Mpina atumia hotuba ya rais wa zanzibar dkt hussein mwinyi kuwaumbua wanaotaka kufuta legacy ya hayati rais dkt magufuli

 

Mbunge
wa Kisesa, Mhe.  Luhaga Mpina akizungumza na waandishi wa habari jijini
Dodoma kuhusiana na mafanikio ya Serikali ya awamu ya tano na kuwataka
wananchi kuendelea kumuunga mkono Rais, Samia Suluhu Hassan katika
kuendeleza kupigania maendeleo ya Tanzania.

Na
Mwandishi Wetu, Dodoma

MBUNGE
wa Kisesa, Mhe. Luhaga Mpina ametumia hotuba ya Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali
Mwinyi kuwashukia vikali kikundi cha watu wanaojiita wakosoaji wanaobeza na
kukashifu mafanikio ya utawala wa
Serikali ya awamu ya tano wakidai ilijaa ufisadi.

Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dodoma, Mpina amehoji ni fisadi gani anayeweza kuongeza
mapato na kudhibiti matumizi ya Serikali, kudhibiti rushwa na ufisadi na
kuongeza bajeti ya maendeleo kutoka wastani wa asilimia 26 hadi asilimia 40 na ku
wezesha kuanza kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kwa fedha
zetu za ndani sambamba na kuboresha utoaji wa huduma za kijamii kwa wananchi.

Mpina
amehoji fisadi gani atenge na kutoa kiasi cha shilingi trilioni 1.01 kugharamia
elimu bila malipo kuanzia shule za msingi hadi sekondari, kuongeza bajeti ya
mikopo ya elimu ya juu kutoka bilioni 348.7 mwaka 2015 hadi  bilioni 450 mwaka 2020. Hatua ambayo
imewezesha watoto wa masikini na wanyonge kupata fursa elimu bila shida yoyote
tofauti na miaka ya nyuma ambapo watoto wa masikini walikosa fursa hiyo

Mpina
ameuliza ni fisadi gani ambaye anaweza kuongeza bajeti ya upatikanaji wa dawa na
  vifaa tiba kutoka sh. Bilioni 31 mwaka 2015
hadi sh. Bilioni 270 mwaka 2020.

“Ni
fisadi gani wa kununua vifaa vya kisasa, kusomesha madaktari bingwa hali
iliyopelekea kuwezesha na kuimarisha matibabu ya kibingwa nchini kwa magonjwa
ya moyo, figo, mifupa na ubongo ambapo imesaidia kupunguza idadi ya rufaa
kwenda nje ya nchi kwa asilimia 95. Leo huduma hizi zinapatikana hapa nchini
ambapo huko nyuma watu wengi walipoteza maisha kwa kukosa huduma”alihoji Mpina.

Pia
Mpina ameuliza ni fisadi gani anayeweza kufungua njia zote za mawasiliano tangu
akiwa Waziri na baadae Rais ambapo barabara za lami zimetandazwa kila sehemu,
madaraja makubwa ya kimkakati yamejengwa, meli na reli mpya kujengwa na
zilizokufa kufufuliwa, Ndege mpya 11 zimenunuliwa na viwanja vya ndege kujengwa
sehemu nyingi ambapo imewawezesha watanzania kufika na kutamba kila kona ndani
na nje ya nchi.

“Ni
fisadi gani anayeweza kusambaza umeme kila kijiji ambapo vijiji vilivyopata
umeme vimeongezeka kutoka 2,018 mwaka 2015 hadi vijiji 9,112 mwaka 2020, kuanza
kutekeleza mradi mkubwa wa Bwawa la Nyerere ambao unagharimu trilioni 6.5 ambao
utawezesha nchi yetu kuzalisha umeme wa 
Megawati 2115 wa bei nafuu” aliongeza Mpina.

Mpina
amebainisha kuwa ni fisadi gani afute mikataba ya kifisadi mingi iliyokuwa
ikilinyonya taifa mfano IPTL, Aggreko na Symbion ambayo ilikuwa ikiligharimu
taifa bilioni 719 kwa mwaka leo fedha hizi zinatumiwa kwenye shughuli za
maendeleo ya wananchi.

