MKAKATI wa madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa wa kumwondoa mstahiki meya wa Halmashauri hiyo Alex Kimbe kupitia chama cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA) umetimia baada ya kura 14 za ndio kati ya kura zote haliali 26 zilizopigwa kutumika kumwondoa meya huyo katika nafasi yake .
Katika kikao hicho maalumu cha baraza la madiwani kilichoitishwa kwa ajili ya kumwondoa meya Kimbe leo ambacho kilifanyika chini ya ulinzi mkali wa polisi na utaratibu wa wajumbe wote wa kikao hicho kuingia kwa barua maalumu ya mwaliko tofauti na vikao vilivyopita ,madiwani wa CHADEMA hawakuweza kuandika chochote katika karatasi ya kupigia kura pamoja na maelekezo ya zoezi hilo kuwataka wapiga kura kupiga kura ya ndio ama hapana.
Mwenyekiti wa kikao hicho Joseph Ryata ambae ni naibu meya wa Halmashauri hiyo akitangaza matokeo ya kura zilizipogwa ambazo upande wa meya Kimbe katika zoezi la wazi la kuhesabu kura hizo aliwakilishwa na mbunge wa jimbo la Iringa mjini Mchungaji Peter Msigwa na upande wa madiwani wa CCM waliokuwa wakimpinga meya huyo kuwakilishwa na diwani Ibrahim Ngwada ,alisema kuwa kura zote 26 zimepigwa na kati ya kura hizo kura 12 ziliharibika na kura 14 ni kura za ndio ambazo zilimtaka meya Kimbe kuondolewa katika nafasi yake .
” Ndugu wajumbe zoezi letu la mchakato wa kupiga kura za kumwondoa meya Alex Kimbe madarakani limekwenda vizuri baada ya wajumbe wote 26 kushiriki kupiga kura za kutokuwa na imani na meya na matokeo kura zilizoharibika ni 12 na kura za hapana hakuna na kura za ndio ni 14 hivyo natangaza rasmi matokeo ya kura zilizopigwa kura waliosema ndio meya aondoke madarakani wajumbe 14 wameshinda hivyo n atangaza rasmi kuwa meya Alex Kimbe kuanzia leo Machi 28 mwaka 2020 sio msitahiki meya tena wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa hadi kufikia hapa kikao kimefungwa ” alisema Ryata huku akifunga mkutano huo na kuondoka .
Akizungumza baada ya kutangawa kuondolewa madarakani aliyekuwa mstahiki meya wa Halmashauri hiyo Alex Kimbe alisema kuwa kuwa kimsingi yeye bado ni meya wa Halmashauri hiyo kwani kikao hicho kimeshindwa kuffikisha wajumbe asilimia mbili ya tatu ya wajumbe wote wote 26 waliopaswa kupiga kura ya ndio hivyo ataendelea kuwa meya hadi hapo taratibu nyingine zitakapofanyika za kumuondoa na zitakazofikisha therufi mbili ya kura za ndio .
” Wameshindwa kunitoa katika nafasi yangu kwa sababu wameshindwa kufikisha mbili ya tayu ya wajumbe wote kama ambavyo kanuni inasema nilichokiona na kumsamehe bure mwenyekiti wa kikao hicho naibu meya Ryata ulimi wake umeteleza badala ya kutangaza mimi bado nitaendelea kuwa meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa yeye ametangaza kuwa mimi sio meya kwani kimsingi therufi mbili wajumbe wote katika Halmashauri hiyo ni 17 na hao walipaswa kuthibitisha mchakato huo kuendelea na leo therufi mbili imezidi maana tulikuwa madiwani 26 lakini ili meya ama mwenyekiti wa Halmashaurti aweze kuondoka madarakani kanuni ipo wazi kuwa wajumbe mbili ya tatu ndio wanapaswaw kumwondoa meya madarakani na waliopiga kura za kuniondoa wapo 14 kumbe ilipaswa wawe 17 hivyo mimi bado meya “
Aidha alisema kuwa katika kikao hicho wakati ikisomwa taarifa ya matokeo ya uchunguzi wa tuhuma dhidi yake alinyimwa haki ya kujieleza mbele ya wajumbe baada ya tuhuma hizo kutolewa jambo ambalo yeye amelitafsiri kama limefanyika kwa maelekezo maalumu kutoka kwa viongozi wa juu wa serikali ya mkoa wa Iringa .
