Waziri mpina azindua agenda za utafiti na kuibua tafiti zilizofichwa makabatini

WAZIRI
wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amezindua Agenda ya Kitaifa ya Utafiti
wa Mifugo, Uvuvi na Ukuzaji wa Viumbe Maji ya mwaka 2020-2025 na
kutangaza kuzifumua na kuziibua tafiti zote  zilizofanywa na wasomi na
kutelekezwa kwenye makabati miaka ya nyuma na kuziingiza kwenye mfumo
rasmi wa matumizi ili kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi na maendeleo.


Pia
agenda hizo zitaleta msisimko mpya wa kufanya utafiti nchini na kuleta
mageuzi makubwa ya kiuchumi na maendeleo tofauti na ilivyokuwa kipindi
cha nyuma ambapo tafiti nyingi zilifanywa na kutelekezwa kwenye makabati
na watafiti mbalimbali wakiwemo Wanafunzi wa Shahada ya Uzamili
(Masters Degree)  na Shahada ya Uzamivu (PHD) katika vyuo vikuu
mbalimbali.

Akizungumza
wakati wa uzinduzi wa agenda hizo kitaifa katika Chuo Kikuu cha Sokoine
cha Kilimo (SUA),  Kampasi ya Mazimbu mjini Morogoro, Waziri Mpina
aliziagiza Taasisi ya Utafiti wa Mifugo(TALIRI) na Taasisi ya Utafiti wa
Uvuvi(TAFIRI) kubadilika ili kufanya tafiti kwa vigezo vilivyowekwa na
kuleta mabadiliko chanya katika sekta za mifugo na uvuvi nchini.

Waziri
Mpina alisema chimbuko la kuandaliwa kwa ajenda hizo za utafiti ni
baada ya kubaini kuwa ajenda zilizokuwepo awali za Mifugo na Uvuvi
zilishindwa kuibua na kuzitumia tafiti zilizofanywa kuchochea mabadiliko
kwenye sekta hiyo muhimu ya uzalishaji.

Pia
ajenda za utafiti zilizokuwepo za Mifugo na Uvuvi hazikuwa na utaratibu
wa kuzitambua, kuziorodhesha na kuzitumia tafiti zinazofanywa na
Wanafunzi wa Shahada ya Uzamili (Masters Degree) na Uzamivu (PHD) lakini
sasa ajenda za utafiti zilizozinduliwa zimeweka utaratibu wa namna ya
kuzitambua, kuziorodhesha na kuzitumia tafiti za wasomi hao.

“Haiwezekani
tafiti za wasomi wa kiwango cha juu kiasi hicho wanazozifanya wakati wa
kukamilisha masomo yao ziishie kupata alama za ufaulu na kutupwa kwenye
makabati, Leo kila mhitimu atalazimika kuandaa policy brief ambayo
itawezesha watumiaji na Serikali kurekebisha au kuandaa Sera na Sheria”
alisema Waziri Mpina.

Aliongeza
kuwa Ajenda za Utafiti zilizokuwepo za Mifugo na Uvuvi hazikuwa na
utaratibu wa kuweka Kanuni ambazo zitahakikisha kuwa utekelezaji  wa
ajenda za utafiti unafanyika, lakini ajenda za utafiti iliyotangazwa
inaweka Kanuni zitakazotoa mwongozo na usimamizi wa utekelezaji na
wajibu wa kila mhusika.

Aidha
Waziri Mpina alibainisha kuwa ajenda za utafiti zilizokuwepo za Mifugo
na Uvuvi hazikuwa na utaratibu wa kuwaunganisha Watafiti wa Mifugo na
Uvuvi nchini, na hivyo kupelekea kila mmoja kufanya utafiti kivyake hali
iliyosababisha jambo moja kufanyiwa utafiti na mtafiti zaidi ya mmoja
na kukosa jukwaa la kuratibu na kuchambua tafiti zinazofanywa nchini.

