Wazee wakionesha bango kutaka zahanati. |
Jiwe la msingi lililowekwa na kiongozi wa Mbio za mwenge wa Uhuru mwaka 2013,Rachel Kasanda kwenye jengo la zahanati ya Azimio Mswiswi.(Picha zote na Joachim Nyambo) |
Jengo la zahanati lililotelekezwa. |
Na
Joachim Nyambo,Mbarali.
WAJAWAZITO
kusafirishwa kwa Bodaboda na Powertiller kutoka kijijini kwao kwaajili ya
kwenda kujifungua wanapopatwa na uchungu hadi mahali wanapoweza kupata huduma
stahiki kumesababisha Baraza la wazee wa kata ya Kongolo wilayani Mbarali
kupaza sauti zao wakitaka kuendelezwa kwa mradi wa ujenzi wa Zahanati ya kijiji
cha Azimio mswiswi uliokwama tangu mwaka 2014.
Kwa
mujibu wa uongozi wa kijiji cha Azimio Mswiswi mradi wa ujenzi wa zahanati ya
kijiji hicho uliibuliwa na wananchi ambao waliandelea na ujenzi wa jengo kuu
hadi hatua ya kupaua lakini mara tu baada yam bio za mwenge wa Uhuru mwaka 2014
ambapo kiongozi wa Mwenge mwaka huo Rachel Kasanda kuweka jiwe la msingi kwenye
jengo hilo ikawa mwisho wa mwendelezo wake.
Kutokana
na kukosekana kwa zahanati kijijini hapo wakazi wameendelea kulazimika kutembea
umbali mrefu hadi kijiji cha Kongolo Mkola kufuata huduma za matibabu ambapo
hulazimika kutumia gharama kusafiri kwenda na kurudi.
Wajawazito
kijijini hapo wanatajwa kuwa miongoni mwa wahanga wakubwa wa kadhia hiyo
kwakuwa kutokana na kutokuwepo kwa usafiri wa gari wanapohitaji huduma ya
matibabu ikiwemo huduma salama ya kujifungua wanapofikwa na uchungu hulazimika
kusafirishwa kwa usafiri wa bodaboda au Trekta ndogo maarufu kama Powertiller
huku barabara nayo ikiwa si rafiki hususani nyakati za masika.
Mwenyekiti
wa kijiji cha Azimio Mswiswi,Aliagiza Ngwipa alisema mradi huo ulianza
kutekelezwa kwa nguvu ya wananchi toka mwaka 2013 lakini ulitelekezwa toka siku
ulipowekewaa jiwe la msingi katika mbio za Mwenge wa uhuru mwaka 2014.
Ngwipa
alikiri kuwa kutokamilika kwa mradi huo kumewafanya wakazi hususani wajawazito
na wazee kupata wakati mgumu kusafiri kufuata matibabu hatua iliyowafanya
wapaze sauti zao na kutaka kujua nini mpango wa Serikali katika kukamilisha
ujenzi huo ili waanze kupata matibabu jirani.
Alisema
kwa sasa wakazi wa kijiji hicho wanalazimika kutembea umbali wa zaidi ya
Kilometa tano kufuata matibabu katika Zahanati ya kijiji cha Kongolo Mkola
ambacho ndicho pekee kina zahanati katika vijiji vyote vitano vinavyounda kata
hiyo.
Aliongeza
kuwa kama uongozi wa kijiji wamefuatilia Halmashauri kujua hatma ya jengo lao
baada ya kuona linaanza kuchakaa likiwa limeezekwa na kuwekwa milango na
kilichosalia ilikuwa uwekaji wa madirisha,kusakafia na kupiga sealingboard.
“Tumefuatilia
sana baadaye uongozi wa wilaya umetuagiza tujenge kwanza choo..tunaendelea
kujichangisha wanakijiji mpaka ujenzi wa choo umefikia hapa tulipo.Kwa tathmini
ya watu wa wilayani walisema gharama ya choo inaweza kawa milioni tano.Kwa
upande wa jengo mafundi wetu wamefanya tathmini wamesema karibia Milioni 10
zinaweza kukamilisha kazi zilizosalia ili jengo liweze kufanya kazi.”
