Hukumu ya kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi chadema kutolewa machi 10, 2020

Mahakama
Ya Hakimu Mkazi Kisutu imepanga Machi 10, mwaka huu kutoa hukumu ya
kesi ya uchochezi dhudi ya viongozi nane wa Chadema akiwemo  Mwenyekiti
wake, Freeman Mbowe pamoja na aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama
hicho,Dk.Vicent Mashinji ambaye hivi karibuni  amehamia CCM. 


 Hakimu
Mkazi Mkuu Thomas Simba amesema sheria inaelekeza pande zote kufanya
majumuisho ili kuisaidia mahakama kutoa uamuzi kwa kuangalia masuala ya
kisheria yaliyoibuliwa wakati wa usikilizaji wa kesi hiyo na wametoa
maelekezo kwa pande hizo kuwasilisha hoja zao katika siku tano za kazi
baada ya mahakama kukamilisha uchapaji wa nyaraka zilizopo kwenye kesi
hiyo na kuwapatia.

Amesema, anatambua kesi hiyo inamvuto kwa jamii, hivyo ni lazima iishe
ili kila mmoja aweze kuendelea na shughuli zake na kuongeza  “Majumuisho
ya mwisho mnatakiwa muyawasilishe siku tano za kazi,” amesema Hakimu
Simba. 


Ameongeza
kesi hiyo inakurasa zaidi ya 1,000 ambazo anatakiwa kuzipitia na kutoa
hukumu hivyo hukumu ya kesi hiyo itatolewa Machi 10, mwaka huu saa 4:30
asubuhi. 


Washitakiwa
wengine katika kesi hiyo ni Naibu Katibu mkuu wa Chadema upande wa
Zanzibar, Salum Mwalimu,  Katibu Mkuu Chadema na Mbunge wa Kibamba, John
Mnyika, Mbunge wa Iringa mjini, Peter Msigwa, Mbunge wa Tarime Mjini,
Ester Matiko, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya
na Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche.

Jumla ya mashahidi nane wa upande wa mashtaka walifika mahakamani hapo
kutoa ushahidi wao ambapo mahakama iliwaona washitakiwa wote kuwa na
kesi ya kujibu na walijitetea kwa kuleta mashahidi kumi na tatu. 
Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka 13 likiwemo la kula njama,
ambapo wote wanadaiwa kuwa, Februari Mosi na 16, mwaka jana, Dar es
Salaam walikuĺa njama ya kutenda kosa la kufanya mkusanyiko usio halali
na kukiuka tamko kutawanyika.