Mali za hoteli ya impala kupigwa mnada

 Mahakama kuu Kanda ya Arusha,imeridhia kuuzwa kwa Mali za mmiliki wa hotel ya Impala na Naura Spring ikiwemo viwanja vinne ili kufidia malipo ya wafanyakazi 238 yanayofikia kiasi Cha zaidi ya sh,milioni 500.


Aidha mahakama hiyo pia imeridhia maombi ya benki ya biashara ya NBC inayoidai hotel ya Impala kiasi Cha zaidi ya sh, bilioni 1.5 ili fedha zitakazobaki baada ya Mali za mdaiwa kuuzwa na kulipwa wafanyakazi zikabidhiwe kwa benki hiyo na sio kwa mdaiwa.

Akitoa hukumu hiyo mapema leo jaji wa mahakama hiyo, Mohamed Gwae alisema baada ya mahakama kupitia pingalizi za mmiliki wa hoteli hizo akipinga uamuzi wa msajili wa mahakama kuu Kanda ya Arusha, masijala Ndogo ya kazi juu ya kuuzwa kwa Mali zake ili kufidia malipo ya wafanyakazi, ameona hayana mashiko.

Jaji Gwae aliamuru viwanja namba 20,21,22 na 23 vilivyopo block B Uzunguni, jijini Arusha kuuzwa na kufidia mishahara ya wafanyakazi wapatao 238 wakiwemo 68 wa hotel ya Naura wanaodai zaidi ya sh,milioni 107 na wafanyakazi 167 wa hoteli ya Naura wanaodai sh, milioni 397 huku magari na jenereta yanayoshikiliwa na dalali wa mahakama yaendelew kushikiliwa.

Awali upande wa waleta maombi ukiwakilishwa na wakili ,Ngereka Miraji ulipinga afisa kazi Mkoa wa Arusha kusimamia madai ya wafanyakazi hao ukidai kwamba hana mamlaka kisheria ispokuwa kamishna kazi pekee ,madai ambayo yalitupwa na jaji Gwae.

Naye wakili anayeiwakilisha benki ya NBC Willbard Masawe kutoka kampuni ya uwakili ya Mawala alisema benki ya NBC inaidai hoteli ya impala Zaidi ya bilioni 1.5 na hivyo ameishukuru mahakama kwa kukubali ombi lao kwamba fedha itakayobaki baada ya malipo ya wafanyakazi ziwekwe kwenye akaunti yao nasio kurudishwa kwa mdaiwa.

Kwa upande wa kaimu afisa kazi mfawidhi Mkoa wa Arusha, Emmanuel Mweta ameishukuru mahakama kuu kwa kutoa maamuzi yaliyowatendea haki wafanyakazi 238 wa Impala.na Naura Hotel baada ya mahakama hiyo kuridhia kuuzwa kwa Mali za mdaiwa ili kufidia malipo ya mishahara yao.

Baadhi ya wafanyakazi waliokuwa wamefurika mahakamani hapo akiwemo Mwenyekiti wao ,Jacob Joel wameishukuru mahakama hiyo kwa kuwatenda haki walidai kuwa wamesotea malipo yao kwa zaidi ya miezi 16 ,hivyo wanaimani Sasa watalipwa stahiki zao zote .


Ends…








IMG_20210208_112646_439.jpg

 

IMG_20210208_105225_283.jpg