Dkt.ndumbaro aipongeza nishati kuwa ya kwanza kutekeleza agizo la rais

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais,
Menejimenti  ya Utumishi wa Umma na Utawala bora, Dkt. Laurian Ndumbaro(
aliyesimama) akizungumza na washiriki wakati akifunga Kikao kazi cha
Wakurugenzi,Mameneja wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wa Wizara
ya Nishati na Taasisi zilizochini yake kilichofanyika mkoani Tanga

.
Mkurugenzi wa Utawala na
Rasilimaliwatu wa Wizara ya Nishati, Raphael Nombo(kushoto) akizungumza
na Washiriki wa Kikao kazi cha Wakurugenzi,Mameneja wa Utawala na
Usimamizi wa Rasilimaliwatu wa Wizara ya Nishati na Taasisi zilizochini
yake(hawapo pichani) kabla ya kufungwa kwa kikao hicho.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais,
Menejimenti  ya Utumishi wa Umma na Utawala bora, Dkt. Laurian Ndumbaro(
katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa Kikao
kazi cha Wakurugenzi,Mameneja wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu
wa Wizara ya Nishati na Taasisi zilizochini yake , baada ya kufunga
kikao hicho kilichofanyika mkoani Tanga.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais,
Menejimenti  ya Utumishi wa Umma na Utawala bora, Dkt. Laurian Ndumbaro(
kushoto) akiwa amembatana na Wakurugenzi,Mameneja wa Utawala na
Usimamizi wa Rasilimaliwatu wa Wizara ya Nishati na Taasisi zilizochini
yake ambao wanaofanya kikao kazi mkoani Tanga ,kilichofungwa na Katibu
Mkuu huyo.
Meneja Mkuu wa Kampuni tanzu ya
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania,( GASCO), Mhandisi Baltazar
Mroso akitoa neno la Shukrani baada ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais,
Menejimenti  ya Utumishi wa Umma na Utawala bora, Dkt. Laurian Ndumbaro,
kufunga kikao kazi cha Wakurugenzi,Mameneja wa Utawala na Usimamizi wa
Rasilimaliwatu wa Wizara ya Nishati na Taasisi zilizochini yake
Na Zuena Msuya, Tanga
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais,
Menejimenti  ya Utumishi wa Umma na Utawala bora, Dkt. Laurian Ndumbaro
ameipongeza Wizara ya Nishati na Taasisi zilizo chini yake kwa kuwa ya
kwanza  kutekeleza agizo la Rais kwa kufanya vikao vya pamoja vya
kujadili masuala mbalimbali yanayohusu utumishi wa umma ,utendaji kazi
na utawala bora kati ya watumishi, wafanyakazi pamoja na viongozi katika
sehemu za kazi.
Dkt. Ndumbaro alisema hayo Novemba
15, 2019, wakati akifunga Kikao kazi cha Wakurugenzi,Mameneja wa
Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wa Wizara ya Nishati na Taasisi
zilizochini yake kilichofanyika mkoani Tanga.
Alisema kuwa kwa kufanya mikutano
ya namna hiyo, ni dhahiri Wizara ya Nishati na Taasisi zilizochini yake
imelenga kutekeleza agizo la Rais na dhima ya serikali inayoelekeza 
utumishi wa umma wenye uwajibikaji, uadilifu, unaofanya kazi kwa juhudi
na maarifa,uzalendo, na ule ambao watumishi wake wanakuwa na sifa
stahiki.
Dkt. Ndumbaro alisema kuwa Wizara
ya Nishati inatekeleza agizo hilo kwa kujadili mambo mbalimbali
yanayohusu Wizara na Taasisi zilizochini yake kwa lengo la kuboresha
utendaji kazi, utumishi wa Umma na Utawala bora sehemu za kazi.
Alisema kuwa utumishi wa umma
unaozingatia misingi yake hujenga utawala bora kwa taifa na wananchi
wake, kwa kuimarisha mahusiano mazuri kati ya wananchi, watumishi wa
umma, wafanyakazi pamoja na viongozi katika nyanja mbalimbali kwa lengo
la kupata matokeo chanya kwa taifa na wananchi wake.
Sambamba na hilo alisema kuwa
wizara hiyo na taasisi zake inatekeleza miradi mingi ya maendeleo kwa
wananchi na taifa, hivyo kuwepo kwa utumishi wa umma wenye kuzingatia
misingi imara sehemu za kazi ni chachu ya kuongeza ari ya watumishi
katika kila sekta kufanya kazi kwa bidii na kujituma bila kuchoka na
kuweka mbele uzalendo na maslahi taifa.
Aliwaelekeza wasimamizi wa
rasilimaliwatu kutoa motisha kwa watumishi au wafanyakazi  wanaofanya
kazi vizuri kwa kuwapatia vyeti au barua maalumu ya utambuzi ambazo
zitaweka katika eneo la mapokezi ili kuinua ari ya kufanya kazi kwa
bidii kwa kila mtumishi au mfanyakazi, na pia kutoa adhabu ya namna hiyo
kwa wale ambao hawafanyi vizuri kazini.
Aliwasisitiza watumishi wa umma
kutofanya kazi kwa mazoea na kwamba watambue kuwa mtumishi wa umma
unaweza kufanya kazi katika ofisi yoyote ya umma iliyopo nchini, na
kwamba wasikariri kuwa watakaa sehemu moja siku zote.
“Watumishi wa umma muwe na tabia
kama ya kuvaa na kuvua makoti tofauti, kwa maana leo utakuwa katika
kutuo cha kazi A, kesho utapelekwa Y, au P na baadaye G, huu ni
utaratibu uliowekwa kwa manufaa ya kujenga na kuboresha utumishi wa
umma”,alisisitiza  Dkt.Ndumbaro 
Aidha aliendelea kukumbusha kuwa
watumishi pamoja na wafanyakazi wapewe nafasi za kwenda kusoma yale
yenye tija kwa wizara ama taasisi husika, na mafunzo hayo yatolewe kwa
watu wote wa kila idara na siyo kupendelea mtu mmoja.
Vilevile alirudia kuwaeleza
watumishi wa umma kuendelea kutunza siri za serikali na kulinda mali ya
umma bila kusahau kupiga vita vitendo vya rushwa.
Katika zoezi linaloendelea la
kuhakiki watumishi wa umma, serikali imebaini kuwa kuna watumishi ambao
majina yaliyopo katika vyeti walivyosomea na majina katika barua
walizoajiriwa ni tofauti, hivyo wanaendelea kufanya utafiti kwa
kushirikisha vyombo vya serikali ili kubaini kama vyeti hivyo ni vya
watumishi hao kihalali au ni vya watu wengine ili waweze kutoa maamuzi
sahihi wakati ukifika.