Tpdc yaokoa trilioni12.7 kuagiza mafuta nje ya nchi

SHIRIKA
la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika kipindi cha miaka minne
ya Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano imefanikiwa kukoa kiasi cha Tsh.
Trilioni 12.7 kwa kutumia gesi asilia katika kuzalisha umeme badala ya
kutumia fedha za kigeni kuagiza mafuta.

Hayo yamesemwa leo (Ijumaa Desemba 13, 2019) Jijini Dar es Salaam na
Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio wakati alipokuwa
akitoa taarifa yake kwa waandishi wa vyombo vya habari kuhusu 
utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo katika kipindi cha miaka minne
ya Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano.

Mataragio alisema kwa kutumia gesi asilia tangu mwaka 2004, TPDC
imesaidia kuokoa kiasi cha Tsh. Trilioni 30.225 ambazo Tsh. Trilioni
27.6 zingetumika kuagiza mafuta kwa ajili ya kuzalisha umeme au kutumika
kama nishati viwandani.

‘’Kwa kutumia gesi asilia kuzalisha umeme au kama nishati viwandani,
TPDC imelisaidia taifa kutotumia fedha za kigeni kuagiza mafguta kwa
ajili ya kuzalisha umeme au kutumika viwandani, ambapo kwa kipindi cha
miaka minne tumeokoa Tsh. Trilioni 12.7’’ alisema Dkt. Mataragio.

Alisema kuwa uzalishaji wa umeme kwa gesi asilia umeongezeka kutoka
Megawati 553 mwaka 2015 hadi kufikia Megwati 892.7 mwaka 2019 ikiwa ni
ongezeko la asilimia 61, huku asilima 57 ya umeme katika gridi ya taifa
ukizalisshwa kwa kutumia gesi asilia, hatua iliyowezesha kuondoa
upungufu wa umeme katika kipindi cha kiangazi.

Akiainisha mafanikio mengine, Dkt. Mataragio alisema kati ya kipindi cha
mwaka 2016/17 hadi Oktoba 2019, TPDC imechangia kwenye pato la Taifa
kiasi cha Tsh. Bilioni 243.05, ambapo matarajio ya ofisi yake ni
kuhakikisha kuwa kati ya mwaka 2020/21 hadi 2023/24 TPDC inachangia
kiasi cha Bilioni 599.62.

Aidha aliongeza kuwa katika kipindi cha mwaka 2016/17 hadi Oktoba 2019,
TPDC imechangia kwenye mfuko wa mafuta na gesi asilia kiasi cha Tsh.
Bilioni 120.56, ukiwa ni mfuko maalum ulioanzishwa kwa mujibu wa Sheria
ya Petroli ya mwaka 2015, na pia kwa mwaka 2018/19 TPDC imefanikiwa
kutoa Gawio kwa Serikali la kiasi cha Tsh. Bilioni 2.5.

Kwa mujibu wa Dkt. Mataragio alisema katika kipindi cha miaka minne
kumekuwepo na ongezeko la matumizi ya gesi asilia kwenye magari, ambapo
hadi sasa kuna magari 305 yanayotumia gesi asilia katika Jiji la Dar es
Salaam na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka zaidi, ambapo TPDC
inatarajia kuweka mikakati madhubuti  ya kufanikisha mpango katika Jiji
la Dar es Salaam.

Akitaja mikakati hiyo, Dkt. Mataragio alisema TPDC ipo katika
utekelezaji wa kujenga vituo vikubwa viwili vya CNG katika Jiji la Dar
es Salaam ambavyo vitawezesha usambazaji wa gesi asilia katika mfumo wa
CNG kwa ajili ya magari na  kuwa na vituo vya kujazia gesia asilia
katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam.

Kuhusu usambazaji wa gesi asilia majumbani, Dkt. Mataragio alisema hadi
kufikia Novemba 2019, matumizi ya gesi asilia majumbani katika Jiji la
Dar es Salaam imefikia yyumba 73 mwaka na wakati kwa Mkoa wa Mtwara
idadi ya nyumba zinazotumia gesi asilia zimefikia 385, ambapo katika
bajeti ya mwaka 2019/2020 TPDC imepanga kuunganisha nyumba zaidi ya 1500
kwa Jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa Mtwara.