Ttcl, tpri kuzindua huduma ya kuhakiki viuatilifu kielektroniki

Kaimu
Mkurugenzi wa Shirika la Mawasiliano TTCL, Kezia Katamboi (kulia),
akibadilishana mkataba na Kaimu Mkurugeni Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa
Viuatilifu vya Kudhibiti Visumbufu katika Ukanda wa Kitropiki (TPRI),
Dk. Margaret Mollel baada ya kusaini mkataba kwa ajili ya maandalizi ya
kutoa huduma ya T- Hakiki ambayo ni maalumu kwa wakulima na wafugaji
kuhakiki kwa njia ya simu viuatilifu vilivyosajiliwa.

Kaimu
Mkurugenzi wa Shirika la Mawasiliano TTCL, Kezia Katamboi (kulia), na
Kaimu Mkurugeni Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu vya Kudhibiti
Visumbufu katika Ukanda wa Kitropiki (TPRI), Dk. Margaret Mollel
wakionesha mikataba walioisaini kwa ajili ya maandalizi ya kutoa huduma
ya T- Hakiki ambayo ni maalumu kwa wakulima na wafugaji kuhakiki kwa
njia ya simu viuatilifu vilivyosajiliwa.
Kaimu
Mkurugenzi wa Shirika la Mawasiliano TTCL, Kezia Katamboi (kulia),
Kaimu Mkurugeni Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu vya Kudhibiti
Visumbufu katika Ukanda wa Kitropiki (TPRI), Dk. Margaret Mollel
(kushoto) na 
Mkurugenzi wa Biashara Quincewood, Fatma Fernandes (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kusaini mikataba ya kwa
ajili ya maandalizi ya kutoa huduma ya T- Hakiki ambayo ni maalumu kwa
wakulima na wafugaji kuhakiki kwa njia ya simu viuatilifu
vilivyosajiliwa.
NA MWANDISHI WETU

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL Corporation), na Taasisi ya
Utafiti wa Viuatilifu Ukanda wa Tropiki (TPRI) zimeingia makubaliano ya
maandalizi ya uzinduzi wa mfumo wa kuhakiki viuatilifu kwa kutumia
teknolojia ya kielektroniki.
Mfumo huo uliopewa jina la ‘T–Hakiki’ ni huduma ya simu ya mkononi
ambayo itamuwezesha mkulima kupata taarifa ya kiuatilifu kilichosajiliwa
na kwa matumizi sahihi ili kuleta tija katika kilimo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana katika
hafla ya kusaini mkataba wa makubaliano, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TTCL
Corporation, Kezia Katamboi alisema baada ya makubaliano hayo, utoaji wa
huduma hiyo unatarajiwa kuanza mwezi ujao ikiwa ni baada ya kukamilisha
baadhi ya taratibu zinazotakiwa.
Alisema makubaliano hayo ni muhimu kwa maendeleo ya sekta ya kilimo, ufugaji na viwanda.
Alisema hii ni hatua kubwa katika kulinda bidhaa za kilimo na ufugaji
kwani itahakikisha wakulima na wafugaji wanapata mavuno yanayostahili.
“Kwa kupitia mfumo huu ambao utatumia mawasiliano ya TTCL Corporation
utakuwa suluhisho ya kuondoa viuatilifu feki sokoni na kuongeza kasi ya
matumizi ya viuatilifu sahihi vya kilimo na ufugaji kwa kuwa mtandao wa
TTCL Corporation umeenea nchi nzima hivyo wakulima wote nchi nzima
watanufaika na mradi huu. 
“Zaidi ya yote huduma hii itapatikana bure kwa wakulima na wafugaji wote
nchini. Kupata huduma hii, mkulima au mfugaji kupitia kwenye simu yake
ya Mkononi, atabofya *148*52# kisha atafuata maelekezo,” alisema. 
Aidha, Mkurugenzi wa Biashara Quincewood ambayo inasimamia mfumo huo wa
kuhakiki viuatilifu kwa kutumia teknolojia ya kielektroniki, Fatma
Fernandes alisema sekta ya kilimo ni muhimili wa maendeleo ya uchumi. 
“Sekta hii inachangia kiasi cha nusu ya pato la Taifa, robo tatu ya
bidhaa zinazouzwa nje ya Nchi na chanzo cha chakula pamoja na utoaji wa
fursa za ajira zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania. 
“Kilimo kina uhusiano na sekta zisizo kuwa za kilimo kupitia uhusiano wa
usafishaji kwenda kwenye usindikaji wa mazao ya kilimo, matumizi ya
ndani, uuzaji nje ya Nchi na uzalishaji wa malighafi kwa ajili ya
viwanda vyetu.
Wakati Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti na Udhibiti wa Viuatilifu
katika Ukanda wa Kitropikia, Dk. Margaret Mollel alifafanua kuwa huduma
hiyo ya “T-Hakiki” itamuwezesha mkulima kupata taarifa kuhusu
viuatilifu vilivyosajiliwa na vyenye ubora unaotakiwa kwa kutumia hapo
alipo kwenye sehemu yake ya kilimo.
“Pia itamwezesha kujua matumizi sahihi ya viuatilifu kulingana na
visumbufu lengwa kwa kuwasiliana na mamlaka ya TPRI pamoja na wamiliki
wa viuatilifu na kutoa taarifa sahihi kwa TPRI kuhusu viuatilifu ambavyo
havina ubora kwa ajili ya ufuatiliaji na kuchukua hatua,” alisema.
Ubunifu wa huduma hiyo pia utaisaidia TPRI kutapa taarifa na ufuatiliaji
wa urahisi wa viuatilifu wakati vikiwa sokoni pamoja na taarifa kutoka
kwa mkulima yaani mtumiaji wa mwisho.
“Pia TPRI kama mdhibiti wa viuatilifu, T-Hakiki itafanya ufuatiliaji
moja kwa moja bila hata kumshirikisha mtengenezaji au muingizaji wa
kiuatilifu baada ya kupata taarifa kutoka kwa mkulima moja kwa moja juu
kiualitifu husika endapo kitakuwa hakifanyi kazi iliyokusudiwa.