Waziri mpina aunda timu uchunguzi ukwepaji wa kodi kampuni ya ufugaji samaki

NA MWANDISHI WETU, MAFIA

WAZIRI
wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ameunda timu ya wataalamu kufanya
uhakiki wa takwimu, mauzo, uzalishaji na uendeshaji wa Kampuni ya
Alphakrust inayojishughulisha na uzalishaji wa samaki aina ya Kambamiti
pamoja na uhalali wa mapato ya Serikali kufuati kuwepo udanganyifu
kwenye biashara hiyo.


Kulingana
na takwimu za mauzo ya Kambamiti nje ya nchi kampuni hiyo ilipaswa
kulipa shilingi milioni 300 kama ushuru wa huduma kwa Halmashauri hiyo
lakini imekuwa ikilipa shilingi milioni 100 kwa mwaka na hivyo kuipunja
Serikali kiasi cha shilingi milioni 200 kila mwaka.

Waziri
Mpina amebaini njama hiyo inayofanywa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia
kwa kushirikiana na Mwekezaji wa Kampuni ya Alphakrust inayofuga samaki
aina ya Kambamiti kisiwani humo kwa lengo la kuiibia Serikali mapato
yake yanayotakiwa kutozwa kama ushuru wa huduma yaani ‘Service Levy’

Alisema
Halmashauri ya Mafia imetengeza makadirio ya kutoza ushuru wa huduma ya
shilingi milioni 9 kwa mwezi kutoka Kampuni ya Apha Krust na kuacha
Kanuni maalumu iliyowekwa kwa mujibu wa Sheria ya ukokotoaji wa mapato
yanayopatikana ya kutakiwa kulipa asilimia 3 ya mapato yote
yanayopatikana kwenye biashara husika.

Udanganyifu
huo umebainika wakati wa ziara ya Waziri Mpina ya kukagua Kituo cha
kutotoleshea vifaranga na Shamba la ufugaji samaki aina ya Kambamiti
lilomilikiwa na Kampuni ya Alphakrust kisiwani Mafia.

Waziri
Mpina katika ziara hiyo aliambatana na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani,
Ramadhani Maneno na Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Mafia
ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Shaib Nnunduma, Wakurugenzi na
Wataalamu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Mpina
alihoji iweje Halmashauri ya Mafia itoze ushuru kinyume cha Sheria
wakati kanuni za ukokotoaji wa mapato zinajulikana na hivyo kuamini kuwa
huo ni mkakati wa siri uliosukwa baina ya Halmashauri ya Mafia na
Kampuni ya Apha Krust kwa lengo la kukwepa kulipa mapato stahiki ya
Serikali.

“Haiwezekani
Halmashauri ya Mafia ikaacha kufuata fumula ya uchukuaji wa ‘service
levy’ uliowekwa na Serikali na kutengeneza utaratibu wake
yenyewe..mwisho wa siku watu wa nje tunachoweza kukielewa ni njama
inayowekwa baina ya Halmashauri na Mwekezaji kuiibia Serikali” alisema
Mpina.

“Kwanini
mkokotoo huo usizingatie sheria takwimu za makusanyo zipo, bei
inayotumika kuuza na masafirisho ya nje ipo kwanini haikutumika
kukokotoa..kwanini itumike fumula ya kukubalina nje ya utaratibu
uliowekwa kwa mujibu wa sheria”alihoji Waziri Mpina.

Waziri
Mpina alisema kama halmashauri inatoza fedha nyingi zaidi za ushuru wa
huduma tofauti na iliyowekwa kwenye Sheria ni makosa kwani Serikali
haiwezi ikatoza fedha ambazo haziko kwenye utaratibu wa sheria lakini
kama halmashauri inakusanya fedha kidogo kuliko sheria inavyosema nalo
ni kosa kwa mujibu wa sheria.

“Kwanini
uchukue fedha kidogo wakati fomula ya kupata makusanyo halisi kwa niaba
ya wananchi ipo..kwanini wewe utumie fumula ya kwako ya kubuni wewe
wakati fumula ya kisheria ipo”alihoji Waziri Mpina.

Mbali
na dosari hizo za ukwepaji kodi, Waziri Mpina alielezea kusikitishwa
kwake na kitendo cha mwekezaji huyo kushindwa kuwashirikisha wananchi
wanaozunguka eneo hilo kujifunza teknolojia hiyo ili kukuza sekta ya
ukuzaji viumbe maji hasa ufugaji wa Kambamiti.

Alisema
Serikali haijapokea maombi yoyote ya upungufu wa wataalamu wenye
utaalamu na uzoefu maalum kuendesha mradi kwani wataalamu hao
wanazalishwa katika vyuo vyetu kikiwemo Chuo Kikuu cha Sokoine cha
Kilimo (SUA), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Dodoma
(UDOM) na Vyuo vya Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA).

“Mradi
huu unaendeshwa kwa usiri na wivu mkubwa kiasi kwamba wananchi wa
kawaida hawawezi kupata utaalamu kupitia mradi huu..kwenye taarifa yenu
sikuona mkichukua vijana wanaomaliza vyuo au kuingia makubaliano na vyuo
(MOU) kufanya mafunzo ya vitendo kwenye mradi huu na kuwalipa kima cha
chini cha mshahara”alihoji Waziri Mpina.

Alisema
wawekezaji kutoka nje wanapofika nchini wanalojukumu katika mikataba
yao ya kusambaza taaluma katika eneo lao la uwekezaji ili kuwawezesha
watanzania wengi kunufaika na uwekezaji wao na kueleza kusikitishwa
kwake na kampuni hiyo kuwabagua wazawa na kuwapa nafasi wageni hata
kwenye kazi ambazo zingeweza kufanywa na watanzania.

“Toka
nimeanza kutembelea miradi hii kuanzia Dar es Salaam nimekuja kwenye
shamba la kambamiti na kituo cha kutotoleshea vifaranga mapokezi na
utolewaji wa maelezo na ufafanuzi unafanywa na wageni hii ni ishara
kwamba uongozi wote umeundwa na wageni au ni sehemu ya kuficha ukweli
juu ya undeshaji wa biashara hiyo’ alihoji Waziri Mpina

Mbali
na hilo Waziri Mpina alisema Serikali inazo taarifa za vijana
wanaokwenda kufanya kazi kwenye uwekezaji huo wanashindwa kufanya kazi
kutokana na ujira mdogo wanaolipwa na mwekezaji huyo na kuvunjika moyo
na kisha kuondoka.

“Kulipwa
mshahara mdogo haijulikani wanalipwa hivyo ili wakate tamaa waondoke na
baadae itengeneze nafasi ya ajira kutoka nje ya nchi au tatizo ni
nini”alihoji Waziri Mpina.

Kwa
upande wake Meneja wa Alphakrust, Ganeshan Vedagiri amelalamikia kukosa
wataalamu wenye weledi na pindi watanzania wanapoajiriwa wanakaa muda
mfupi na kuondoka huku akilalamikia kudaiwa ushuru kwenye halmashauri
zaidi ya moja

Alisema
mradi huo wa Mafia una mabwawa 31 ya Kambamiti ambapo kwa mwaka
huzalisha wastani wa tani 400 huku asilimia 90 ya samaki hao wakiuzwa
nchini ufaransa huku asilimia 10 zikiuzwa hapa nchini. 

 
Kaimu
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mafia, Chuchu Silvery licha ya kuwepo
kwenye ziara hiyo hakuweza kuzungumzia chochote kuhusiana na dosari
hizo.