Alisema
“Sera
ya Serikali inasema kila kijiji kiwe na zahanati na kila kata kituo cha afya
lakini huku kwetu haijatekelezwa.Pamoja na jitihada zilizofanywa na wananchi
kuanzisha ujenzi.Halmashauri baadaye ilichangia fedha kidogo lakini baada ya
kuweka jiwe la msingi kukawa kimya.Tunasubiri baada ya kujenga choo wanakijiji
tuone mkono wa Serikali na sisi ili tupate matibabu stahiki.Vipo vitongoji
vingi vya wafuagi ambavyo vipo mbali zaidi ya hapa tulipo ambavyo watu wake
wangerahisishiwa kwa kupata matibabu hapa.” Aliongeza mwenyekiti huyo.
Baraza
la wazee linasema linasikitishwa zaidi linaposikia jitihada zinazofanywa na
wananchi na wadau kwenye maeneo mbalimbali ambazo wanasikia kwenye vyombo vya
habari nchini kuwa zinaungwa mkono na Serikali na hatimaye wananchi hususani
wajawazito na wazee kuanza kunufaika na miradi ya huduma za afya jirani na
kuhoji kwa nini kwenye kata yao isiwezekane.
Katibu
wa Baraza la Wazee wilaya ya Mbarali,Ezron Kapwela alisema imefika wakati wadau
kuhakikisha ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho unakamilika ili kuepusha pia
vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga wanaohitaji huduma rafiki wakati wa
kujifungua na kuzaliwa.
“Tunaona
na kusikia kila siku kupitia vyombo vya habari kulee mradi umekamilika….kuleee
mradi wananchi wameibua Serikali imewasaidia umeanza kutoa huduma..sijui wapi
wajawazito sasa wameacha kutembea umbali mrefu…na maeneo mengine ni ya hapahapa
mkoani kwetu Mbeya..sasa tunajiuliza hivi sisi tunashindwa wapi?.Hatuwezi
kulifumbia macho jambo hili maana wakati wa mvua nyingi barabara pia huku
kwenye maeneo mengi ya kata yetu hayapitiki kwakuwa maji yanatapakaa na hauwezi
kujua barabara iko wapi” alisema Kapwela.
Mkazi
wa kijiji hicho Mary Kyando anasema “Miaka yote zahanati haiishi..wagonjwa
wanafia njiani..mtoto anashikwa na uchungu hapa anabebwaje kwenye bodaboda
mpaka kule zahanati iliko..yaani anafungwa minati kwenye bodaboda utafikiri
mzigo wa kuni.Tunataka tuone matunda ya michango yetu.”
Akimwakilisha
mganga mkuu wa mkoa wa Mbeya kwenye,Afisa kutoka Ofisi hiyo,Dk Peter Mereki
aliwapongeza wakazi wa kijiji hicho kwa kuchukua uamuzi wa kuanzisha mradi na
kuwahakikishia kuwa Serikali haiwezi kuacha mchango wao ukapotea bure bali
jitihada za dhati zitafanyika ili kuikamilisha zahanati ianze kutoa huduma.
Dk
Mereki aliitaja kata ya Kongoro kuwa miongoni mwa maeneo mkoani hapa yaliyo na
mwamko mkubwa katika kujiunga na Bima ya Afya hivyo ni muhimu wakazi wake
wakajengewa mazingira ya kupata huduma za afya kwa karibu ili wafaidi matunda
ya mwamko wao.
Aliwataka
wakazi wa vijiji vingine vya kata hiyo kuiga mfano wa wenzao wa Azimio Mswiswi
kwa kuanzisha ujenzi wa zahanati wao wenyewe badala ya kusubiri mpaka Serikali
ikawaanzishie hatua aliyosema inaweza kuwachelewesha zaidi.
“Hatukuja
hapa kwaajili ya kuona tu..Yote mliyoyafanya tumeyaelewa na kuyathamini.Huduma
za matibabu tunaendelea kuboresha siku hadi siku.Suala la milioni 10 za
kumalizia jengo nitaliwasilisha kwa uzito wake.Ninyi mmejitambua mmeitambua
mpaka Sera.Na mmejitolea bado choo tu ambacho nacho mmefikia hatua nzuri.Vijiji
vingine navyo viige mfano wenu.”alihimiza Dk Mereki.