Mbunge husna mwilima aomba radhi, atengua kauli yake kwa wanawake wa shirika la ndege kuwa hawana mvuto

Mbunge wa Kigoma Kusini (CCM), Husna Mwilima, ameomba radhi kufuatia
kauli yake ya kudai idadi kubwa ya watumishi wa kike katika Shirika la
Ndege la Tanzania (ATCL) hawana mvuto, na kudai lengo la kauli yake
ilikuwa ni kushinikiza maboresho kwenye shirika hilo.
Mwilima ametoa kauli hiyo Bungeni jijini Dodoma, leo Novemba 14, 2019,
wakati wa kipindi cha maswali na majibu kwenda kwa Wizara ya TAMISEMI,
ambapo kabla ya kuuliza swali lake aliomba radhi kwa Watanzania.
Mbunge Mwilima amesema kuwa “nilitoa ile kauli lengo lilikuwa ni
kuboresha Shirika letu la Ndege la ATCL, kwa kuwa ile kauli yangu
iliwaboa sana Watanzania hasa wanawake nitumie nafasi hii kuomba radhi
Watanzania hasa wanawake wenzangu”
Mara baada ya kutoa kauli hiyo, Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai alimpongeza na kusema msamaha wake umepokelewa.
Novemba 7, 2019 wakati akichangia kwenye mpango wa maendeleo ya Taifa
Bungeni jijini Dodoma, Mbunge Mwilima alidai kuwa watumishi wanawake
kwenye Shirika la Ndege la ATCL, hawana mvuto na kupelekea kutokuwa na
hamasa kwa wateja.