Visa vya maambukizi ya ugonjwa wa Corona vimetajwa kuongezeka nchini Kenya na Uganda .
imethibitisha visa saba zaidi vya maambukizi ya ugonjwa wa coronavirus, huku Uganda ikiandikisha visa vingine vitano vya ugonjwa huo hatari.
Akizungumza katika kikao na wanahabari siku ya Jumamosi, waziri wa Afya nchini Kenya Mutahi Kagwe amesema kwamba idadi hiyo inaongeza visa vya maambukizi nchini Kenya kufikia 38, huku mtu mmoja akiripotiwa kufariki naye mwengine akipona maambukizi hayo.
Kagwe amesema kwamba kufikia sasa mji mkuu wa Nairobi unaongoza kwa maambukizi ya visa 28.
- Jinsi coronavirus inavyoisaidia filamu ya zamani kutazamwa sasa
- Je, virusi vya Corona vimewatengenisha watu na imani zao?
- Je joto kali linaweza kuuwa coronavirus?
Amesema kwamba kati ya visa hivyo saba kuna Wakenya wanne raia wawili wa DR Congo na raia mmoja wa China.
Ameongezea kwamba idadi hiyo ni miongoni mwa watu 81 ambao walifanyiwa vipimo katika maabara tofauti nchini katika kipindi cha saa 24.
‘Walioambukizwa wana historia ya kusafiri’
Amesema wanne kati ya visa hivyo ni watu wenye historia ya kusafiri katika mataifa yenye idadi kubwa ya maambukizi huku mmoja akiripotiwa kusafiri hadi Mombasa nao wengine wawili wakiambukizwa na visa vya awali.
Vilevile waziri huyo alikuwa na habari njema pale aliposema kwamba wagonjwa wawili waliokuwa wakiugua virusi hivyo wamepona.
”Mgonjwa wetu wa kwanza na watatu wamepona virusi hivyo , watafanyiwa vipimo vingine katika kipindi cha saa 48 , tuna matumaini kwamba vipimo hivyo vya pili vitabaini kwamba wamepona kabisa ili kuruhusiwa kutoka katika vituo vyetu vya tiba”, alisema.
Nairobi inaongoza kwa maambukizi
Amesema kwamba visa vyote saba vinatoka katika kaunti ya Nairobi ikiwa ndio inayoongoza , ikifuatiwa na kilifi visa 6, Mombasa visa 2 huku kajiado na Kwale zikiwa na kisa kimoja kila moja.
Aidha waziri huyo amesisitiza umuhimu wa kujitenga akisema mwanawe na mpwa wake wametengwa ili kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huo.
”Mimi mwenyewe nina mwanangu ambaye amewekwa karantini . Pia nina mpwa wangu ambaye amewekwa karantini . Tunachosisitiza ni kwamba wakati mtu anapowekwa katika karantini anajilinda yeye na maisha ya wengine”, alisema Kagwe bila kutoa maelezo zaidi.
Nchini Uganda
Wakati huohuo Idadi ya watu waliopata maambukizi ya virusi vya corona nchini Uganda imeongezeka na kufikia 23 kutoka 18 baada ya watu wengine watano kukutwa na maambukizi siku ya Ijumaa.
Kati ya sampuli 227 zilizofanyiwa vipimo siku ya Ijumaa watu 222 hawakupatikana na virusi vya corona huku watu watano wakipatikana na ugonjwa huo, alisema Dkt. Jane Ruth Aceng katika chapisho lake la mutandao wa twitter.
”Waganda tafadhalini fuateni maelezo na mikakati ya kuzuia kusambaa kwa virusi hivi. Tunaweza kuzuia maambukizi ya virusi hivi pamoja”, alisema afisa huyo.
Hatahivyo Aceng hakutoa maelezo ya watu walioambukizwa.
Rais Museveni alisema kwamba kutokana na visa hivyo vipya huenda kukawa na umhimu wa kuchukua hatua kali zaidi ili kuzuia maambukizi kulingana na ujumbe wa twitter uliotumwa na katibu wake wa maswala ya habari bwana Don Wanyama .
Maafisa wa afya wanasema kwamba watu wote 14 waliothibitishwa hapo awali kuwa na virusi hivyo wanaendleea vyema katika hospitali ya Entebbe Grade B , Hospitali ya Mulago na hospitali kuu ya Adjumani.