Bodi ya rea yampa siku 14 mkandarasi wa umeme mkoani simiyu kujirekebisha

Na Teresia Mhagama, Simiyu

Bodi
ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imempa siku 14 mkandarasi wa umeme
vijijini mkoani Simiyu kuongeza kasi ya usambazaji umeme katika vijiji
alivyopangiwa la sivyo Bodi hiyo haitasita kuchukua hatua mbalimbali za
kimkataba ikiwemo ya kusitisha mkataba.

Mwenyekiti wa Bodi ya REA, Wakili Julius Kalolo  alisema hayo tarehe 16
Novemba, 2019 wilayani Busega mkoani Simiyu mara baada ya kukagua kazi
ya usambazaji umeme katika Vijiji mbalimbali vya wilaya ya Bariadi na
Busega akiwa amembatana na Mjumbe wa Bodi hiyo, Dkt Andrew Komba na
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Amos Maganga.
” Bodi haijaridhishwa na kasi ya mkandarasi huyu kwani amepewa kazi ya
kupeleka umeme katika vijiji 152 vya Mkoa wa Simiyu lakini mpaka sasa
amesambaza katika vijiji 54 ambayo ni takribani asilimia 30 tu ya kazi
anayopaswa kufanya hivyo tumempa siku 14 aonyeshe mabadiliko la sivyo
tutachukua hatua.” Alisema
Wakili Kalolo alieleza kuwa, Serikali imetimiza jukumu la kutoa malipo
kwa mkandarasi huyo ili kazi ya usambazaji umeme ifanyike kwa kasi hivyo
visingizio vya ucheleweshaji wa kazi havikubaliki kwani kwa mujibu wa
mkataba wa mkandarasi huyo anapaswa kumaliza kazi mwezi Aprili mwaka
2020.
Aidha, alimwagiza mkandarasi huyo kampuni ya Whitecity Guangdong JV,
kuwasilisha mpango kazi wake kwa Bodi hiyo, Mameneja wa TANESCO mkoani
Simiyu pamoja Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu ili kuweza
kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa kazi anazofanya.
Awali Bodi hiyo ilikutana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Jumanne
Sagini ambapo, Mjumbe wa Bodi ya REA, Dkt. Andrew Komba alitoa shukrani
kwa viongozi wa mkoa wa Simiyu kwa kufuatilia utekelezaji wa kazi ya
usambazaji umeme vijijini.
Aidha, aliomba kasi hiyo iongezeke ili Mradi wa usambazaji umeme
vijijini wa Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Kwanza (REA III) ukamilike kwa
wakati.
Alisema kuwa, msukumo wa kuwafuatilia wakandarasi unahitajika ili
kutimiza lengo la Serikali  la kupeleka umeme katika vijiji vyote
vilivyopo katika mpango  wa REA III mzunguko wa kwanza ifikapo mwezi
Disemba mwaka huu.
Aidha alitoa wito kwa viongozi wa Serikali katika  ngazi mbalimbali za
mkoa, kuhamasisha wananchi kujiunga na huduma ya umeme kwani Serikali
imefanya uwekezaji mkubwa katika kuwasambazia umeme wananchi hivyo
wanapaswa kuunganisha umeme kwa wingi na kuutumia katika shughuli za
kiuchumi na kijamii