Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya Kilimo wamekutana kupitia rasimu ya Mkakati wa Kitaifa wa Mawasiliano ya kudhibiti sumukuvu ili kuwezesha jitihada za kukabililiana na tatizo hilo miongoni wananchi, hususan wakulima wa mazao.
Akizungumza kwenye mkutano huo, mjini Morogoro (16.06.2020) Kaimu Mkurugenzi wa Usalama wa Chakula kutoka Wizara ya Kilimo, Dkt.Honest Kessy alisema lengo la serikali ni kuhakikisha elimu juu ya tatizo la sumukuvu inatolewa kwa wakulima na wananchi kwa usahihi.
Alisema kuwa,mawasiliano yasipowekwa vizuri, yanaweza athiri wakulima kutozingatia kanuni bora za k ilimo katika kumaliza tatizo la sumukuvu.
“ Mkutano huu unalenga kupokea maoni ya wadau wa kilimo kuhusu kukamilisha mkakati wa wa Taifa mawasiliano ili wakulima na wananchi waweze kujua namna ya kudhibiti tatizo la sumukuvu kwenye mazao hususan mahindi na karanga” alisisitiza
Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa kudhibiti Sumukuvu (TANIPAC) Ndugu Clepin Josephat alisema lengo la mradi huu ni kuhakikisha nchi inakuwa na usalama wa chakula na afya za walaji zinalindwa kwa mazao kutochafuliwa na sumukuvu.
Clepin alipongeza jitihada za wadau waliowezesha kuandaliwa kwa rasimu ya mkakati wa mawasiliano ambao utasaidia kufikisha elimu kwa umma kwa njia rahisi na sahihi.
Takwimu zinazonyesha kuwa tangu kugundulika kwa tatizo la sumukuvu kwenye mazao mwaka 2016, watu 68 waliougua na kulazwa kutokana na kula chakula kilichochafuliwa na sumukuvu kwenye wilaya za Kiteto na Chemba ambapo watu 20 walifariki dunia.
“ Jumla ya watu 20 walipoteza maisha mwaka 2016 kwenye wilaya za Kiteto na Chemba kutokana na kula chakula kilichochafuliwa na sumukuvu,hivyo tunahitaji mkakati wa kufikisha elimu ya udhibiti sumukuvu kwa umma “ alisema Clepin.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Usalama wa Chakula Zanzibar Ndugu Hamad Masoud alisema katika mwaka huu wafanyabiashara wengi toka Zanzibar watafika Bara kwa ajili ya kununua mazao ya chakula hivyo uwepo wa elimu ya sumukuvu ni muhimu katika kuwalinda walaji.