MKUU wa Mkoa wa Tanga Martine Shigella akizungumza wakati akifungua mafunzo ya ukaguzi wa dawa yaliyofanyika katika ukumbi wa wizara ya afya hospitali ya Bombo kulia ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga (RMO) Dkt Jonathan Budemu
Mratibu wa Ofisi
za Kanda na Serikali za Mitaa, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Henry
Irunde akizungumza jambo wakati wa mafunzo hayo
MKUU wa Mkoa wa Tanga Martine
Shigella ameitaka Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kuhakikisha wanatoa elimu
zaidi kwa wananchi ili waweze kufahamu ubora wa dawa sambamba na kuzingatia
muda wa mwisho wa matumizi hususani maeneo yaliyopo mipakani.
Shigella aliyasema hayo wakati wa
akifungua mafunzo ya ukaguzi wa dawa yaliyofanyika katika ukumbi wa
wizara ya afya hospitali ya Bombo ambapo amesema kuwa hata wananchi wanawajibu
wa kutambua dawa hizo na wakijiwekea utamaduni wa kusoma ili kutambua
muda wa matumizi ya dawa hizo.
Alisema kwamba iwapo wananchi
wakipatiwa elimu hiyo itawasaidia kwani mtumiaji mmoja mmoja akinunua dawa na
akajenga utamaduni wa kusoma na kujua muda wa matumizi ya dawa yenyewe itasaidia
kutambua ambazo zimekwisha muda wake ambazo hazina ubora.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema kwamba kila
kifaa tiba na kila aina ya dawa kabla haijaingia kwenye matumizi lazima mamlaka
hiyo ijiridhishe ubora wake kama unakidhi mahitaji ya binadamu na iweze
kusajiliwa na kuingia kwenye soko rasmi.
“Kama kuna dawa yoyote ambayo inatumika
au kifaa tiba ambacho kinatumika na hakijasajiliwa na TMDA hakuna maelezo
mengine zaidi ya kusema hawa ni wahujumu uchumi kama wahujumu uchumi wengine.”
Alisema Shigella.
Awali akizungumza, Mratibu wa Ofisi
za Kanda na Serikali za Mitaa, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Henry
Irunde amesema kuwa katika Mkoa wa Tanga pamoja na udhibiti kwenye vituo vya
forodha na soko umeimarishwa.
Irunde amesema kuwa bado kuna
changamoto ya uwepo wa dawa ambazo hazijasajiliwa na baadhi ya maduka ya dawa
kutokuwa na vibali ikiwemo kukosa wataalamu wenye sifa stahili hivyo maduka
hayo yanapaswa kukaguliwa mara kwa mara ili kuhakikisha uzingatiaji wa sheria.
Pia amesema kuwa mafunzo hayo
yamezingatia masuala muhimu kwa wakaguzi ikiwa pamoja na kuwakumbusha wakaguzi
juu ya maadili na taratibu za kazi katika kutimiza majukumu yao.