Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi {CCM} mkoa wa Iringa wameshauriwa kutumia kipindi hiki cha Uchaguzi mkuu wa Rais,Wabunge na Madiwani kuwachagua waogombea walio na nia njema ya kuwaletea maendeleo katika njanja mbalimbali za kimaendeleo.
Hayo yamesemwa na mwenyekiti wa CCM mkoa wa Iringa, DKT. Abel Nyamahanga katika ukumbi wa Chama Cha Mapinduzi Iringa Mjini, akifungua shughuli ya uchaguzi wa wabunge wa Viti maalum watakaowakilisha mkoa wa Iringa katika bunge la 12.
“Wanawake tuhakikishe tunawachagua wagombea wa viti maalum walio na nia njema ya kuwasaidia na kuwaletea maendeleo ya kweli. Wanawake mnachangamoto nyingi lakini bila nyie wenyewe kuamua zinaweza zisimalizikie au kupungua”
DKT. Nyamahanga amewataka wanawake kuacha tabia ya kuwachagua wagombea wanaotumia muda wao kuomba kura kwa kutumia uwezo wa kifedha kuwarubuni wapiga kura waweze kuwapatia nafasi na kuwakimbia baada ya kuchaguliwa.
“Msifanye makosa kwa kuwachagua wagombea ambao wanatumia fedha katika kipindi hiki cha uchaguzi kuwaomba kura za Ndio. Wagombea wa namna hii ni wa hatari watakimbia mtakapowachagua”
Nae Msimamizi mkuu wa Uchaguzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Alli Hapi ameahidi kuwashughulikia wagombea wote watakaobanika kutumia rushwa kuwarubuni wapiga kura katika kipindi hiki cha Uchaguzi ili kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na wa haki kwa watu wote.
“Sisi kama serikali tumejipanga kuhakikisha hakuna vitendo vya rushwa katika kipindi hiki cha uchaguzi. Hatutafumba macho kwa mtu yeyote atakayekamatwa kwa kupokea au kutoa rushwa ili aweze kupatiwa nafasi ya kuwa kiongozi”
Aidha Hapi amewataka wapiga kura kuchagua viongozi watakaoweza kwenda na kasi ya viongozi wa serikali ya DKT John Magufuli ambaye amejidhihirisha kama moja ya kiongozi mwenye nia ya kuwasaidia wananchi wa Tanzania.
“Wanawake mchague viongozi watakaokwenda sawa na kasi ya Rais wetu DKT. John Pombe Magufuli kuhakikisha tunawaletea maendeleo ya kweli wananchi wa Tanzania kwa sababu serikali ya awamu ya tano imejipambanua kuwasaidia wananchi wake”
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa CCM Mkoa wa Iringa, Mama Nicolina Lulandala amewaomba wanawake wa Mkoa wa Iringa kuwa watulivu katika kipindi hiki cha kuwachagua viongozi watakaowakilisha kundi la wanawake wa mkoa wa Iringa.