana katika kilimo na biashara ya kilimo huku
wakiwaondoa kwenye mfumo wa biashara kwa kile kinachodaiwa ni ushirika, kwanini
tuanzishe ushirika wa kuua soko huria?, kwanini tusiwe na vyama vya ushirika
vya kushindana na wanunuzi wengine ili wakulima wachangue na wakauze kwa mwenye
bei nzuri. 

Lakini pia ninavyofahamu ushirika unaundwa na wanachama kwanini iwe
lazima kwa kila mtu hata hivyo Bunge hili lielezwe ni sheria gani
inayowalazimisha wananchi kuuzia mazao yao katika ushirika?

Katika
hotuba ya Waziri anathibitisha kuwa vyama vingi vya ushirika havina uwezo na
vina changamoto kubwa ya wizi na ubadhirifu wa fedha za ushirika akitolea mfano
vyama vikuu vya ushirika 35 vilifanyiwa ukaguzi na COASCO ambapo vyama 17
vilibainika kuwa na wizi na ubadhirifu wa fedha na mali za ushirika.

Vile vile
COASCO ilifanya ukaguzi katika vyama vya ushirika 6,021 ambapo vyama vya ushirika
289 tu  vilipata hati safi sawa na
asilimia 5 tu huku vyama vya msingi 5,732 vikipata hati mbaya sawa na asilimia
95. Kwa taarifa hizi za ukaguzi wa COASCO kwanini Serikali imeamua kuwahujumu
kiasi hiki wakulima wake?

Changamoto
kubwa ya wakulima na wadau wa sekta ya kilimo ni ukosefu wa masoko ya
uhakika  bei nzuri mazao yao na sababu
hii kwa kiasi kikubwa inasababishwa na nchi yetu kuuza mazao kama malighafi
katika masoko ya nje.

Hali hii inamepelekea wananchi kuuza mazao yao kwa  bei ya kutupa, kunahamisha ajira na
kunufaisha vijana wa mataifa mengine, 
watanzania wamegeuka kuwa manamba wa nchi za kigeni kuhaingaika na
kilimo wanaonufaika ni nchi za kigeni huku vijana waliowasomesha wenyewe kwa
gharama kubwa wakibaki hawana ajira. Kushindwa kukuza uchumi inavyostahili,
kushuka kwa mapato ya Serikali na kupungua kwa uwekezaji nchini.

Tanzania
inauza malighafi nje ya nchi na kununua bidhaa za viwandani yaani finished
product na kusababisha naksi kubwa katika biashara (imbalance of trade).

Kwanini
nchi yetu haina viwanda vya kuongeza thamani ya mazao? nini kilichotukwamisha
kujenga viwanda vya kuongeza thamani mazao yetu kabla ya kuyauza nje ya nchi?
mpaka lini wakulima na wadau na sekta ya kilimo wataendelea kunyonywa kwa
kukosa masoko na kupewa bei ndogo?, mpaka lini wananchi wataendelea kuuza
malighali katika masoko ya Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, Agoa, Jumuiya ya Afrika
Mashariki, India, China  SADC na nk.

Zipo
sababu nyingi zinazotufanya tukose viwanda vya kuongeza thamani mazao nchini kama
ifuatavyo:-

(i)
Ukosefu wa mitaji ya kujenga viwanda vya kimkakati na hapa ninamanisha viwanda
vikubwa vinavyoweza kutoa bidhaa zinazoweza kushindana na bidhaa zingine zozote
duniani, baadhi ya wawekezaji wetu wanaotaka kuwekeza kwenye sekta ya kilimo hawana
mitaji.

Tutaendelea
mpaka lini kusubiri wawekezaji wa kuja kujenga viwanda vikubwa vya nyuzi na
nguo zitokanazo na pamba?, tutaendelea mpaka lini kusubiri wawekezaji wakubwa
wa kuja kuwekeza viwanda vikubwa vya kubangua korosho yetu yote nchini?,  Tutaendelea mpaka lini kusubiri wawekezaji wa
viwanda vikubwa vya kusindika Michikichi, Parachichi, Mpunga, Alizeti, Mahindi
nk.

Ushauri
wangu kwa Serikali tuanze kutenga fedha kupitia bajeti ya kujenga viwanda
vikubwa vya kimkakati ambavyo vitawezesha kuongeza thamani mazao yanayozalishwa
na wananchi wetu. Tumeweza kwenye barabara, tumeweza kwenye umeme,
hatutashindwa viwanda.

Kwa
mfano tunaweza kuanza Kanda ya Ziwa kwa kujenga viwanda vikubwa vitano
vinavyotumia malighali ya pamba 1. Kiwanda cha Nyuzi, 2. Kiwanda cha nguo, 3.
Kiwanda cha vifaa tiba, 4. Kiwanda cha Mafuta, 5. Kiwanda cha chakula cha
mifugo.

