Kijana wa miaka 22 atupwa jela miaka 30 kwa kumbaka mwanamke wa miaka 27

Mahakama ya Wilaya ya Pangani mkoani
Tanga, imemuhukumu Kijana Mahadi Elias maarufu kwa jina Maiko, mwenye
umri wa miaka 22 mkazi wa Kijiji cha Stahabu wilayani humo, kifungo cha
miaka 30 jela kwa tuhuma za kumbaka mwanamke mwenye umri wa miaka 27.

Hukumu hiyo imetolewa Jana Disemba 2,
2019, na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo Joel Mnguto, ambapo
Maiko amehukumiwa kwenda jela miaka 30 na kutakiwa kumlipa fidia
mwanamke huyo ya Shilingi laki tatu kwa kosa la kufanya kitendo cha
ubakaji huku akijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Inadaiwa Maiko alitenda kosa hilo April
5, 2019, majira ya usiku, katika kijiji cha Sange, baada ya kumvamia
mwanamke huyo chumbani alikokuwa amelala na kisha kumuingilia kimwili
bila ridhaa yake, huku akimuwekea kisu shingoni na kumtisha kuwa
asipokubali atamuuwa kwa kumchinja.

Awali mtuhumiwa alikana kosa hilo ambapo
upande wa mashtaka ulilazimika kuleta mashahidi 11 ili kuthibitisha
kosa hilo, ambapo pamoja na mshtakiwa kujitetea, ushahidi ulipokamilika
mtuhumiwa alikutwa na hatia.