Jukwaa la Wanawake
na wanasiasa nchini (TWCP/ULINGO) wamelaani tabia za baadhi ya wanasiasa
kutumia lugha za vitisho, uvunjifu wa amani na utulivu, katika kipindi
cha nngwe ya mwisho ya kampeni za kuelekea uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Aidha wameshauri
kuchukuliwa hatua kwa baadhi ya vyama vya siasa vinavyofanya siasa za
udini kwa kuhusisha viongozi wa dini katika kampeni zao, huku vikitambua
kuwa ni kinyume cha Katiba ya nchi na Sheria ya Vyama vya siasa.
Akizungumza kwa njia
ya simu wakati wa Mkutano wa Jukwaa la Wanawake viongozi kutoka vyama
mbalimbali vya siasa, Taasisi za kijamii na makundi ya wenye Ulemavu kwa
kushirikiana na Jukwaa la Wanawake Wanasiasa (TWCP/ULINGO) Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista
Muhagama, alisema jukumu lililopo kwa wanawake wakati huu ni
kuhakikisha amani inadumishwa katika uchaguzi.
Alisema wanawake
wanapaswa kuwa mawakala wa amani ili kusaidia Watanzania kuwa na umoja
wa kitaifa na kuondokana na mihemko yenye matokeo hasi nchini.
Aliongeza kwa
kuwataka wanawake na jamii nyingine nchini, kujitokeza kushiriki kupiga
kura kwani ndio wakati sahihi wa kuchagua viongozi watakaokidhi haja na
matakwa yao.
Kwa upande wake
Mratibu wa Jukwaa hiloambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha UDP, Saumu
Rashid, alisema kwa umoja wao wanalaani tabia zilizoanza kujitokeza
kutoka kwa baadhi ya wanasiasa wakitumia lugha za vitisho na uvunjifu wa
amani na utulivu.
“Katika kipindi hiki
ambacho tunamalizia kampeni, zimekuwa zikizuka lugha na matamko
mbalimbali yanayoashiria uvunjifu wa amani ni vyema tuwe makini,”
alisema.
Aidha alishauri
kuchukuliwa hatua kwa badhi ya vyama vya siasa vinavyoendeleza siasa za
udini kwa kuhusisha viongozi wa dini kwenye mikutano ya kampeni zake,
jambo ambalo ni kinyume cha katiba na Sheria ya Vyama vya Siasa.
“Tunavitaka vyama
vya siasa kutowatumia viongozi wa dini kwa maslahi yao binafsi ili
kutugawa Watanzania hususani katika kipindi hiki cha uchaguzi na baada,”
alisema.
Alisema kwa mujibu
wa Ibara ya 20(2)(a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya
mwaka 1977 na kifungu cha 9(2)(a) cha sehria ya Vyama vya Siasa sura ya
258, vinakata Chama cha siasa kufanya siasa za udini.
Alipongeza Jeshi la
Polisi, kwa namna linavyofanya kazi kwa weledi, uadilifu katika ulinzi
wa raia na mali zao hususan kwenye kipindi cha Uchaguzi.
Naye Mjumbe wa
Jukwaa hilo ambaye pia ni mwakilishi wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa
Chama Cha Mapinduzi (UWT), Ottow Mgeni, alisema kwa kuwa wanawake ndio
wasimamizi wa njamii ni wajibu wao kukemea viashiria vyote vya uvunjifu
wa amani nchini.
Alisema wanasiasa
wanatakiwa kutambua kuwa mshindi yeyote wa Uchaguzi huo, atatokana na
chaguo la wananchi hivyo wasijihusishe katika njama zozote zenye dhamira
ya kuhatarisha amani ya nchi.