Serikali yawataka madiwani kutoa majina ya mitaa


Naibu Waziri wa Uchukuzi na
Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye akitoa maelekezo kwa Mhandisi wa
Vodacom, Michael Mjatta (wa kwanza kushoto) wakati wa ziara yake ya
kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwenye kata ya Nyamtukuza
wilayani Kakonko, Kigoma
Naibu Waziri wa Uchukuzi na
Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye akifafanua jambo kwa diwani wa
kata ya Nyabibuye, Stephine Mnigankiko wakati wa ziara yake ya kukagua
upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwenye kata hiyo, Kakonko, Kigoma
Mkuu wa Uendeshaji wa Mfuko wa
Mawasiliano kwa Wote, Albert Richard akitoa taarifa ya upatikanaji wa
huduma za mawasiliano kwa Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano,
Mhandisi Atashasta Nditiye (aliyevaa koti) wakati wa ziara yake Kakonko,
Kigoma ya kukagua huduma hizo
Mhandisi wa Vodacom, Michael
Mjatta (wa kwanza kushoto) akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Uchukuzi
na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (wa nne kulia) kuhusu
upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa wananchi wa kata wa Nyamtukuza,
Kakonko, Kigoma
Naibu Waziri wa Uchukuzi na
Mawasiliano, Mhandisi wa Atashasta Nditiye (katikati) akimsikiliza
diwani wa kata ya Nyamtukuza, Abdallah Magembe, wakati wa ziara yake ya
kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano wilayani Kakonko, Kigoma.
Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Kanali Hosea Maloda
Naibu Waziri wa Uchukuzi na
Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye, aliyesimama mbele katikati,
akiwa kwenye picha ya pamoja na watendaji wa Wilaya za Mkoa wa Kigoma
baada ya kufungua mafunzo ya kujenga uelewa wa kufanikisha utekelezaji
wa mpango wa anwani za makazi na postikodi yaliyofanyika, Kibondo
Na Prisca Ulomi, Kigoma
Serikali imewataka madiwani wote
nchi nzima kutoa majina ya mitaa ili kufanikisha utekelezaji wa mpango
wa anwani za makazi na postikodi.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye wakati akifungua
mafunzo ya kujenga uelewa kuhusu umuhimu na manufaa ya kutekeleza mpango
wa anwani za makazi na postikodi kwa madiwani, viongozi wa Serikali na
watendaji mbali mbali wa Mkoa wa Kigoma yaliyofanyika wilayani Kibondo
yaliyotolewa na wataalamu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
kwa pamoja na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
“Madiwani tupeni majina ya mitaa
ili vifurushi, barua na vipeto viwe vinakwenda moja kwa moja kwa
wananchi, tufanye biashara mtandao na kuimarisha ulinzi na usalama,”
amesema Nditiye.
Ameongeza kuwa biashara mtandao ni
nzuri, tunataka kifurushi cha mtu kiletwe anapoishi na tayari nchi
nzima kata zote zina postikodi, madiwani tupeni majina ya mitaa ili
tuweke vibao na namba za nyumba ili wananchi watambulike
“Unaweza kupata postikodi ya kata
au wadi yako kupitia simu yako ya mkononi kwa kupiga *152*00# kisha
chagua 3 (ajira na utambuzi), 3 (TCRA – Postcode) endelea kufuata
maelekezo hadi kupata postikodi ya kata yako”, amesema Nditiye.
Amefafanua kuwa utekelezaji wa
mpango wa anwani za makazi na postikodi nchi nzima unalenga kuhakikisha
kuwa kila mwananchi anakuwa na anwani yake ya mahali alipo iwe mahali pa
kazi, nyumbani au ofisini ili kuwezesha mwananchi kuhudumiwa kwa
urahisi. 
Ametoa rai kwa madiwani wote nchi
nzima kutoa majina ya mitaa ili Wizara iweze kuweka nguzo zenye majina
ya barabara na namba za nyumba au majengo katika maeneo yao kwa kuwa
tayari kata zote nchi nzima zina postikodi.
Ameeleza kuwa kuna maneno yamezoeleka kuwa Dunia ni kama Kijiji, ili
dunia iweze kuwa kijiji kunategemea uwepo wa mfumo wa utambuzi wa
makazi na wakazi kwa ajili ya kurahisisha utoaji na ufikishaji wa huduma
kwa wananchi ambapo anwani za makazi na postikodi zinawezesha utambuzi
husika na nchi zilizoendelea zilishafika hatua hii na zinaendelea
kunufaika na matunda ya utambuzi husika kijamii na kiuchumi 
Naye Mkuu wa Kanda ya Kati wa
TCRA, Antonio Manyanda wakati akitoa mafunzo hayo amesema kuwa mpango wa
anwani za makazi na postikodi utaongeza ajira kutokana na fursa za
kusambaza bidhaa za wateja katika maeneo yao na mahali walipo;
kurahisisha biashara mtandao hivyo kukuza uchumi; kuongeza mapato ya
Serikali kwa kuwa mamlaka zinazohusika na ukusanyaji wa mapato zitakuwa
na taarifa ya mahali walipo walipa kodi au wananchi hivyo kuwezesha
ukusanyaji wa mapato kwa ufanisi.
Manyanda amezitaja faida nyingine
za mpango huo ni kurahisisha utoaji wa huduma mbali mbali za kijamii
kama vile usajili wa mali, biashara, vizazi na vifo; kuongeza usalama
kwa wananchi kwa kutoa huduma za dharura kwa wakati kwa mfano matukio ya
moto,ugonjwa na uhalifu; kuboresha utendaji wa taasisi mbali mbali kwa
mfano benki kuwa na uhakika wa mahali anapopatikana mteja wakati wa
utoaji na urejeshaji wa mkopo; kurahisisha utambulisho wa watu na mahali
wanapoishi; na kuwezesha utambuzi na mwelekeo na eneo ambalo mtu
anahitaji kwenda 
Wakati akimkaribisha Nditiye,
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kibondo, Ayubu Sebabili amesema kuwa wako
tayari kutekeleza mpango huo ili wananchi waweze kuuza na kununua bidhaa
kutoka ndani nan je ya nchi na kupelekea sehemu nyingine duniani kwa
urahisi na wakati hivyo kuongeza ajira na kipato kwa wananchi

Katika hatua nyingine, Nditiye
amekagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano wilayani Kibondo kwa
kutembelea minara iliyopo kata ya Nyabibuye na Nyamtukuza iliyojengwa na
Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ambapo alielekeza kampuni za simu
za mkononi kuongeza nguvu ya minara hiyo ili iweze kutoa huduma ya data
badala ya sauti pekee kutoka teknolojia ya 2G hadi kufikia teknolojia
ya 3G 

“Maeneo mengi watu walianza na 2G,
tunao waalimu, madaktari, siku hizi kuna wasomi wengi sana vijijini,
nimewaelekeza UCSAF washirikiane na kampuni za simu ili kuhakikisha kuwa
minara iliyopo vijijini inatoa huduma za 3G ili huduma hii itupe fedha
Serikalini kwa kuwa ukitumia data unalipa gharama,” amesema Nditiye
 
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kakonko,
Kanali Hosea Maloda Ndagala amemweleza Nditiye kuwa intaneti ni ndogo
hata mtu akikutumia nyaraka kwa what’s app inachukua muda mrefu
kufunguka
Akiwa ziarani Wilayani Kakonko,
Nditiye ametoa rai kwa viongozi wa Wilaya hiyo kuelimisha wananchi
umuhimu wa kusajili laini za simu kwa alama za vidole na kutekeleza
mpango wa anwani za makazi na postikodi