Wananchi 1018 wapatiwa msaada kisheria



Na Stella Kalinga, Simiyu RS

 Msajili
wa Taasisi za watoa huduma za msaada wa kisheria kutoka Wizara ya
Katiba na Sheria, Bi. Felistas Mushi amesema  takribani wananchi 1018 
wamepata huduma ya msaada wa kisheria katika maadhimisho ya wiki ya
msaada wa kisheria tangu Oktoba 21, 2019 mpaka Oktoba 25, 2019,
yaliyofanyika Kitaifa katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi
Mkoani Simiyu.


Mushi
ametoa taarifa hiyo katika Kilele cha Maadhimisho hayo, Oktoba 25, 2019
ambapo amebainisha kuwa asilimia kubwa ya matatizo ya kisheria yalihusu
migogoro ya ardhi na yameshafikishwa mahakamani  na yako katika hatua
mbalimbali.

Amesema
huduma walizopata wananchi katika wiki ya msaada wa kisheria ni pamoja
na huduma za usuluhishi, ushauri wa kisheria, kuandaa nyaraka na
maelekezo ya sehemu  sahihi ya kwenda pindi wanapopata migogoro.

“Mbali
na huduma kwa wananchi mafunzo yametolewa kwa makundi mbalimbali ya
watumishi wa umma wapatao 1300 wakiwemo, wajumbe wa menejimenti ya
sekretarieti ya mkoa, wajumbe wa kamati ya parole, wajumbe wa mabaraza
ya ardhi ya kata na vijiji, wajumbe wa kamati ya maadili ya mahakimu,
askari polisi na magereza, wajumbe wa kamati za shule na watendaji wa
vijiji na kata, “ alisema Mushi.

Kwa
upande wake Hakimu Mary Nyangusi akimwakilisha Hakimu Mkazi Mfawidhi wa
Mahakama ya Wilaya ya Bariadi, Mhe. Mary Mrio, ametoa wito kwa wananchi
kuandika wosia ili kupunguza migogoro ya ardhi ambayo mingi inatokea
mara nyingi wanaume( baba) wanapofariki na wake(mke) na watoto
kudhulumiwa haki zao.

Adam
Kisinza ni Mmoja wa wananchi waliofika kupata msaada wa kisheria katika
maadhimisho hayo amesema, “nashukuru nimeelewesha ninachotakiwa kufanya
maana kule kwetu baba mwenye mji anapokuwa amefariki wakabaki watoto na
mama, wanakuwa hawana mamlaka juu ya mali iliyoachwa maana kila mtu
anataka achukue chake wakati mzee hakuacha hata  wosia”.

Akifunga
Maadhimisho ya Wiki ya Msaada wa Kisheria,Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.
Anthony Mtaka amesema ni vema wizara ya katiba na sheria ikaona umuhimu
wa kupeleka maadhimisho ya wiki ya msaada wa huduma za kisheria katika
maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma hiyo, ili wananchi wapate uelewa wa
masuala ya kisheria na kupata matokeo yatakayoonekana.

Maadhimisho
ya Wiki ya Msaada wa Kisheria Kitaifa mwaka 2019 yanaongozwa na Kauli
Mbiu:- “Msaada wa Kisheria kwa Maendeleo Endelevu”ambapo kilele cha
maadhimisho haya kimeenda sambamba na uzinduzi wa Jarida la Msaada wa
Kisheria, ambalo limezinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony
Mtaka.