Kwani alisema kuwa kanuni za Halmashauri hiyo zipo wazi kuwa mkutano wa kumwondoa madarakani mwenyekiti anayetuhumiwa utaongozwa na makamu mwenyekiti isipo kuwa mtuhumiwa atapata nafasi ya kujitetea mbele ya wajumbe baada ya tuhuma dhidi yake kutolewa ila imekuwa kinyume baada ya tuhuma kusomwa hakupewa nafasi ya kujitetea zaidi ya kuelekea zoezi la kupiga kura .
Huku kwa upande wake mbunge wa Iringa mjini Mchungaji Peter Msigwa alisema kuwa mbinu ambayo waliitumia jana kupiga kura ni mbinu kabambe ya kubaini wasaliti ndani ya CHADEMA baada ya kupata taarifa za ndani kutoka CCM kuwa kuna mbinu ya kuwanunua madiwani watatu ama zaidi ili wapige kura za ndio za kumwondoa meya madarakani na ndipo walipoamua kuja na mpango wa wajumbe 12 wa CHADEMA kupokea karatasi ya kupigia kura ya kuiweka kwenye sanduku la kura bila kuandika chochote na zoezi hilo kufanyika pasipo kificho kwa kila anayepewa karatasi kulinyanyua juu bila kuandika na kisha kutumbukiza kwenye sanduku .
” Tulitaka kura zetu 12 kuwa salama bila kununuliwa lakini wakati huo huo sio kwamba hizo kura kura 12 hazijapigwa zimepigwa hivyo kura zilizopigwa ndani ya ukumbi ni kura 26 na zilizomtaka meya aondoke ni kura zao CCM 14 na 12 ni kura zilizoharibika na kanuni ipo wazi inamtaka meya kuondoka kwa therufi mbili ya kura zilizopigwa si vinginevyo walihitaji kura nyingine tatu ambazo hawajazipata katika mchakato wao huo wa kumuondoa meya hivyo kitendo cha kumtoa meya kuwa wamemtoa meya ni kichekesho maana wamekosa kura tatu ” alisema Mchungaji Msigwa .
Mbunge Msigwa alisema kuwa wao wanatambua kuwa zoezi la kumtoa meya limekwama baada ya kura 3 kukosekana na hivyo meya bado halali katika nafasi yake na ataendelea kufanya kazi yake kama kawaida na wao kama CHADEMA hawatafanya fujo yoyote na wanataka madiwani wa CCM kufuata taratibu ili kulinda demokrasia nchini .
Alisema anashangazwa na nguvu kubwa inayotumiwa na serikali ya CCM ya kumtoa meya Kimbe wakati kimsingi muda uliobaki ni mdogo sana na ni vikao viwili pekee ndivyo vimesalia ili kuvunjwa kwa baraza la madiwani kabla ya kuingia katika zoezi la uchaguzi mwingine .
Kwa upande wake diwani wa CCM Nguvu Chengula na Ibrahim Ngwada alisema kuwa Chadema walikuwa wametengeneza mbinu ya kutopiga kura ila mbinu hiyo imekwama baada ya zoezi hilo kufanyika kwa mafanikio kwa CCM maana kura zimeweza kuamua kumuondoa meya huyo madarakani .
Alisema kuwa kitendo cha madiwani kutopiga kabisa kura kimetoa nafasi ya meya kuondolewa madarakani kwani walipaswa kupiga kura za hapana na sio kutopiga kura kabisa na hivyo kuwataka madiwani hao 12 watambue kuwa wameungana na CCM kumwondoa meya wao .
