Fao yasema tusipowadhibiti nzige wanaoikabilia ethiopia, kenya na somalia watasambaa

Shirika
la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO limeonya kwamba nzige
walioivamia Ethiopia, Kenya na Somalia sasa ni wimbi kubwa kuwahi
kushuhudiwa hivi karibuni na lisipodhibitiwa kuna uwezekano wa kusambaa
katika nchi nyingine za Afrika Mashariki.


Wimbi
kubwa la nzige walionekana kutamalaki angani na kughubika mashamba
pembe ya Afrika, kwa mujibu wa FAO tayari limeshasababisha uharibifu
mkubwa kwa kusambaratisha maelfu ya ekari za mazao hali ambayo inaathiri
uhakika wa chakula katika nchi hizo ambazo zinakabiliwa na changamoto
nyingine nyingi ikiwemo kutokuwa na uhakika wa chakula katika baadhi ya
maeneo.

Rosanne
Marchesich kiongozi wa timu ya dharura na mnepo ya FAO anasema mlipuko
wa safari hii wa nzige ni mkubwa sana, “Tunachojua kuhusu uvamizi huu wa
nzige wa jangwani ni kwamba ni mbaya zaidi kuwahi kushuhudia Ethiopia
na Somalia katika kipindi cha miaka 25 na ni mbaya zaidi kushudiwa Kenya
kwa zaidi ya miaka 70.”

Hata
hivyo amesema kiwango cha nzige hao kinatofautiana kutoka nchi moja
hadi nyingine lakini kwa sasa nchi zilizoathirika zaidi ni Ethiopia ,
Kenya na Somalia na nzige wameshasababisha athari kubwa , na hofu ni
kwamba wanavyoendelea kuvamia sehemu zingine za nchi hizo athari hasa
katika uhakika wa chakula zitakuwa kubwa zaidi, lakini pia katika
kilimo, na maisha kwa wakulima na wafugaji.

FAO
imetoa wito wa kuwa na kampeni ya pamoja kukabiliana na janga hilo la
nzige ikihofia kwamba janga linaweza kusambaa kwa nchi zingine za Afrika
Mashariki.

“Kuna
hatari ya kusambaa, nchi muhimu zaidi zinazoangaliwa hivi sasa ni
Uganda na Sudan Kusini. Uganda haijawahi kukabiliana na wimbi la nzige
tangu miaka ya 60, hivyo kuna wasiwasi kuhusu uwezo wa wataalam
mashinani kuweza kukabiliana na janga hilo bila msaada toka nje. Na
katika nchi kama Sudan Kusini tayari kuna asilimia 47 ya watu wasio na
uhakika wa chakula.”


Ameongeza kuwa mbali ya zahma zingine zinazowakabili mabadiliko ya tabianchi yamekuwa kichocheo kikubwa cha nzige kuzaliana.

Pamoja
na kufuatilia janga hili kwa karibu FAO inatoa msaada wa hatua za
kuwadhibiti nzige hao kwa njia ya anga na ardhini lakini pia mbinu za
kuweza kuwasaidia wakulima na wafugaji kuendesha maisha yao.

Pia imeonya kwamba mazingira ya kuruhusu kuzaliana bado yapo na ongezeko la nzige linaweza kuendelea hadi Juni mwaka huu 2020.

Umoja wa Mataifa waingilia kati
Ofisi
ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya kibinadamu na msaada wa dharura OCHA
imesema imetoa dola milioni 10 kutoka katika mfuko wake mkuu wa dharura
CERF ili kuongeza nguvu katika kupambana na mlipuko wa nzige wa Jangwani
ambao wamevamia maeneo kadhaa ya Afrika Mashariki. 

Akizungumza 
na vyombo vya habari mjini Geneva Uswisi, Msemaji wa OCHA Jens Laerk
amesema,“Ni mlipuko ambao uko Afrika Mashariki na pembe ya Afrika. Pia
umebainika kusini magharibi mwa Asia na Bahari ya shamu, ni mlipuko
mbaya wa aina yake katika miaka 25 kwa Ethiopia na Somalia na ni mbaya
zaidi kwa Kenya kuwahi kuuona katika miaka 70. Madhara katika nchi hizo
ni mabaya kwa kuwa malisho na mazao yanatoweka katika jamii ambazo
tayari zilikuwa zinakabiliwa na upungufu wa chakula.”

Credit: Umoja wa Mataifa