Watuhumiwa kesi ya uhujumu uchumi waomba kurejeshewa kadi zao za benki

Mkurugenzi
wa Uthamini wa madini ya almasi na vito wa serikali, Archad Kalugendo
na Edward Rweyemamu, wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi
wamewasilisha maombi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakiomba
kurejeshewa kadi zao za benki.

Wakili
wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, jana amekiri mbele ya Hakimu
Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kupokea nakala ya maombi hayo.

Wankyo alidai upande wa Jamhuri unaomba siku 14 kwa ajili ya kujibu maombi ya utetezi.

Upande wa utetezi haukuwa na pingamizi kuhusu ombi la Jamhuri kupewa siku 14.

Awali
upande wa Jamhuri ulidai kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa
na kwamba upelelezi wake bado haujakamilika, lakini wamewaelekeza
wapelelezi wafanikishe maeneo machahe yaliyobaki.

Hakimu
Shaidi alisema, maombi hayo yatatajwa Machi 6, na kesi ya msingi
itatajwa Machi 20, mwaka huu, washtakiwa wataendelea kukaa mahabusu.

Katika
kesi ya msingi, washtakiwa wanakabiliwa na kesi ya kuisababishia
serikali hasara ya Sh. 2,486,397,982.54 kati ya Agosti 25 na 31, 2017
katika maeneo mbalimbali ya mikoa ya Dar es Salaam na Shinyanga.