Ngwada alisema kuwa kukataliwa kwa meya huyo ni dalili mbaya kwa mbunge Msigwa kuondoka katika uchaguzi mkuu ujao kwani kitendo cha Meya kuondolewa na ishara ya mbunge kutotakiwa katika jimbo la Iringa mjini na kuwa tuhuma zilizotolewa ambao ameshindwa kuzijibu zinaonesha wazi ni jinsi gani ambavyo meya huyo alitumia vibaya nafasi yake kwa kujinufaisha mwenyewe na madiwani wenzake wa Chadema na hivyo kuitaka taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) kumchunguza meya Kimbe kwa ubadhilifu wa fedha za Halmashauri ambao umebainika katika ripoti ya kiuchunguzi dhidi yake .
Mwanasheria wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Nicholaus Mwwakasungura alisema kuwa kitendo ambacho wamekifanyha chadema cha kutopiga kura ya hapana ama ya ndio ndiko kumetengeneza mazingira ya kuonesha kura za hapana zimeshinda katika mchakato huo wa kumuondoa meya madarakani .
Hivyo alisema kuwa azmio la madiwani lililotolewa kwa njia ya kura kwenye kikao hicho maalumu ni sahihi hivyo uamuzi wa kura 14 za ndio zilizomtaka aondoke madarakani ndio unaopaswa kuheshimika na kutekelezwa kwa mujibu wa kanuni za baraza la madiwani la Halmashauri hiyo .
” Kutokana na kura zilizotangazwa na naibu meya ambae alikuwa akiongoza kikao hicho Joseph Ryata kwa kutangaza matokeo ya kura 14 zilizoshinda na kura 12 zilizo haribika hivyo kura za ndio za madiwani wa CCM zimeshinda katika zoezi la kumng’oa meya Alex Kimbe madarakani na kwa matokeo hayo ni wazi kuanzia leo Machi 28 Meya Kimbe ameondolewa madarakani na sio meya tena wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa na anapaswa kukabidhi ofisi ” alisema mwanasheria huyo wa Manispaa ya Iringa Mwakasungura .
Awali kabla ya kufanyika kwa zoezi la kupiga kura za kumwondoa meya Kimbe mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Himid Njovu aliwasilisha ripoti ya uchunguzi wa tuhuma dhidi ya meya na kuwa uchunguzi uliofanywa ulibaini kuwa tuhuma zote zilizotolewa tuhuma zaidi ya tatu zina ukweli na meya alipoitwa kutakiwa kujibu tuhuma hizo aligoma kutoa maelezo kwa madai jambo hilo halikufuata utaratibu .
Alisema kuwa timu ya uchunguzi imebaini kuwa mstahiki meya Alex Kimbe anamiliki mali nyingi ambazo zipo katika maeneo mbali mbali ya mkoa wa Iringa na nje ya mkoa na baadhi ya mali hizo ni shamba kubwa lenye ukubwa wa ekari 30 lililopo katika mataa wa CHautinde kata ya Isakalilo ,Shamba kubwa lenye ekari 35 lililopo Pawaga ambalo analitumia katika kilimo cha Mpunga ,Shamba kubwa ekari 9 lililopo Pawaga ambalo pia analima mpunga , Shamba ekari 6 mtaa wa Kitasengwa kata yake ya Isakalilo na mashamba mengine yaliyopo Kilolo na nje ya mkoa wa Iringa pia ana nyumba tatu ,gari aina ya Nadia ambavyo vyote hivyo alipata kati ya mwaka 2015 na 202o kipindi akiwa Meya
” Imebainika kuwa meya Kimbe anamiliki mali ambazo haziendani na kipato chake kwani kipato chake kwa mwaka ni wastani wa shilingi milioni 15 fedha inayohusisha na posho za vikao ,posho ya madaraka,takrimu pamoja na posho za vikao na shughuli za kilimo ,fuka la vipuri na biashara ya wakala wa VODA ni vyanzo hafifu vya mapato ya meya huyo kuweza kumiliki mali hizo .
Pia alisema eneo jingine ni la Chautinde lenye ukubwa wa zaidi ya ekari 25 maeneo hayo yapo ndani ya kata anayoiongoza ya Isakalilo kuwa Manispaa ya Iringa iliweka mpango wa uendeshaji wa skimu ya umwagiliaji kuelekea eneo hilo ila meya huyo alinunua eneo la Mtwivila (mkoga ) eneo hilo lipo jirani na eneo linalomilikiwa na Fredrick Luvinga ambae ni rafiki wa meya kimsingi maeneo yote mawili yapo kwenye mpango wa uendelezaji wa skimu kwa ajili ya wananchi hivyo kujimilikisha ni kuwanyima fursa wananchi .
