Mradi wa kilimo cha umwagiliaji uliotolewa na tasaf ukangemakete wafanikiwa kuinua kipato kwa wanufaika



Wanufaika wa mpango wa kunusuru
kaya masikini katika kijiji cha Ukange kata ya Lupila wilayani Makete
mkoani Njombe wameipongeza TASAF kwa kuwapa mradi wa kilimo cha
umwagiliaji wenye thamani ya mil 71 ambao wamedai kuwa tangu waanze
kutekeleza mradi huo umekuwa na matokeo chanya katika maisha yao.


Mradi huo ambao unatekelezwa
kupitia kikundi cha wanufaika 71 wa mpango umetajwa kuimarisha kipato
kwa wanufaika na wanakijiji wanaofanya kilimo cha umwagiliaji katika
kata hiyo kwa kuwa wamekuwa wakifanya shughuli za kilimo cha viazi
,bustani na nyingine nyingi katika chote cha mwaka hatua ambayo inawapa
uhakika wa mlo pamoja ujenzi wa nyumba za kuishi , kusomesha watoto na
mambo mengine.


Stelia Sanga ni mmoja wa wanufaika
wa mpango wa TASAF katika kijiji cha Ukange akizungumzia hali ya maisha
ya familia yake ilivyokuwa awali kabla ya kuanza kupata fedha za mpango
huo amesema maisha yake yalikuwa duni kiasi ambacho hakuwa na uhakika
wa milo mitatu na kuishi katika nyumba ya nyasi.


“Kabla ya kuanza kutambuliwa na
TASAF maisha yangu na familia yangu yalikuwa sio kitu ,sikua na uhakika
wa chakula na kuishi katika nyumba ya nyasi hivyo tangu nianze kupokea
fedha hizi niliweka malengo na kuanza kudunduliza mpaka nikajenga
“alisema Sanga.


Kuhusu matokeo chanya ya
kuanzishwa kwa mradi wa umwagiliaji kijijini hapo ambao umetolewa na
TASF  Maltin Msigwa ambaye pia ni mnufaika amesema umeweza kumuongezea
kipato hatua ambayo imemfanya na yeye kuanza kufanya kilimo cha viazi
katika shamba la ekari moja na nusu na pia kuweza kujenga nyumba ya
kuishi pamoja na ufagaji wa kuku na mbuzi hatua ambayo ilikuwa ni ngumu
kufanyika awali.


Kufuatia mafanikio hayo kuletwa na
mradi huo wakazi wa kijiji cha Ukange wanashindwa kuzuia hisia zao kwa
serikali ya awamu ya tano kwa kuwapa mradi huo na kuomba kuendelea
kuwapa nafasi ya upendeleo endapo ukiendelea ili waweze kuondokana na
wimbi la umasikini.


Mbali na hilo kijiji hicho ambacho
kimekuwa kikifanya kilimo cha viazi mviringo kwa wingi kimetoa rai kwa
serikali kuwatafutia masoko ya viazi ili kuepusha unyonyaji mkubwa
unaofanywa na wafanyabiashara na walanguzi ambao wamekuwa wakinunua
viazi kwa debe badala ya kilo na kuwanyonya ambapo wamesema kwa wastani
kila debe moja wamekuwa wakinunua shilingi elfu 2 badala ya elfu 7 jambo
ambalo linawatia hasara kubwa.


Unyonyaji huo unawafanya
kupaza sauti kwa serikali kuanzisha vituo vya pamoja vya biashara ili
kuwa na sauti ya pamoja ya bei pamoja na viwanda vya kuongeza thamani
mazao yao  ili kutengeneza faida.


Kufuatia wakulima kutoa kilio
hicho kwa serikali mtandao huu unapiga hodi kwa mkurugenzi wa
halmashauri ya wiilaya ya Makete Fransis Namaumbo ambaye anaeleza
jitihada ambazo zimeendelea kuchukuliwa ili kuhakikisha wakulima
wanapata masoko ya uhakika ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara
pamoja uimarishaji wa vyama vya ushirika ili kuvitumia kama kituo cha
biashara ya malighafi ama bidhaa wanazozalisha.


Namaumbo amesema serikali iko
katika maboresho ya barabara za kuelekea masokoni kwa kiwango cha lami
hatua ambayo itamfanya mkulima kusafirisha mazao yake mpaka masokoni na
kuuza kwa faida huku pia akidai kuwa taratibu za kuanzisha maghala
zimeanza.


“Tunashukuru serikali ya awamu ya
tano imeanza ujenzi wa barabara ya Njombe hadi Makete Kwa Kiwango cha
Lami pamoja kuvijengea uwezo vyama vya ushirika ili vitumike na wakulima
kama vuto vyao vya biashara ili kudhibiti unyonyaji unaofanywa na
wafanyabiashara” alisema Fransis Namaumbo.


Nae Jakrin Mlosso ambaye ni
mratibu wa TASAF katika halmashauri ya wilaya ya Makete akieleza sababu
ya kutoa mradi wa umwagiliaji katika kijiji cha Ukange anasema ni
kutokana na wakazi wake kujikita zaidi katika shughuli za kilimo.


Kuhusu kiwango cha fedha
kilichotolewa kutekeleza miradi tangu 2015 hadi sasa Mlosso anasema ni
bil 2.5 ambazo zimetumika kutekeleza miradi 39 kutoka sekta ya
afya,elimu,barabara na nyinginezo huku nae afisa maendeleo kata ya
Lupila Veronica Kalimba akidai mpango huo wa kunusuru kaya Masikini
umeleta mabadiliko makubwa ikiwa ni pamoja na kupunguza kiwango cha
udumavu.