Mangula atoa onyo kwa wanaopita kwa wananchi kutangaza nia ya kugombea uongozi

Makamu
mwenyekiti wa CCM Tanzania bara Philipo Mangula ametoa onyo na kuahidi
kuanza kuwachukulia hatua kali za kimaadili kupitia kamati za ngazi
tofauti za siasa ndani ya chama wanasiasa wote ambao wameanza kupita kwa
wananchi na kutangaza nia ya kugombea nafasi mbalimbali jambo ambalo ni
kinyume na kalenda ya chama.


Mangula
ametoa katazo hilo katika kikao cha halmashauri kuu ya chama wilaya ya
Wanging’ombe ambacho kimeketi kwa lengo la kupokea ripoti ya utekelezaji
wa ilani ya Chama kwa mbunge na mkuu wa wilaya hiyo katika kipindi cha
2015 -2020 ambapo amesema kufanya hivyo kunakiuka misingi na maadili ya
chama na kuathiri utendaji wa viongozi waliopo madarakani na kupiga
marufuku kutoa zawadi ama msaada wa aina yeyote bila mawasiliano na
mwakilishi.

Awali
wakiwasilisha ripoti ya utekelezaji mbunge wa jimbo la Wanging’ombe
mhandisi Gerson Lwenge na mkuu wa wilaya hiyo Comrade Ally Kassinge
wamesema licha ya uchanga wa wilaya hiyo lakini katika kipindi cha miaka
mitano wamefanya mabadiliko makubwa katika sekta ya elimu,umeme,viwanda
,miundombinu na uchukuzi na kuahidi kuendelea kuchapa kazi.

Nao
baadhi ya wajumbe akiwemo Juma Nambaila na Paulina Samatta  wanakiri
kuridhishwa na utendaji wa viongozi hao huku wakiwataka mwaka huu
kuelekeza nguvu katika kusogeza nishati ya umeme na utatuzi wa migogoro
ambao umekithiri katika wilaya hiyo.
Katika
kikao hicho nae katibu wa siasa na uenezi wa chama hicho mkoa wa
Njombe  Erasto Ngole anatumia fursa hiyo kuwataka wananchi kujitokeza
kujiandikisha katika daftari la kudumu la mpiga kura ambalo limeanza
kufanyika tangu januari mosi na kuhitimishwa januari 7.