Nsato marijani : umakini unahitajika tunapohakiki wakimbizi dar

Na Veronica Mwafisi, MOHA-Dar es Salaam
UHUISHAJI takwimu za wakimbizi waishio jijini Dar es Salaam na mikoa
mingine nchini, unapaswa kufanywa kwa umakini mkubwa kwani unagusa
usalama wa nchi. 

Mkurugenzi Msaidizi wa Uendeshaji Makambi na Makazi, kutoka Wizara ya
Mambo ya Ndani ya Nchi, Idara ya Huduma kwa Wakimbizi, Nsato Marijani,
aliyasema hayo jana wakati akifungua mafunzo ya uhuishaji takwimu za
wakimbizi. 

Mafunzo hayo yalifanyika kwenye Ukumbi wa Polisi Officer’s Mess,
Oysterbay, Dar es Salaam yakihusisha watendaji wa Idara ya Huduma kwa
Wakimbizi, Uhamiaji, Ofisi ya Rais, Polisi pamoja na UNHCR. 

Alisema uhuishaji takwimu utahusisha wakimbizi wote waishio jijini Dar
es Salaam wenye nyaraka, walioruhusiwa kuishi nje ya kambi za wakimbizi,
maeneo mengine kuanzia kesho (Novemba 4), saa 2 asubuhi hadi Novemba 7,
mwaka huu. 

Alifafanua kuwa, uhuishaji huo utafanyika katika Ofisi za Shirika la
Relief of Development Society (REDOSO), zilizopo eneo la Biafra,
Kinondoni. 

“Matarajio ni kuhuisha takwimu za wakimbizi 243 lakini idadi hiyo
inaweza kuongezeka kutokana na wakimbizi kutoka nchi mbalimbali ambao
watajitokeza. 

Marijani alisema idara zote ambazo zinahusika na uhuishaji takwimu hizo,
zinapaswa kufanya uhakiki huo kwa umakini mkubwa kwani zoezi hilo
linagusa usalama wa nchi. 

“Jambo la msingi fanyeni kazi kwa ushirikiano na umoja kati ya watendaji
wa idara za serikali na UNHCR, hakuna aliye juu ya mwingine,”
alifafanua Marijani. 

Alifafanua kuwa, katika uhuishaji huo zinaweza kutokea changamoto ambapo
utatuzi wake unapaswa kushirikisha viongozi na watendaji wa pande
zote. 

Afisa Mkuu wa Uendeshaji, Utawala na Makambi kutoka idara hiyo, Stephen
Msangi, alisema wanatarajia kuhuisha taariza za wakimbizi 231
waliojadiliwa. 

Alisema pia kua wakimbizi 12 ambao wameongezeka hivi karibuni hivyo
kufikia idadi ya wakimbizi 243 walioandikishwa ambao taarifa zao
zitahakikiwa na kuthibitishwa. 

Naye Monday Iddi ambaye ni Afisa Hifadhi ya Wakimbizi mkoani Kigoma,
alisema lengo la uhuishaji huo ni kufahamu idadi ya wakimbizi waliopo
katika mikoa mbalimbali nchini.

“Baada ya uhuishaji, taarifa zao zitakuwa katika mfumo hivyo watashindwa
kujiandikisha zaidi ya mara moja, uhuishaji huu utahusisha alama za
vidole na macho (mboni),” alisema. 


Mkimbizi yeyote ambaye hatajitokeza wakati wa uhuishaji takwimu taarifa zake hazitahuishwa, usajili wake utasitishwa.
Wakimbizi hao wanatakiwa kufika na nyaraka za utambulisho zikiwemo barua
ya uthibitisho wa mkimbizi, usajili, kibali cha kuishi nje ya kambi,
vyeti vya kuzaliwa. 

Nyaraka nyingine ni vyeti vya ndoa, hati ya kusafiria, vitambulisho vya
kazi, shule, chuo na nyaraka nyingine yoyote inayomtambulisha mkimbizi
ambayo inatambulika kisheria. 

Shughuli zote zinazohusiana na uhakiki wa taarifa za mkimbizi na waomba
hifadhi zinatolewa bure ambapo uhuishaji huo hautahusisha wakimbizi wa
mwaka 1972. 

Wakimbizi hao ni wale wanaotoka makazi ya Ulyankulu, Katumba, Mishano na waishio vijijini mkoani Kigoma.