Waziri mkuu: nchi yetu inahitaji wataalamu wa sekta ya uvuvi


WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amesema Tanzania inahitaji kupata watendaji wa sekta ya
uvuvi kuanzia ngazi ya vitongoji kwani kuna vijiji vina mito, maziwa na
baadhi vimepakana na bahari na hivyo kutoa fursa za uvuvi.

“Nchi yetu
inahitaji kupata watendaji kuanzia ngazi ya vitongoji kwani vipo vijiji
vyenye fursa za uvuvi hivyo vinahitaji maofisa ugani ili waweze kufanya
kazi vijijini na katika vitongoji, lengo likiwa ni kuwasaidia wavuvi
wadogowadogo wajue namna bora ya kuvua na kuhifadhi samaki,” amesema.

Waziri Mkuu
ametoa kauli leo jioni (Alhamisi, Novemba 28, 2019), wakati
akizungungumza na wahadhiri na wanafunzi mara baada ya ziara yake ya
kutembelea Kampasi ya Kunduchi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Amesema hivi
sasa Serikali inaandaa mazingira mazuri ya kuendesha sekta ya uvuvi kwa
kupata watalaamu wa ngazi mbalimbali watakaoisimamia sekta hiyo.

“Serikali ya
Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli ambayo imejikita
katika ujenzi wa uchumi wa viwanda inasisitiza uwepo wa vyuo vya ngazi
mbalimbali ili tuweze kupata watalaamu wa kuendesha viwanda
vinavyojengwa nchini,” amesema.

Amesema
Serikali inawatambua na inawahitaji sana wasomi wanaopata taaluma zao
katika vyuo mbalimbali hapa nchini ikiwemo  kampasi ya Kunduchi ya Chuo
Kikuu cha Dar es salaam  ambayo kwa sasa inatumika kwa ajili ya kutoa
mafunzo kwa vitendo ya shahada ya awali, kufundishia na kufanya utafiti
kwa wanafunzi wa Shahada ya Uzamili pamoja na wafanyakazi watafiti.

Waziri Mkuu
amesema angependa kuona watafiti na watalaam wanapewa fursa ya kuongoza
na kusimamia maeneo mbalimbali yanayohusiana na utafiti walioufanya ili
kupata matokeo sahihi na chanya ya utafiti wao. 

Amesisitiza
kuwa Dkt. John Pombe Magufuli alitoa maelekezo thabiti ambayo
amemkabidhi Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Bw. Luhaga Mpina ambaye
ameyafanyia kazi  na yameleta mafanikio makubwa katika sekta ya uvuvi
nchini.

“Hatua ya
kwanza ya kuboresha sekta ya uvuvi ilikuwa ni kuwaondoa watumishi wabovu
na wasio waamifu  na nafasi zao kuwapa watumishi  wazuri, wenye taaluma
ya uvuvi, waaminifu  na wanaojali zaidi maslahi ya Taifa, kazi ambayo
imefanywa na Waziri na watendaji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi,” amesema.

Naye Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge,  Ajira, Kazi ,Vijana na
Wenye Ulemavu, Bibi Jenista Mhagama amesema Serikali inaitegemea sana
Kampasi ya Kunduchi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam  kwa vile watalaam
wanaopata taaluma zao katika kampasi hiyo wanahitajika sana katika
maendeleo ya uvuvi nchini.

  

Amesema Serikali
ya Awamu ya Tano imeamua kujenga uchumi wa viwanda ambavyo vitatumia
malighafi inayopatikana nchini ikizalishwa na Watanzania wenyewe na
bidhaa zake kuuzwa ndani na nje ya nchi ili kupata fedha za kigeni.

Naye Waziri
wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amewahakikishia Watanzania kuwa hivi
sasa idadi ya samaki na mapato ya Serikali yanayotokana na uvuvi
yameongezeka.

Amesema kabla
ya Serikali ya Awamu ya Tano kuanza kazi ya usimamizi wa  na udhibiti
wa uvuvi nchini, mauzo ya bidhaa za uvuvi nje ya nchi yalikuwa ni sh.
bilioni  371 kwa mwaka na hivi sasa Serikali inajipatia sh. biloni 691
kwa mwaka.