Vile
Vile ukanda  wa Kusini mwa Tanzania,
tutenge fedha za kujenga kiwanda kikubwa cha kubangua korosho na kwa kufanya
hivyo kutatuwezesha kutokuuza tena pamba na korosho ghafi nje ya nchi na hivyo
kupata soko la uhakika, bei nzuri, ajira, fedha za kigeni  na mapato ya Serikali kuongezeka.

Hapa
sisemi kwamba sasa Serikali ifanye biashara isipokuwa kipaumbele cha kwanza ni
kuwa na kiwanda chetu suala la nani aendeshe ni uamuzi wetu wenyewe,  tunaweza kukabidhi sekta binafsi iendeshe,
tunaweza kuwakopesha watanzania wazalendo kujenga viwanda hivyo kwa masharti
nafuu ambayo ni pamoja na kuwadhamini na kuwapa muda mrefu wa kurejesha mkopo
huo hata kwa miaka 30.

Kwa
kuwa viwanda vinakavyojengwa vitapelekea kuwa na soko la uhakika la  mazao ya kilimo ya watanzania, vitatoa bei
nzuri ya mazao na hivyo kuongeza nguvu ya manunuzi (purchasing power) kwa
wananchi,  vitalipa kodi za Serikali, vitazalisha
ajira za watanzania, vitawezesha kupatikana kwa gharama nafuu bidhaa
zinazozalishwa kama nguo.

Jambo
la kushangaza pamba inanunuliwa kilo moja sh 1,050, ili kushona shati
zinahitajika kilo tatu zenye thamani ya tsh 3,450, shati likishonwa huko China,
Indonesia, Thailand, Vietnam na India  na
baadae kuuzwa nchini kati ya  sh 50,000
hadi 100,000. TUSIKUBALI HAYA YAENDELEE!

(ii)
Mfumo mbaya wa kodi (unsupportive taxation regime) ambapo unakuta kuna baadhi
ya kodi zinalinda viwanda vya nje kwa kuweka unafuu wa kodi huku viwanda vya
ndani vikitozwa kodi kubwa na kushindwa kushindana,  wawekezaji wetu wamelalamika zaidi ya miaka 10
sasa lakini hakuna muafaka  uliyopatikana
na wengine waliokuwa na nia ya kuwekeza waliacha na wengine walifunga viwanda
vyao na kufilisika.

Swali
la kujiuliza, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Viwanda na Biashara,  Wizara ya Fedha, TRA na Wadau wamefanya
tathmini mara ngapi na kubaini kasoro zilizopo katika baadhi ya kodi na hatua
gani zilichukuliwa, nimesoma hotuba ya Waziri wa Kilimo sijaona mahali popote
amelizungumzia suala hili  jambo hili
halijaguswa mahali popote licha ya ukubwa wa tatizo hili ambalo limekuwa
machinjio ya uwekezaji nchini.

Tumekuwa
na Sera, Sheria na Mipango zinazohamasisha uagizaji wa  bidhaa nje ya nchi badala ya kuzalisha ndani
ya nchi yetu, tunahamasisha ujenzi wa viwanda vya nje na kuua viwanda vya
ndani. Waziri alihaikishie Bunge hili itakapowasilishwa  Finance bill 2021 itazingatia suala hili.

(iii)
Kukosekana kwa ulinzi wa viwanda vya ndani, Leo hakuna ulinzi wa kutosha
wa  soko la ndani viwanda vya ndani
kunakopelekea ushindani usio wa sawa na wa haki, hivi leo bado kuna uingizaji
mkubwa wa bidhaa za kilimo kutoka nje ya nchi ambazo huingizwa nchini bila
kulipa kodi, zingine kupitwa na muda wa matumizi, zingine ni feki na bandia
zinapoingizwa nchini huuzwa kwa bei ndogo na kuua soko la ndani pamoja na kuua
viwanda na ajira nchini.

Mbinu
mbalimbali zimekuwa zikitumika ikiwemo kupitia bandari bubu, njia zisizo rasmi,
under declaration na under invoice, soko la ndani limevamiwa kwa kuwa hata
baadhi ya mazao yanayozalishwa nchini yamekuwa yakiingia kwa wingi kutoka nje
ya nchi.

Mfano  maembe, parachichi, nyanya, ma apple, carot
hali inayopelekea wakulima wetu kukosa soko wakiteseka kutembea kutwa nzima
kutafuta mteja wa fungu moja la maembe nk. mambo haya yanathibitisha
ukitembelea kwenye Super Market zetu

Wizara
ya Kilimo, Wizara ya Fedha, Wizara ya Viwanda na Biashara, TRA,  Vyombo vya Dola mko wapi?

(iv)
Kasi ndogo ya Serikali kusaka masoko ya mazao na bidhaa za Kilimo nchini, sioni
jitihada za makusudi zinazofanywa na Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano na Kimataifa kupitia Waheshimiwa Mabalozi wote
katika nchi mbalimbali wanazotuwakilisha hali hii imepelekea kukosekana kwa
masoko na bei nzuri ya mazao ya wananchi.