Tsc yaainisha makosa sugu ya walimu nchini

Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi
wa Walimu (TSC), Moses Chitama, akiwasilisha mada kuhusu maadili katika
mkutano wa pili wa Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania
Bara , uliofanyika jijini Dodoma, Januari 5, 2021.


Mkurugenzi kutoka Ofisi ya Rais,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), anayesimamia Elimu ya
Awali na Msingi, Susan Nussu, akisisitiza kuhusu maadili ya walimu,
wakati wa mkutano wa pili wa Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi
Tanzania Bara (hawapo pichani), uliofanyika jijini Dodoma, Januari 5,
2021.


Sehemu ya Wajumbe wa Mkutano wa
Pili wa Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania Bara (hawapo
pichani), wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa wakati
wa mkutano huo uliofanyika jijini Dodoma, Januari 5, 2021.



Na Veronica Simba


Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi
wa Walimu Tanzania (TSC), Moses Chitama ametaja makosa sugu yanayofanywa
na baadhi ya walimu nchini kuwa ni utoro, ulevi pamoja na kujihusisha
kimapenzi na wanafunzi.


Aliyasema hayo Januari 5 mwaka
huu, wakati akiwasilisha mada kuhusu maadili, katika Mkutano wa Pili wa
Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania Bara, uliofanyika
jijini Dodoma.


Chitama alifafanua kuwa, TSC ikiwa
ni Mamlaka ya Nidhamu kwa Walimu nchini, imebaini kuwa makosa hayo
matatu ndiyo yanaongoza kuripotiwa kwa sasa, miongoni mwa makosa kadhaa
yanayohusiana na utovu wa nidhamu katika kada husika.


Aliendelea kueleza zaidi kuwa, kwa
kulitambua hilo, Tume imekuwa ikitumia mbinu mbalimbali katika
kuhakikisha suala hilo linatokomezwa ikiwemo kutoa elimu kwa wahusika na
kuchukua hatua kali za kinidhamu kwa wanaothibitika kutenda makosa
hayo.


Aidha, Kaimu Katibu Chitama
alitumia jukwaa hilo kukemea vikali walimu wenye tabia hiyo na kuwataka
kuacha mara moja huku akisisitiza kuwa Serikali kupitia Tume husika,
haitawavumilia.


Alisema kuwa walimu ndiyo chanzo
kikuu cha maendeleo ya nchi kwani ndiyo wamepewa dhamana ya kuwalea
kiakili na kimwili watoto, ambao wanategemewa na Taifa kuja kuwa
viongozi na wataalamu katika nyanja mbalimbali, hivyo wanapaswa kutimiza
wajibu wao ipasavyo.


“Ninyi walimu msiposimamia maadili
ya taaluma yenu pamoja na maadili ya watoto mnaowafundisha, tutakuwa na
Taifa bovu, lililokosa mwelekeo na lenye mmomonyoko wa maadili.


Akitoa takwimu, Chitama
alibainisha kuwa, katika kipindi cha miaka mitano (2016 – 2020), jumla
ya walimu 9,819 walifunguliwa mashauri na waajiri wao, ambapo 5,441 kati
yao walifukuzwa kazi.


Aidha, alieleza kuwa, katika
kipindi hicho, walimu 1,803 walipewa maonyo na makaripio, 520
walipunguziwa mishahara, 244 walisimamishiwa nyongeza ya mishahara na
403 waliteremshwa vyeo.


Kwa upande mwingine, alisema walimu 149 walilipwa fidia na wengine 438 kuachiwa huru.


Akihitimisha, Kaimu Katibu Chitama
aliwataka walimu kuwachukulia wanafunzi kama watoto wao wa kuzaa hivyo
wawatendee sawa na wanavyotendea familia zao.


Akizungumza katika Mkutano huo,
Mkurugenzi kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI), anayesimamia Elimu ya Awali na Msingi, Susan Nussu,
aliwasisitiza walimu kujiepusha na masuala ya udanganyifu wa mitihani
katika shule zao.


Alisema wengi hutenda kosa hilo
kwa tamaa ya kujitafutia sifa ya ufaulu katika shule zao lakini
akawataka kukumbuka kuwa kitendo hicho huwaponza wanafunzi wao kwa
kuwasababishia kufutiwa matokeo.


Aidha, aliwataka Walimu Wakuu wa
Shule za Msingi kuacha tabia ya kuwapanga walimu wazembe na wavivu
kufundisha madarasa ya awali badala yake wawapange walimu wenye weledi
ili waweze kuwajengea watoto msingi mzuri wa elimu.


Mkutano huo wa Pili wa Umoja wa
Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania, uliongozwa na kaulimbiu
isemayo uongozi na usimamizi makini wa elimu, utaimarisha Tanzania
katika uchumi wa kati.