Vodacom yafungia laini za wateja 157,000

Na MWANDISHI WETU
-DAR ES SALAAM,
WATEJA 157,00 wa Kampuni ya simu za
mkononi ya Vodacom Tanzania wamefungiwa huduma zao kutokana na kushindwa kujisajili
kwa kutumia alama za vidole.

Mkurugenzi
Mtendaji wa Vodacom Tanzania PLC, Hisham Hendi ametangaza uamuzi huo leo
Januari 22, mwaka 2020 jijini Dar es Salaam.
Kutokana na hatua hiyo Hendi amewaomba
wateja wote waliofungiwa laini zao kutembelea vituo vya huduma au mawakala wa
kampuni hiyo zaidi ya 35,000 nchini kusajili laini zao ili kuendelea kufurahia
huduma za kampuni hiyo.
Amesema baadhi
ya maduka yao kwenye miji mikubwa yatakuwa wazi Saa 24 ili kuhakikisha wateja wanaendelea
kupatiwa huduma hususani kwa wenye vitambulisho vya taifa,” amesema Hendi.
Hatua hii inatokana na agizo la
Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA), kuziagiza kampuni zote za simu nchini
kuwafungia wateja ambao wameshindwa kusajili kwa kutumia alama za vidole
ifikapo Januari 20, mwaka huu.
Amesema
wateja walioathiriwa na zoezi hili ni wale tu waliopokea namba za vitambulisho
vya Taifa kutoka NIDA, lakini wameshindwa kujisajili kwa sababu moja au
nyingine.
“Kwa kuwa
zoezi hili ni endelevu, wateja wetu wote ambao hawajapata namba za utambulisho
kutoka NIDA, waendelee na mchakato wa kupata namba hizo au vitambulisho
vitakavyowawezesha kujisajili kwa kutumia alama za vidole na kuepuka usumbufu
wa kufungiwa huduma,” amesema.
Pamoja na
mambo mengine, Hendi amesema zoezi la usajili kwa alama za vidole litasaidia
kupunguza idadi ya matapeli wanaosumbua wateja ambapo itarahisisha vyombo vya usalama
kupambana na matukio hayo ya kitapeli.

Kwa upande
wake, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja, Harriet Lwakatare amesema kwa wale
walioathiriwa na zoezi hili la kufungiwa wasiwe na wasiwasi kwa vile taarifa
zao zitatunzwa kwa muda wa miezi sita ambapo wanatarajiwa wawe wamejisajili kwa
alama za vidole.