Serikali kuajiri walimu wapya 16,000

Serikali imesema inatarajia kuajiri walimu 16,000 wa shule za msingi na sekondari muda wowote kuanzia sasa.


Waziri
Mkuu Kasim Majaliwa, alitangaza neema hiyo bungeni jana alipojibu swali
la Mbunge wa Mlalo, Abdallah Shangazi (CCM), aliyetaka kufahamu mkakati
wa serikali kuhakikisha sekta za elimu na afya zinakuwa na watumishi
wengi.

“Sekta
za elimu na afya zina upungufu mkubwa sana wa watumishi. Sasa, ni upi
mkakati wa serikali kuhakikisha tunapata watumishi wa kutosha kwenda
kuwahudumia Watanzania?” mbunge huyo alihoji.

Katika
majibu yake, Waziri Mkuu alikiri sekta hizo mbili zina uhitaji wa
watumishi kutokana na serikali kutanua huduma zake hadi ngazi ya
vitongoji.

“Serikali
imeanza kutoa vibali vya ajira katika sekta hizi mbili za afya na
elimu, hata kwenye kilimo. Mwaka jana, tuliajiri watumishi 6,000 na sasa
tuna kibali ambacho kitatoka hivi karibuni cha watumishi 16,000 kwa
upande wa sekondari na msingi.

“Tunaamini
baada ya ajira hizi kwenye sekondari na elimu msingi, tutakuwa
tumepunguza kwa kiasi kikubwa uhaba wa walimu, hivyo hivyo kwenye sekta
ya afya, tunataka kuhakikisha tunapeleka wataalamu. Mkakati wa kujenga
miundombinu utakwenda sambamba na kuajiri wataalamu,” alisema.

Aliongeza
kuwa serikali imefanya maboresho makubwa na sera inaeleza kuwa kila
kata kuwe na kituo cha afya na kila wilaya iwe na hospitali. Alisema
kinachoendelea kwa sasa ni ujenzi wa zahanati na vituo vya afya vyenye
uhitaji wa madaktari.