Jeshi la magereza lajipanga kimkakati kuzalisha chakula cha wafungwa kwa mwaka 2020

Na ASP Lucas Mboje, Dodoma

JESHI
la Magereza limejipanga kwa mwaka 2020 kuendelea na utekelezaji wa
jukumu la uzalishaji wa chakula cha kutosha cha wafungwa kwa kutumia
rasilimali zilizopo katika Jeshi hilo ili kufikia adhma ya Serikali ya
awamu ya tano kuhusu kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa magerezani.

Akizungumza
na Maafisa na askari wa Jeshi hilo katika Baraza Maalum la kufunga
mwaka 2019 na kuukaribisha mwaka mpya 2020 jana jijini Dodoma, Kamishna
Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike amesema kuwa Jeshi hilo
tayari limejiwekea mkakati maalum wa kujitosheleza kwa chakula cha
wafungwa magerezani.

Katika
kulifanyia kazi suala hilo, Kamishna Jenerali Kasike amesema kuwa
mavuno yameongezeka katika msimu wa kilimo 2018/2019 ambapo Jeshi hilo
limeweza kuzalisha chakula cha wafungwa katika magereza kumi(10) ya
kimkakati(Songwe, Mollo, Ludewa, Arusha, Pawaga, Idete, Kitete, Isupilo,
Kitai na Kitengule).

“Kupitia
Shirika la Uzalishaji Mali la Magereza(SHIMA), Jeshi limeweza kulisha
unga wa mahindi kwa wahalifu magerezani kwa kipindi cha mwaka mzima
katika mikoa ya Lindi, Ruvuma, Mtwara, Rukwa, Njombe na Katavi. Aidha,
katika mikoa mingine Shirika limeweza kulisha unga kwa miezi mitatu hadi
sita”, amesema Kamishna Jenerali Kasike.

Ameongeza
kuwa kuna mkakati wa muda mrefu wa kuanzisha kilimo cha umwagiliaji kwa
kutumia vyanzo vya maji vilivyopo katika maeneo mbalimbali ya magereza
ambapo Jeshi hilo tayari limekamilisha andiko linalohusu mapindizi ya
kilimo na tayari limewasilishwa serikalini katika hatua mbalimbali za
ngazi ya maamuzi.

Akizungumzia
mafanikio mengi ya kujivunia kwa mwaka 2019 Kamishna Jenerali Kasike
amesema kuwa kumekuwa na mwitikio mkubwa miongoni mwa maafisa na askari
katika kuishi na ajenda mahususi ya Jeshi hilo kuhusu umuhimu wa
kubadilika kimtizamo, kifikra na utendaji kama nguzo ya mabadiliko
katika Jeshi hilo.

“Naomba
nisistize kuwa bado tuendelee kuishi na ajenda hii ya mabadiliko ya
kimtizamo na kifikra katika mwaka mpya 2020 tunaoutarajia kuuanza muda
mfupi ujao kwa kufanya kazi kwa weledi, ubunifu katika maeneo yetu ya
kazi. Tradition die hard”, amesisitiza Kamishna Jenerali Kasike.

Mafanikio
mengine aliyoyaainisha ni pamoja na utekelezaji wa agizo la Serikali
kuhusu kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa, ujenzi wa nyumba za
watumishi wa Jeshi hilo katika maeneo mbalimbali nchini kwa njia ya
ubunifu, udhibiti wa uingizaji wa vitu visivyoruhusiwa magerezani kwa
kufunga CCTV camera katika baadhi ya magereza. Aidha, katika kuhakikisha
kuwa wafungwa waliopo magerezani wanafanya kazi, Jeshi kupitia Shirika
lake limefanikiwa kupata  leseni ya usajili ya kuwatumia wafungwa katika
kandarasi mbalimbali ikiwemo kufanya usafi katika Barabara zilizopo
nchini na shughuli nyinginezo za kuweza kuliingizia faida Shirika hilo.

“Shirika
la Magereza limefanikisha utaratibu wa kuingiza miradi yake yote katika
mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali(GePG) na
hivyo kuziba mianya ya upotevu wa mapato ya Serikali. Pia, Shirika hilo
limeweza kutoa mchango wake Serikalini kiasi cha Tsh. Milioni mia moja
na therasini kwa mwaka 2019”, ameainisha Kamishna Jenerali Kasike.

Aidha,
pamoja na mafanikio hayo Kamishna Jenerali Kasike amebainisha
changamoto zinazolikabili Jeshi hilo ikiwemo ufinyu wa bajeti, uhaba wa
vitendea kazi mbalimbali kama vile magari, vyombo vya mawasiliano, pia
changamoto za makazi na uchache wa nguvu kazi ya maafisa na askari
katika Jeshi hilo.

Kamishna
Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike amehitimisha hotuba yake
leo jijini Dodoma kwa kuwatakia heri ya mwaka mpya 2020 maafisa, askari
pamoja na watumishi wote wa Jeshi hilo na amewataka kuendelea kutekeleza
majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya kazi, Dira na Dhima ya Jeshi
hilo.