Wizara ya maji yatenga shilingi bilioni 10.8 kumaliza kero ya maji isimani na kilolo..

Mkuu wa mkoa wa Iringa Ally Hapi na viongozi mbali mbali wakikagua mradi wa maji wa Kilolo -Isimani Jana 
………………

Wizara ya maji yatenga  kiasi cha shilingi bilioni 10.8 kwa ajili ya  kujenga mradi mkubwa wa maji utakaomaliza kero ya maji vijiji 29 vya Kilolo  -Isimani .

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo leo kwa mkuu wa mkoa wa Iringa wakati wa ziara ya Iringa mpya awamu ya pili msimamizi wa mradi huo wa maji Robina katundu alisema tayari serikali kupitia wizara ya maji imekwisha tuma pesa kiasi cha shilingi milioni 185 kwa ajili ya kuanza mradi huo .

Kati ya fedha hizo walizoingiziwa tayari kiasi cha shilingi milioni 45 zimekwisha tumika katika shughuli mbali mbali za utekelezaji wa mradi huo ikiwemo ya ufyatuaji wa tofali za kujengea tanki la maji .

Alisema kuwa wizara ya maji  imeendelea kutekeleza mbali mbali ya maji ndani ya mkoa wa Iringa na kuwa mradi huo wa Kilolo -Isimani utawahudumia wananchi zaidi  46,380 wa wilaya ya Kilolo na Iringa .

Alisema kuwa utekelezaji wa mradi huo unajengwa na timu tatu  kwa kutumia wataalam wa ndani ikiwemo timu ya  Mamlaka ya maji Makambako (MKUWASA) ,mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira mjini Iringa (IRUWASA) na wakala wa huduma za maji vijijini (RUWASA) huku mkurugenzi wa IRUWASA ndie msimamizi mkuu wa mradi huo .

Aidha alisema mradi huo utatekelezwa kwa awamu tatu awamu ya kwanza ni ujenzi wa matanki ya maji na awamu ya pili ni ukatabati wa matanki ,ujenzi wa vitu vya kuchotea maji na nyingine wakati awamu ya tatu kazi zitakazofanyika ni ukabarati wa mtambo wa katibu maji Mbigili pamojana kujenga mtambo mpya mwingine wa katibu maji .

Katundu alisema utekelezaji wa mradi huo umeanza Disemba mwaka jana unatarajiwa kukamilika mwezi Juni mwakani .

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Iringa Ally Hapi mbali ya kupongeza kazi zinazoendelea katika utekelezaji wa mradi huo bado alitaka kasi ya ujenzi iongezwe zaidi na iendane na ufanisi .

“Mimi ningetamani sana mradi huu ukamilike kabla ya muda uliopangwa kama ingekuwa ni amri yangu maana ni mradi unaoendana na utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ambayo inamalizika mwaka huu lakini siwezi kuwaharakisha kulingana na taratibu zenu za kazi “alisema Hapi

Aliwataka wataalam wanaosimamia mradi huo kufanya kazi kwa uzalendo zaidi maana  mradi huo haujengwi na mkandarasi hivyo wasimamizi hao wanatakiwa kusimamia wenyewe vizuri zaidi .

Alisema kuwa hakuna sababu ya kisingizio cha mkandarasi kutolipwa ana vifaa kutofika maana kila kitu wanacho na wao wanalipwa mahahara na serikali .

Hapi alisema lengo la serikali kutoa fedha za ujenzi wa miradi ya maji ni kutatua kero ya maji na kumtua ndoo ya maji mama kichwani .

Pia aliagiza mchakato wa kuzifanyia kazi jumuiya za watumiaji maji vijijini kuboreshwa ili jumuiya hizo kwani zimekuwa ni kero kubwa kwa wananchi .

Alisema kuwa  sehemu nyingi jumuiya za watumiaji maji zimekuwa ni kikwazo na hivyo lazima kuangalia uwezekano wa kuboresha jumuiya hizo na kuangalia uwezekano wa kuondokana na utaratibu wa kuchota maji kwenye vizimba na badala yake wananchi kuingiziwa maji katika nyumba zao.

Akikagua  mradi wa maji Ruahambuyuni mkuu huyo wa mkoa alitaka wananchi kutoa ushirikiano kwa miradi ya maji na kuepuka  kuweka vikwazo vya kutaka fidia katika miradi ya maji .

Pia alionya wananchi wenye tabia ya kuhujumu miradi ya maji kwa kukata mabomba ya maji .

Kwani alisema serikali ya awamu ya tano imeendelea kuboresha sekta mbali mbali ikiwemo ya maji ,afya na elimu hivyo lazima wananchi kulinda miradi hiyo na wale wanaopewa majukumu ya kujenga miradi kujenga kwa ufanisi zaidi