“Ni
fisadi gani aliyeweza kuumaliza ufisadi wenyewe, rushwa, ujangili, ujambazi,
uvuvi haramu, madawa ya kulevya, mauaji ya vikongwe na albino, ajali za
barabarani, aliyekomesha dhuluma kwa wananchi wanyonge”.alihoji.

Hivyo
Mpina amesema tutaendelea kumkumbuka na kumuenzi Mbabe wa Vita Mtetezi wa
Wanyonge, kipenzi cha wengi Hayati Dk.
John Pombe Joseph Magufuli
kwa wema wake usiomithilika na kwa  jinsi alivyopigana kiume kupambania maendeleo
ya nchi yake.

“Naungana
na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk.  Hussein Ali
Mwinyi
aliyesema kuwa ni nadra sana kupata viongozi wa aina
ya Dk. Magufuli”alisema Mpina.

Mpina
ameongeza kuwa tumeshuhudia pia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa maarufu kama
Baraza la 75 lililokamilisha mkutano wake maalum uliolenga kumkumbuka na
kumuenzi Rais wa awamu ya tano wa Tanzania, Hayati Dk. John Pombe Joseph
Magufuli, ambapo Umoja huo umetambua uwezo na jitihada alizokuwanazo JPM za
kupambana na Rushwa na Ufisadi.

Pia
kuboresha huduma, kujenga miradi mikubwa ya maendeleo na mageuzi makubwa
ya
uchumi kwa muda mfupi ambao umepelekea Tanzania kuingia uchumi wa kati
katika kipindi kifupi cha miaka 5 badala ya miaka 10 iliyotarajiwa.
Umoja huo wa Mataifa umetambua kuwa JPM aliwapenda sana Watanzania na
aliipenda nchi yake.

Aidha
Mpina amesema tunakumbuka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa ziliamua kupeperusha
bendera zake nusu mlingoti tarehe 26.03.2021 siku ya mazishi ya Dk. Magufuli
ambapo pia tulishuhudia zaidi ya watu bilioni 4 duniani kote wakifuatilia tukio
la mazishi yake.

“Hiyo
ni heshima kubwa sana kwetu watanzania na duniani kwa ujumla kwa kuwa si kila
kiongozi anapofariki kwa nafasi ya urais anapewa heshima hiyo kama aliyopewa
Hayati Rais Magufuli”alisema.

Pia
Mpina amepongeza Rais, Samia Suluhu Hassan Mwanamke Shupavu na Jasiri kwa
uamuzi wake wa kukubali kuendesha kongamano maalum la kitaifa la viongozi wa
dini kama sehemu ya kuendelea kuenzi na kutambua mchango Hayati Dk. John Pombe
Magufuli uamuzi huu umegusa sana mioyo ya watanzania.

“Ndio
maana nina kila sababu ya kusema wale wanaotumia kila aina ya mbinu kufuta
‘legacy’ ya Dk. Magufuli ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu, watanzania
wanamfahamu JPM kwa namna alivyoyagusa maisha yao,  hivyo wenye chuki binafsi waache mara moja na
badala yake tuungane na Rais wetu mpendwa 
Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa
Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
katika kuendeleza mafanikio na
kulijenga taifa letu. Ninajua Mungu wetu wa mbinguni kamwe hatatuacha”amesema
Mpina.

Hata
hivyo Mpina amesema pamoja na mafanikio mengi tuliyoyapata kwenye eneo la
ukusanyaji wa mapato ameshauri Serikali kufanya tathmini ya vyanzo vya mapato
ili kuibua fursa mpya na kuondoa changamoto zinazokwaza ukusanyaji wa mapato
ili kuongeza mapato ya Serikali.

Pia
ameshauri Wizara na taasisi zenye vyanzo vya mapato ziwasilishe fursa na
changamoto zilizopo katika Kamati ya Bunge ya Bajeti kabla ya kusomwa Bajeti ya
Serikali na Finance Bill kwa nia ya kuongeza wigo wa kukusanya kodi na kuondoa
changamoto zilizopo.

Mpina pia ameshauri Serikali ikubali kuwekeza fedha
katika miradi na maeneo yanayoweza kuongeza mapato ya Serikali kwa muda mfupi
na kuendelea kuimarisha usimamizi kwa mujibu wa sheria.