Lugola: siku za mtu anayejiita kigogo kwenye mitandao ya kijamii zinahesabika

Waziri
wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola, amesema kuwa hivi karibuni Jeshi la
Polisi litamtia nguvuni mtu anayejiita kigogo kupitia ukurasa wa
Twitter.

Ametoa kauli hiyo leo Novemba 2, 2019 katika mkutano na wanahabari
wakati akitoa tathimini ya hali ya usalama hapa nchini kuelekea Uchaguzi
wa Serikali za Mitaa, ambapo amesema kuwa muda si mrefu polisi watamtia
nguvuni mtu huyo.
“Kalenda inazo tarehe, utahesabu mwezi mfupi na mrefu, nataka niwaambie
kwa kifupi siku za huyo Kigogo zinahesabika na hana siku nyingi”,
amesema Waziri Lugola.
Aidha katika hatua nyingine, Waziri Lugola ametoa wito kwa wananchi
kuendelea kuwa na utulivu na amani na kutoa onyo kwa yeyote atakayekuwa
na mpango wa kuvuruga uchaguzi ama kampeni basi atatumbukizwa kwenye
gari lenye maji ya kuwashawasha.
”Niwaonye wanasiasa, siasa za majitaka na lugha ya matusi zinazoudhi
wengine, Jeshi la Polisi limejipanga vizuri ikiwa ni pamoja na
kuwashusha kwenye majukwaa ili wasiendelee kumwaga sumu inayohatarisha
amani kwa wananchi”, amesema.
“Ole wake yule mwenye mpango wa kuvuruga kampeni au uchaguzi
tutamshughulikia, tuna magari ya washawasha, wakorofi na watakaoleta
fujo watawashwawashwa kweli, hatutawamwagia tu bali wakorofi kabisa
tutawatumbukiza na kuwakogesha kwenye hayo maji yanayowashawasha”,
ameongeza Kangi Lugola.