Serikali kupitia upya mipaka ya hifadhi za taifa na mapori tengefu

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na hatua ambayo wizara inataka kuichukua kupima upya mipaka ya hifadhi za taifa na mapori tengefu kutokana na kuwepo kwa taarifa za baadhi ya vijiji kuvamia maeneo ya hifadhi na kuendesha shughuli za kijamii

Daniel Pius Kaimu Mkuu wa Kanda akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za kanda zilizopo njiro Jijini Arusha
Askari wa kikosi cha kulinda wanyamapori kanda ya kaskazini wakimsikiliza Naibu Waziri Constantine Kanyasu(hayuko pichani)

Na Seif Mangwangi, Arusha
SERIKALI imesema iko kwenye
mikakati ya kupitia na kuhakiki upya mipaka ya hifadhi za Taifa na mapori
tengefu inayopakana na vijiji ili kumaliza migogoro ya mara kwa mara ambayo
imekuwa ikiendelea kutokea baina ya vijiji na hifadhi.
Naibu Waziri wa Maliasili na
Utalii Constantine Kanyasu amesema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa
habari mara baada ya kumaliza kikao kazi na wafanyakazi wa Mamlaka ya usimamizi
wanyamapori kanda ya kaskazini (TAWA) katika ofisi zao zilizopo njiro jijini
Arusha.
Kanyasu amesema Wizara ya
Maliasili na Utalii imekuwa ikilipa fidia kubwa kwa wakazi wanaoishi karibu na
hifadhi za Taifa kutokana na kudhuriwa na wanyamapori lakini kuna taarifa kuwa wananchi
katika baadhi ya vijiji ambavyo vimekuwa vikiathirika wamekuwa wakiishi katika
maeneo hayo kinyume cha sheria baada ya kuyavamia.
Amesema taarifa zilizopo ni
kwamba baadhi ya mapori tengefu yamekuwa yakimegwa na vijiji vinavyozunguka na
kuzuia mapito ya wanyamapori ambayo wamekuwa wakiyatumia kama njia lakini pia
kuzaliana kwa baadhi ya wanyama.
Hata hivyo ameagiza viongozi wa
TAWA kuhakikisha kwenye maeneo ambayo kumekuwepo na migogoro mingi ya wananchi
kudhuriwa na wanyamapori kuweka kambi za kudumu ili askari wanyamapori waweze
kupatikana saa zote pindi madhara yanapotokea.
“Nimeagiza  mamlaka ya TAWA iweke kambi za kudumu kwenye
maeneo ambayo wananchi wamekuwa wakidhuriwa mara kwa mara na wanyamapori, hii
itasaidia kupunguza vifo vya wananchi lakini pia wanyama kuvamia
vijiji,”amesema.
Kwa upande wake Daniel Pius Kaimu
Mkuu wa Kanda, Mamlaka ya Wanyamapori (TAWA), amesema suala la ujangili
limepungua kwa kasi kubwa katika ukanda wa Kaskazini lakini wamekuwa na
changamoto kubwa ya uvamizi katika mapori tengefu kwa wananchi kuyatumia kwaajili
ya kilimo.