“Agenda
ninayoizindua leo inakwenda kujumuisha watafiti na wataalam mbalimbali
waliobobea katika fani za mifugo, uvuvi na ukuzaji wa viumbe maji ili
kuyapitia matokeo ya utafiti, teknolojia zilizoibuliwa na utafiti na
kuzisambaza kwa watumiaji kwa manufaa ya Taifa” alisema Waziri Mpina

Pia
Waziri Mpina alibainisha mapungufu mengine yaliyomo kwenye ajenda za
utafiti zilizokuwepo za Mifugo na Uvuvi ni pamoja na kutoweka msingi
mzuri wa kusimamia Watafiti na kufanya tafiti kulingana na mahitaji ya
soko badala yake  Taasisi za Utafiti na Watafiti kufanya tafiti nyingi
za nje na mambo muhimu ya wananchi yanayohitaji kufanyiwa utafiti
kutelekezwa.

“Leo
hii agenda ninazozizindua zimeweka utaratibu wa kuzingatia vipaumbele
vya kitaifa, kupanua mtandao wa utafiti  na kufanya tafiti zote
kulingana na mahitaji ya wananchi.  Mfano katika maeneo ya nyama,
maziwa, samaki, ngozi, chakula cha samaki na mifugo, magonjwa, malisho
na migogoro” alisema Mpina.

Aidha
dosari nyingine zilizokuwepo kwenye ajenda za utafiti zilizokuwepo za
Mifugo na Uvuvi ni kutojumuisha katika vipaumbele masuala mengi muhimu
yenye changamoto nyingi ikiwemo  Mitaala na hali ya ajira.

Mpina
alisema mitaala inapoanzishwa haifanyiwi utafiti wa mara kwa mara
matokeo yake mafunzo yanayotolewa sio yale yanayohitajika katika soko la
ajira huku Wanafunzi wanaohitimu mafunzo hawajulikani wanakwenda wapi
baada ya kuhitimu na hakuna mfumo wowote wa uratibu.

“Ukienda
kwa wafugaji wanaofuga na kuchunga sio hao waliosomea mifugo, ukienda
kwa Wavuvi na Ukuzaji viumbe maji wanaovua na kufuga si hao waliosomea
taaluma hizo, ukienda viwandani vilevile”alisema Mpina.

Pia
Masoko na Biashara, Uongezaji wa mnyororo wa thamani wa mazao ya mifugo
na uvuvi (Livestock & Fisheries value chain & value addition),
agenda iliyopita ilizingatia uzalishaji pekee bila kuangalia upande wa
soko wakati vitu hivi vinakwenda kwa pamoja kwani hakuna uzalishaji bila
soko.

Waziri
Mpina pia alisema licha ya kushamiri kwa migogoro ya wafugaji na
watumiaji wengine wa ardhi na eneo hilo kugubikwa na changamoto nyingi 
ikiwemo  mifugo kutaifishwa, kupigwa risasi, kufilisiwa, kuuwawa kwa
watu na mifugo  na kupigwa faini kubwa kiasi cha kutishia uendelevu wa
sekta lakini eneo hili halikujumuishwa katika Agenda ya utafiti
iliyopita.

Pia
masuala mtambuka, afya ya wanyama na magonjwa ya afya ya jamii
(Zoonotic Diseases) ambapo hivi sasa asilimia 60 ya magonjwa
yasiyoambukiza yanatokana na mazao ya mifugo, malisho, nyanda za malisho
na vyakula vya mifugo na samaki, uvuvi endelevu katika maji ya asili
(Uvuvi Haramu na utoroshaji wa mazao ya uvuvi)  ambayo nayo
hayakuzingatiwa katika agenda za utafiti zilizopita .

Hivyo
Waziri Mpina aliwahakikishia watanzania kuwa Wizara yake itaendelea
kushirikiana na wadau wote kuhakikisha kuwa matokeo ya tafiti
zinazofanywa zinawafikia walengwa kwa wakati ili tafiti hizo ziongeze
tija na kipato kwa watuamiaji na Taifa kwa ujumla. 

 
Makamu
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Profesa Raphael
Chibunda alimhakikishia Waziri Mpina kuwa kwa niaba ya watafiti wa Chuo
kikuu hicho watatakwenda kuwa sehemu ya utekelezaji wa agenda hizo.