Aidha alisema Kimbe analo eneo jingine ambalo lipo katika eneo ambalo Halmashauri inakusudia kulitoa kwa ajili ya wizara ya afya ili liweze kujengwa Hospitali ya mafunzo kwa vitendo kuwa timu ya uchunguzi ilijiridhisha kuwa maeneo yote mawili yanamiliki kihalali na meya Kimbe ameyapata akiwa katika nafasi yake .
” Timu ya uchunguzi imebaini kuwa Kimbe ana urafiki wa karibu na Frederick Luvinga urafiki wao ni wa muda hata kabla ya kuwa meya na wawili hao ni wakazi wa mtaa wa Kihondombi A kata ya Isakalilo inayoongozwa na meya huyo na timu ya uchunguzi imejiridhisha pasipo shaka kuwa jengo la abiria katika stendi ya Igumbilo nilalo jengwa na Luvinga wa kampuni ya yake ya ukandarasi ya Mwakalu Company Ltd na kimsingi jengo lilipaswa kujengwa na Local Fund na siyo kampuni ”
Kuwa jengo hilo Luvinga na kampuni yake anatekeleza kazi nyingine ya ujenzi wwa sekondari ya kata ya Isakalilo inayojengwa katika eneo la Kitasengwa kazi hiyo anaitekeleza kwa utaratibu wa Force Account kwwa gharama ya shilingi 33,210,000 ambapo anajenga madarasa sita kwa shilingi 33,210,000 na vyoo vya matundu 16.
Kuwa zabuni ya kazi hiyo ilitangazwa na baadae kamati ya ujenzi ya kata ya Isakalilo ilipitisha maombi tarehe 4/11 mwaka 2019 kumteua Luvinga kufanya kazi hiyo wakati kwa mujibu wa kifungu cha 60 (4) cha sheria ya ununuzi katika sekta ya umma ,mkataba wowote kabla haujasainiwa unatakiwa kupata kibali cha kamati ya fedha na uongozi ambayo mwenyekiti wake Mstahiki meya pia hata jengo la abiria Igumbilo meya aliidhinisha mkakaba kuwa Luvinga afanye kazi hiyo .
Kuhusu tuhuma za rushwa ya ngono zinazomkabili meya huyo alisema timu ya uchunguzi imebaini kuwa meya amekuwa akimlazimisha mapenzi Nancy Nyalusi kwa kutumia madaraka yake ya umeya kinyume na kanuni namba 9(3) ya maadili (mamlaka za miji ) ya mwaka 2000 na kuwa alifanya hivyo ili kumsaidia kupata kazi ya ukusanyaji mapato Katika halmashauri hiyo .
katika maoni ya matatu ya kamati ya uchunguzi ilipendekeza mstahiki meya Kimbe kuwa anatakiwa wakati wote anapotekeleza majukumu yake kuzingatia sheria ,kanuni na taratibu na kuwa na kiwwango cha juu kabisa cha uadilifu kama inavyosisitizwa kwenye kanuni ya 8(a) (b0 na kanuni ya 9 ya kanuni ya maadili ya madiwani (mamlaka za miji ) za mwaka 2000.
Pia kutokana na kuthibitika kuwa tuhuma nyingi zinazomkabili mstahiki meya huyo ,timu ya uchunguzi inapendekeza kuwa Halmashauri iendelee na mchakato kama inavyoelekezwa kwenye kanuni namba 5 (7) ya kanuni za kudumu za Halmashauri na maoni ya mwisho ni kutaka TAKUKURU kuchunguza kwa kina mwenendo wa mstahiki meya Alex Kimbe hususani mali zake na namna alivyozipata ili kubaini na iwwapo mali hizo ni halali au la hatua stahiki zichukuliwe dhidi yake .
MWISHO